MLND: Ugonjwa hatari wa mahindi

Muktasari:

Ugonjwa huu umeanza kuua matumaini ya wakulima katika harakati za kuendeleza kilimo cha mahindi kama zao kuu la chakula.

Ugonjwa hatari wa mahindi ujulikanao kwa jina la kitaalamu “Maize Lethal Necrosis Disease” umethibitika kuwepo nchini Tanzania.

Ugonjwa huu umeanza kuua matumaini ya wakulima katika harakati za kuendeleza kilimo cha mahindi kama zao kuu la chakula.

Taarifa mbalimbali zinaeleza kuwa ugonjwa huo ulianzia huko nchini Marekani mwaka 1976 na kuingia nchini Kenya mwaka 2011.

Aidha, mnamo mwaka 2012 ulianza kuonekana rasmi nchini Tanzania huku ikiathiri maeneo machache na kukithiri kwa kiasi kikubwa katika wilaya ya Babati mkoani Manyara na Simiyu mkoani Shinyanga.

Hadi katikati mwa mwaka 2015, ugonjwa huu umebainika kuwepo katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mwanza na Mara.

Chanzo cha ugonjwa

Wataalamu katika tafiti zao wanasema kuwa, ugonjwa huu husababishwa na virusi vya aina mbili vinavyoathiri mmea wa mahindi kwa pamoja ambavyo ni Maize Chlorotic Mottle Virus (MCMV) na Sugarcane Mosaic Virus (SCMV).

Virusi hivi husambazwa na wadudu wa aina mbili, ambao ni Thrips na Aphids, japo kuna wadudu wengine wanaweza kubeba na kusambaza ugonjwa huo kama vile beetles and leafhoppers pamoja na matumizi ya mbegu zilizoathirika.

Mahindi yanavyoathirika

Ugonjwa huu huathiri mahindi katika hatua zake zote za ukuaji. Dalili zikianza kuonekana katika shina la jani hadi kwenye ncha ya jani kama ifuatavyo;

Majani machanga ya juu hugeuka na kuwa na rangi ya njano na hatimaye kukauka kuanzia pembezoni mwa jani kuelekea katikati na hatimaye mmea kufa.

Mmea huweza kutoa machipukizi mengi sana. Mbelewele hukosa chamvua hivyo mmea kutozaa. Mahindi yakishambuliwa wakati yanajaza mbegu, gunzi husinyaa na kuweka mbegu chache au kutojaza kabisa.

Mahindi yaliyoathirika hushambuliwa na magonjwa nyemelezi hasa ukungu. Kwa mimea iliyoanza kusinyaa huonyesha dalili za kukomaa kabla ya wakati, huku hindi likiwa katika hali ya kuchoma maganda na kuonyesha utayari wa kuvunwa.

Aidha, ugonjwa huo unaposhambulia katika hindi lililokomaa, huingia moja kwa moja katika kiini cha punje.

Mahindi yaliyoathiriwa na ugonjwa huu huota fangasi ambayo wataalamu wanasema ina sumu kali ijulikanayo kama Aflatoxin. Sumu hiyo, husababisha madhara kwa binadamu na wanyama.

Madhara

Utafiti uliofanywa na wataalamu mbalimbali wakiwamo wale wa Taasisi ya utafiti wa Kilimo ya Seliani (SARI) wamebaini kuwa sumu hiyo (Aflatoxin) inayotokana na fangasi husababisha ugonjwa wa saratani ya ini kwa binadamu na wanyama.

Utafiti huo pia unaeleza kuwa ugonjwa huo unaweza usionekane kwa haraka na huweza hata kuchukua muda wa mwaka ndipo kujitokeza.

Hivyo basi, ni lazima mataifa yote kuwa makini na kuchukulia jambo hili kwa uzito zaidi.

Mbinu za kuepuka ugonjwa huu

Panda mbegu bora zilizothibitishwa na Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI) nchini. Usipande mbegu zilizovunwa msimu uliopita kutoka katika shamba lililoshambuliwa na ugonjwa.

Safisha shamba kwa kuondoa magugu na masalia yote ya mazao na kuyachoma/kuyafukia kuepuka maficho ya wadudu na virusi vya ugonjwa. Kagua shamba mara kwa mara na kama utaona dalili zilizotajwa hapo juu, toa taarifa kwa mtaalamu wa kilimo aliye karibu nawe.

Makala haya kwa hisani ya mkulimambunifu. www.mkulimambunifu.org