MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Uainishaji wa maneno katika Kiswahili

Muktasari:

  • Kumekuwa na kutofautiana miongoni mwa wataalamu kuhusu uainishaji na idadi ya maneno.
  • Baadhi ya wataalamu wanataja aina saba za maneno ilhali wengine wanataja aina nane.

Uainishaji wa maneno ni dhana inayorejelea kupanga kategoria za kisarufi ambapo maneno ya lugha fulani huwekwa kutegemea na dhima zake kisarufi.

Kumekuwa na kutofautiana miongoni mwa wataalamu kuhusu uainishaji na idadi ya maneno.

Baadhi ya wataalamu wanataja aina saba za maneno ilhali wengine wanataja aina nane.

Lengo letu katika makala haya si kuonyesha tofauti hizo baina ya wataalamu, bali kuonyesha uainishaji huo unavyowakanganya baadhi ya wanafunzi katika kiwango cha sekondari na namna ya kutanzua tatizo linalowakabili.

Kwa kawaida katika lugha maneno tayari yamewekwa katika kategoria mbalimbali. Mathalani maneno kama Jumatatu, yule, mrefu na mengineyo; kupitia aina za maneno tulizo nazo ni rahisi kubaini kuwa yanaingia katika kategoria zipi.

Aidha, maneno hayo yanapotumiwa katika tungo kutegemeana na miktadha ya anuwai ya utumizi, huweza kubadili kategoria.

Neno ambalo linaweza kutumiwa katika tungo kama nomino, linaweza kubadilika na kuwa kivumishi au aina nyingine ya neno.

Hili ndilo tatizo linalowakabili baadhi ya wanafunzi. Wapo wanafunzi ambao wakishakariri kwamba neno fulani ni nomino, basi popote linapotumika hulichukulia hivyo.

Jambo la msingi la kuzingatiwa na wanafunzi na wachambuzi wengine wa lugha ni kwamba, kigezo kikubwa cha uainishaji wa maneno katika lugha ni namna maneno hayo yanavyofanya kazi katika tungo husika.

Kwa sababu hiyo, yapo baadhi ya maneno katika lugha ambayo huwapa shida wanafunzi kuyaainisha yanapotumiwa katika miktadha mbalimbali.

Katika kufanya hivyo, makala haya tutaangalia baadhi ya maneno ambayo huwatatiza wengi. Uanishaji huo utafanyika kupitia sentensi teule kama ifuatavyo:

i). Mtoto huyu ni mwema. Katika sentensi hii wanafunzi wengi wanapopewa tungo yenye muundo huo kuainisha, neno ‘ni’ huliainisha kama kiunganishi (U) lakini katika uhalisia neno hilo si kiunganishi bali ni kitenzi kishirikishi (t) ambacho huonyesha tabia au hali ya mtoto anayezungumziwa.

ii). Mtoto aliyetumwa sokoni hajarudi. Baadhi ya wanafunzi wakipewa tungo kama hiyo ili waainishe neno lililopigiwa mstari, watasema ni kitenzi kisaidizi. Neno hilo si kitenzi bali ni kivumishi (V) kwa kuwa hufafanua zaidi kuhusu nomino mtoto.

iii). Wewe u mwema. Neno hili ‘u’ ni kitenzi kishirikishi (t) kinachoonyesha tabia. Siyo kihisishi (H) kama baadhi ya wanafunzi wanavyoainisha.

iv). Neema angali mgonjwa. Neno lililopigiwa mstari ni kitenzi kishirikishi (t) siyo kiunganishi. Hata hivyo, neno hilo likitumiwa tofauti huweza kuingia katika kategoria nyingine.

Kwa mfano: Mwalimu angali anasimamia wanafunzi katika usafi. Neno ‘angali’ katika tungo hii si kitenzi kishirikishi kama ilivyo katika sentensi iliyotangulia bali ni kitenzi kisaidizi ambacho kimetumika sambamba na kitenzi kikuu (anasimamia) ili kukamilisha ujumbe.

v). Wanafunzi walikuwa darasani. Neno ‘walikuwa’ katika tungo hii limetumika kama kitenzi kishirikishi (t) lakini linaweza pia kutumika kama kitenzi kisaidizi likitumiwa kwa namna tofauti mathalani, wanafunzi walikuwa wanacheza mpira. Neno ‘walikuwa’ ni kitenzi kisaidizi ilhali ‘wanacheza’ ni kitenzi kikuu.

Mpenzi msomaji, tunatoa msisitizo kuwa maneno huainishwa kulingana na yanavyotumiwa katika tungo husika. Ni vyema kuyachunguza kwa makini maneno katika tungo na kubaini uhusiano wake ili kujua kategoria ya neno kuliko kufanya uainishaji kwa kukariri maneno katika kategoria zilizopo.