MBALAMWEZI YA KISWAHILI: Matumizi ya mofimu katika Kiswahili

Matumizi ya sarufi ni miongoni mwa mada zinazowatatiza wanafunzi katika shule za sekondari.

Makala haya yatashughulikia baadhi ya vipengele vinavyojitokeza katika mada hii. Hata hivyo, uchambuzi huu ni mahususi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wanafunzi wa sekondari.

Mofimu ni kipashio kidogo cha kimofolojia chenye maana kisarufi au kileksika. Mofimu zenye maana kileksika ni zile ambazo haziambatishwi kipashio kingine chochote.

Mfano wa mofimu hizo ni babu, hodari na Mungu. Hizi ni mofimu zisizo na maana kamili kwa namna zilivyo wala hazihitaji kuongezewa mofimu nyingine ili kuleta maana.

Mofimu zenye maana kisarufi ni zile zinazoambatishwa mofimu nyingine ili kuunda maneno kamili. Mfano wa mofimu hizo ni tu-na-som-a, na a-li-li-a.

Mofimu zina dhima mbalimbali katika lugha. Aidha, mofimu moja inaweza kuwa na dhima zaidi ya moja kulingana na inavyotumika.

Katika mjadala huu tutaangalia mofimu zenye maana kisarufi.  Kwa kuanza leo hii tuangalie matumizi ya mofimu ‘ki’, ‘ku’ na ‘ni’.

Yafuatayo ni baadhi ya matumizi ya mofimu ‘ki’:

i). Hutumika kudogesha. Mfano: kitoto, kimeza; ‘ki’ iliyopigiwa mstari imetumika kuonyesha dhana ya udogo. Maneno ‘mtoto’ na ‘meza’ ndiyo yaliyojengewa dhana ya udogo.

ii). Kuunda mzizi wa kitenzi. Mfano: kimbia, kinga; ‘ki’ hapo ni sehemu ya mizizi ya vitenzi ambavyo ni -kimbi- na -king-.

iii). Huonyesha idadi. Mfano: kijiji, kitabu; ‘ki’ imetumika kuonyesha idadi ambayo ni umoja. Maneno mawili yaliyotolewa mifano yapo katika umoja.

iv). Huonyesha upatanishi wa kisarufi. Kuwiana kwa viambishi vya maneno katika tungo ndiko kunakorejelewa kama upatanishi wa kisarufi. Mfano: kiatu kimechakaa.

v). Kuonyesha mtendwa katika tungo. Mfano: anachokipenda; katika tungo hii ‘ki’ inaonyesha kitendwa; yaani kitu kinachopendwa huweza kuwa kiatu, chakula n.k.

vi). Kuonyesha nafsi ya tatu umoja. Mfano: kikikipenda; ‘ki’ iliyopigiwa mstari inaoneha nafsi ya tatu ya mtenda/kitenda.

Baada ya kuangalia ‘ki’,  sasa tuangalie matumizi ya mofimu ‘ku’:

i). Huonyesha wakati uliopita. Mfano: Mgonjwa hakula. ‘ku’ imetumika kama njeo ya wakati uliopita.

ii).Hutumika kuunda kitenzi nomino/kitenzi jina. Mfano:  kucheza, kusoma; ‘ku’ iliyopigiwa mstari inaunda vitenzi jina hivyo.

iii). Hujenga shina la neno lenye mzizi wa silabi moja. Mfano: kufa, kula, kuja

iv). Huunda ngeli ya KU. Mfano: Kucheka kunaongeza afya.

v). Kuonyesha mtendwa wa nafsi ya pili umoja. Mfano: anakusalimia. Anayesalimiwa ni mtendwa wa nafsi ya pili ‘wewe’.

vi). Husaidia shina la kitenzi la silabi moja kubeba mofimu ya wakati. Mfano: Hakufa

vii). Hutumika kuunda mzizi wa kitenzi. Mfano: kuna, kumba, kumbuka; mizizi ya vitenzi hivyo ni -kun-, -kumb- na -kumbuk-.

Aidha, mofimu ‘ni’ ina dhima zifuatazo:

i). Huonyesha mahali ambapo tukio hutendeka. Mfano: Wanafunzi wamo ofisini.

ii). Hutumika kuonyesha urejeshi wa mtendwa. Mfano: Ananisaidia. Anayetendwa ni nafsi ya kwanza umoja mimi ambaye huwakilishwa na ‘ni’.

iii). Kuonyesha nafsi ya kwanza umoja Mfano: Nina kalamu iv). Hutumika kuonyesha idadi (umoja). Mfano: Ninacheza