MAONI YA MHARIRI: Tuwekeze kwenye afya ya macho

Jana nchi mbalimbali ziliadhimisha Siku ya Afya ya Macho Duniani, ambayo kwa mwaka huu imebebwa na kauli mbiu isemayo: Afya ya macho kwa wote.

Taarifa zinaonyesha kwamba, siku hii ilianza kuadhimishwa mwaka 1998 kutokana na pendekezo la taasisi ya Lions Club Foundation.

Ni pendekezo ambalo baadaye liliungwa mkono na wadau mbalimbali wa afya, likiwamo Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), muungano wa mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na huduma za macho, serikali za nchi mbalimbali, wataalamu wa masuala ya afya, taasisi na watu binafsi.

Kwa Watanzania, tunapoadhimisha siku hii tunapaswa kujiuliza maswali kadhaa, likiwamo kubwa la kuongezeka kwa watu wenye upofu na matatizo ya uoni hafifu.

Miaka ya zamani ungeweza kuhesabu watu wanaotumia miwani katika maeneo kama vile shuleni, vyuoni, ofisini na katika mikusanyiko mingine. Lakini leo inashangaza kuona kuwa hata watoto chini ya miaka saba wanavaa miwani tena ya lensi kali.

Huu ni mfano mdogo wa kuonyesha ukubwa wa tatizo ambalo kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii Jinsia, Wazee na Watoto linaweza kuzuilika.

Taarifa hiyo inabainisha kuwa asilimia moja (takriban watu 573,000) ya Watanzania hawaoni kabisa, huku wenye matatizo ya kuona kwa viwango mbalimbali hapa wakikadiriwa kuwa ni mara tatu ya watu wasioona ambao ni takriban watu 1,730,000.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya ya macho, sababu zinazochangia matatizo ya macho ni pamoja na tatizo la retina litokanalo na ugonjwa wa kisukari na umri mkubwa; upofu wa utotoni utokanao na upungufu wa Vitamini A, mtoto wa jicho, maambukizi ya surua na maambukizi ya kisonono kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Sababu nyingine ni makovu kwenye kioo cha jicho, upungufu wa upeo wa macho kuona na uoni hafifu, trakoma/vikope, mtoto wa jicho na shinikizo la jicho.

Sababu hizi zinaweza kuepukika ikiwa Taifa na kila mmoja kwa nafasi yake atathamini afya ya macho yake. Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa, katika kila watu watano wenye tatizo la kuona, wanne walipata tatizo hilo kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika.

Wengi hatujali afya ya macho yetu na ndio maana ni wachache wenye taratibu za kupima macho angalau mara moja kwa mwaka.

Kitaifa, tunaisihi Serikali na wadau wengine kulivalia njuga suala hili hasa kipindi hiki tunapoelekea mwishoni mwa utekelezaji wa dira ya kutokomeza upofu unaozuilika ifikapo mwaka 2020.

Miongoni mwa mambo ambayo Serikali inaweza kufanya ni pamoja na kuongeza bajeti katika eneo hili, kuongeza wataalamu na vifaa tiba na kuhakikisha huduma za afya ya macho zinatolewa katika ngazi mbalimbali za mfumo wa afya nchini.

Tanzania mpya ya viwanda na yenye dhamira ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2015, inahitaji pamoja na mambo megine nguvu kazi ya watu wenye afya bora.

Afya ya macho ni muhimu kwa nguvu kazi hii. Kuendelea kulipa kisogo tatizo la afya ya macho, kutafifisha dhamira na jitihada za kuiendeleza nchi yetu.