MSD inahitaji mshindani ili kuongeza ufanisi, kuboresha huduma

Muktasari:

  • Baada ya kuagiza dawa, vifaa, vifaa tiba na vitenganishi kutoka kwa wazalishaji ambao wanaweza kuwa wa ndani au nje ya nchi, ofisi za kanda na vituo vya mauzo vina wajibu wa kuzipokea kutoka MSD makao makuu siku 14 tangu ziagizwe.

Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ina majukumu ya kununua, kutunza, kusambaza dawa, vifaa, vifaa tiba na vitenganishi nchini. Ndio mamlaka pekee yenye jukumu hilo.

Baada ya kuagiza dawa, vifaa, vifaa tiba na vitenganishi kutoka kwa wazalishaji ambao wanaweza kuwa wa ndani au nje ya nchi, ofisi za kanda na vituo vya mauzo vina wajibu wa kuzipokea kutoka MSD makao makuu siku 14 tangu ziagizwe.

Hospitali za halmashauri na vituo vya afya hutuma maombi kila baada ya miezi mitatu au robo mwaka na kupatiwa mahitaji yao kutoka ofisi za bohari za kanda. Mfumo wa kuwasilisha bidhaa kwa wahitaji huanzia makau makuu ya bohari na baada ya hapo kuwasilishwa hospitali za rufaa, mikoa na kanda pamoja na wilaya.

Hospitali za halmashauri huwasilisha bidhaa katika zahanati na vituo vya afya vya umma na vile za asasi zisizo za serikali (Azise).

Mwaka 2013 MSD ilianzisha utaratibu wa kupeleka dawa na vifaa tiba kwenye kituo cha kutolea huduma za afya. Pamoja na mambo mengine, lengo la utaratibu huo lilikuwa kupunguza mlolongo mrefu na usio na tija kwa wahitaji.

Pamoja na MSD kuhudumu peke yake katika ununuzi, utunzaji na usambazaji wa dawa na vifaa tiba zipo changamoto kadhaa ambazo zinaikabili. Moja ya changamoto ambayo kimsingi ndio kubwa ni ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa wakati muafaka.

Mchakato wa uagizaji wa dawa hadi kufika kwa wahusika huchukua muda mrefu. Hii inasababishwa na MSD kwa upande mmoja na watendaji kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa upande mwingine.

Baadhi wa watendaji kwenye vituo vya kutolea huduma za afya huchelewa kutuma maombi MSD. Wengine husubiri mpaka dawa au vifaa tiba viishe ndipo waagize. Utaratibu huu husababisha dawa na vifaatiba muhimu kukosekana vituoni hivyo kuhatarisha maisha ya wagonjwa.

Changamoto nyingine ni baadhi ya wafamasia kuchelewa kutuma maombi wanayopokea kutoka kwa wahitaji kwenda MSD. Pamoja na maboresho yanayofanywa na MSD ikiwamo kutuma maombi kwa njia ya mtandao, upatikanaji wa dawa umeendelea kuwa changamoto.

Licha ya kuchelewa kusambaza dawa, MSD inakabiliwa na upungufu wa dawa za aina mbalimbali. Hata hivyo kituo cha kutolea huduma ya afya hakiruhusiwi kununua dawa kutoka kwa mtoa huduma mwingine bila kibali cha MSD kuthibitisha kukosa bidhaa hiyo.

Hata hivyo kituo cha kutolea huduma ya afya hulazimika kufuata utaratibu wa ununuzi wa umma ili kumpata mtoa huduma mwingine wa vifaa na dawa. Wakati mwingine vikao vya bodi ya ununuzi huchukua muda kuketi na kutoa maamuzi hivyo kusababisha wananchi kukosa huduma waliyoitarajia kwa muda muafaka.

Ukosefu wa dawa, vifaa, na vifaa tiba katika vituo vya afya umeendelea kuwa kero kwa wananchi hasa masikini na wanyonge. Mwaka 2015/2016 Serikali ilikuwa inadaiwa takribani Sh108 bilioni na MSD ingawa imeendelea kulipa deni hilo na kuiwezesha bohari. Hata hivyo, vituo vingi vya afya navyo vinaidai MSD dawa, vifaa, vifaa tiba na vitenganishi.

Kutokana na wananchi kuendelea kuteseka na wakati mwingine kupoteza maisha, ni wakati wa Serikali ama kuiboresha MSD kwa kuitengea fedha za kutosha kutekeleza shughuli zake kadri ya mahitaji au kubadilisha sheria na kuitafutia MSD mshindani wa kutoa huduma hiyo.

Kuendelea kubaki peke yake sokoni kunasababisha huduma kuwa duni. Kama Serikali itaamua kuachia eneo hili kuwa huru, ni vyema ikaweka udhibiti kuhakikisha dawa na vifaa vinavyoingizwa vinakidhi vigezo.

Hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitenganishi katika vituo vya kutolea huduma za afya si ya kuridhisha. Wananchi wameendelea kuteseka kwa kukosa huduma hii muhimu ambayo pengine ingetakiwa kuwa kipaumbele namba moja cha Serikali.

Kama Serikali inaona hakuna umuhimu wa kuitafutia MSD mshindani inapaswa kuielekezea nguvu nyingi ikiwamo kuipatia rasilimali fedha, vifaa kama magari na pikipiki na mahitaji mengine ili kuporesha mfumo wa ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa.

Haya yote yafanyike lengo kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya zilizoboreshwa na kwa wakati stahiki.

Mwandishi ni Mtakwimu na Ofisa Mipango.