Miaka 15 ya MDGS inayoyoma bila dawa ya kumaliza umaskini

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) nchi maskini zaidi duniani ni zile zenye viashiria hafifu vya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na maendeleo ya binadamu. Picha na maktaba

Muktasari:

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) nchi maskini zaidi duniani ni zile zenye viashiria hafifu vya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na maendeleo ya binadamu.

Dar es Salaam. Tanzania ni kati ya nchi 48 zinazotajwa kuwa maskini sana duniani licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) nchi maskini zaidi duniani ni zile zenye viashiria hafifu vya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na maendeleo ya binadamu.

Katika kundi hilo, Afrika inazo nchi 34 ambazo ni Tanzania, Angola, Benin, Burkina Faso, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Djibouti, Equatorial Guinea, Eritrea.

Ethiopia, Gambia, Guinea Guinea-Bissau, Lesotho Liberia Madagascar, Malawi, Mali Mauritania, Msumbiji, Niger, Rwanda, Sao Tomé na Príncipe, Senegal, Sierra Leone, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Togo, Uganda, Zambia.

Asia, inazo nchi tisa ambazo ni Afghanistan, Bhutan, Bangladesh, Cambodia, East Timor, Laos, Myanmar, Nepal, Yemen.

Nchi nyingine ni visiwa vya Kiribati, Solomon, Tuvalu na Vanuatu huku Amerika Kaskazini ikiwa na Haiti ambayo idadi kubwa ya wakazi wake ni wenye asili ya Afrika.

Kutokana na ufa kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea kuwa kubwa, mwaka 2000 UN iliandaa mkutano uliolenga kuziinua nchi maskini kiuchumi na kijamii.

Mkutano huo ndiyo uliozaa Malengo ya Milenia (MDGs) na nchi 189, ikiwamo Tanzania, zilitia saini na kuahidi kuyatimiza ifikapo mwaka 2015.

Malengo hayo ni pamoja kutokomeza umasikini uliokithiri, njaa, elimu ya msingi kwa wote, kuwawezesha wanawake kuwa na usawa kati yao na wanaume, kupunguza vifo vya watoto walio chini ya umri chini ya miaka mitano kwa theluthi moja na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa robo tatu.

Mengine ni kuzuia kuenea kwa magonjwa yanayoua hasa virusi vya Ukimwi, Ukimwi na malaria, utunzaji wa mazingira na kuanzisha uhusiano wa kimataifa ili kushughulikia misaada, biashara na misamaha ya madeni.

Nafasi ya Tanzania

Wakati ukiwa umebaki mwaka mmoja tu wa kutekeleza ahadi ya utekelezaji wa malengo ya milenia, hali siyo nzuri kwani umasikini bado umetamalaki.

Tanzania imekuwa ikitekeleza Malengo ya Milenia kupitia sera na mikakati ya Taifa kama vile, Dira ya Taifa ya 2025, Dira ya Zanzibar ya hadi 2020, Mkukuta, Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu (2010 – 2025) na Mpango wa Maendeleo wa kati (2010- 2015; 2015-2025).

Tathmini ya Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) ambayo imepewa jukumu na Ofisi ya Rais- Tume ya Mipango kuendesha na kusimamia mjadala kuhusu ajenda ya maendeleo baada ya malengo ya milenia, inayoonyesha kuwa Tanzania haitaweza kutekeleza baadhi ya malengo ifikapo 2015.

Akizungumzia utekelezaji, mafanikio na changamoto za malengo hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam, mtafiti wa uchumi wa taasisi hiyo, Dk Oswald Mashindano anasema bado umaskini umetamalaki.

“Umaskini wa huduma muhimu umepungua toka asilimia 39 mwaka 1990 kwenda asilimia 36 mwaka 2000,” anasema.

Mwaka 2008 ulikuwa asilimia 34 na mwaka 2013 ulikuwa asilimia 28.2. Lengo ni kufikia asilimia 19.5 ifikapo 2015,” anasema Dk Mashindano.

“Bahati mbaya umaskini umepungua nchini kwa kiasi kidogo ukilinganisha na kukua kwa pato la taifa. Hili ndilo tatizo kubwa linaloonekana kuathiri ustawi wa jamii yetu.”

Anafafanua kuwa malengo mengine ni pamoja uandikishaji wa watoto katika shule za msingi, akisema umeongezeka kutoka asilimia 54 mwaka 1990 na kufikia asilimia 97 mwaka 2008, wakati lengo lilikuwa ni kufikia asilimia 100.

“Vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka watoto 115 katika 1,000 mwaka 1990 kwenda 99 na kuwa 68 kati ya watoto 1,000 mwaka 2008 wakati lengo lilikuwa kufikia 38 kwa 1,000 mwaka 2015,” anasema.

“Matokeo ya tathmini ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia zilizofanyika mwaka 2008 hadi 2010 yanaonyesha wazi kuwa Tanzania, kama nchi nyingine zinazoendelea, haitaweza kufikia baadhi ya malengo hayo ifikapo 2015.”

Kwa nini malengo hayatekelezeki?

Akitaja sababu ya kutofikia malengo hayo, Dk Mashindano anasema ni kutokana na kutowashirikisha kikamilifu watendaji wa ngazi za chini kama vile halmashauri, kata na vijiji katika uandaaji wa mipango, bajeti na utekelezaji.

“Kutoshirikishwa kikamilifu watendaji katika ngazi za msingi kama halmashauri, kati na vijiji kwa mfano utayarishaji wa mipango, uandaaji wa bajeti na utekelezaji,” anasema.

“Kutowajengea uwezo wa utendaji wadau au watendaji katika ngazi za chini au katika ngazi za msingi kama vile halmashauri, kata na vijiji.”

Mkurugenzi mtendaji wa ESRF, Dk Hoseana Lunogelo anasema kwa kuwa malengo hayo hayakuwashirikisha zaidi wananchi, mkakati wa sasa ni kuchukua maoni ya wananchi kabla ya kupeleka taarifa UN.

“Malengo haya ya milenia yalipangwa na UN yalipangwa bila kuwashirikisha wananchi, hivyo kwa sasa mkakati uliopo ni kukusanya maoni ya wananchi ili kujua vipaumbele vyao,” anasema.

“Kwa mfano katika elimu ya msingi, tulishakuwa tumefikia malengo, hivyo wangeshirikisha wananchi wangepata sehemu zenye matatizo zaidi.

“ESRF imepewa jukumu na Ofisi ya Rais- Tume ya Mipango la kuongoza na kusimamia majadiliano ya wadau kitaifa kuhusu mchakato wa maendeleo baada ya kufikia kipindi cha malengo ya milenia mwaka 2015.”

Mikakati

Baada ya kugundua upungufu uliojitokeza katika utekelezaji wa Malengo ya Milenia, hatua kadhaa zimechukuliwa na Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na wafadhili.

Dk. Oswald Mashindano anasema mkakati uliopo ni kuanzishwa kwa mradi wa matumizi ya teknolojia ya habari kwa lengo la kusaidia kufikisha malengo hayo ngazi za chini. Mradi huo umeanzishwa mwaka 2011 katika wilaya nne ambazo ni Bukoba Vijijini, Bunda, Morogoro Vijijini na Uyui. “Lengo la mradi huu lilikuwa ni kusaidia kuyafikisha Malengo ya Milenia kwenye ngazi ya chini kwa kuboresha matumizi ya teknolojia ya mawasiliano katika sekta ya afya, mazingira, uvuvi na kilimo,” anasema Dk Mashindano.

Anataja mradi mwingine wa kuharakisha matokeo ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia ulioanzishwa katika wilaya za Bukoba vijijini na Bunda.

“Lengo la mradi huo lilikuwa kuharakisha utekelezaji na kufikia Malengo ya Milenia kwa kuwashirikisha na kuwajengea uwezo watendaji katika ngazi za chini,” anasema. Mradi mwingine ni wa kuhimiza masuala ya umaskini, mazingira na jinsia katika uandaaji wa mipango na bajeti katika ngazi za halmashauri, kata na vijiji.

“Kuna miradi inayolenga kujenga uwezo wa Halmashauri, kata na vijiji katika kutekeleza miradi kwa kuingiza masuala ya umasikini, mazingira na jinsia katika mipango ya bajeti kwa ngazi za halmashaur, kata na vijiji,” anasema na kuongeza:

“Miradi hiyo itaanaza kutekelezwa katika wilaya sita ambazo ni Nyasa, Sengerema, Bunda, Bukoba na Ileje. Wilaya hizo zimechaguliwa kwa vigezo vya kuwa na umasikini, utofauti wa jinsia mwenendo wa uharibifu na thari za mabadiliko ya tabia nchi.”

Hata hivyo, Dk. Mashindano anasema Tanzania kama moja ya nchi zilizo chini ya UN , zimeonyesha nia kubwa kushirikisha kikamilifu watendaji katika ngazi za chini kutekeleza ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015.