MTAZAMO: Itatubidi tu tuishangilie Uganda Fainali za Afcon 2017

Natumai ungekuwepo Zambia, ungeona jinsi watu walivyokuwa wakishangilia kama wendawazimu, furaha ilipitiliza, watu wengine walipoteza maisha, watu hawakulala kwa siku kadhaa, jezi na alama mbalimbali za Zambia zilitawala, ilikuwa ni furaha kila mahali kuanzia maeneo ya starehe, mitaani kwenye maofisi, sehemu za biashara majumbani,” hayo yalikuwa ni maneno ya rafiki yangu, Elias Chipepo mwandishi wa habari za michezo nchini Zambia anayefanya kazi katika gazeti la Serikali la Times aliniambia hayo mwezi Machi mwaka 2012.

Chipepo alikuwa akinisimulia kilichotokea nchini Zambia tangu timu hiyo ilipotwaa ubingwa wa Fainali za 28 za Afrika zilizofanyika Gabon na Guinea ya Ikweta 2012.

Mwandishi mwingine wa Zambia wa kituo cha televisheni cha MUVI, Modern Sinkala yeye nilikuwa nikiwasiliana naye kabla kikosi cha Zambia ‘Chipolopolo’ hakijaondoka Zambia kwenda kwenye fainali hizo za Afrika.

Kabla Chipolopolo hawajakwenda Afrika Kusini kwa ajili ya kambi aliniambia ana uhakika watakapokwenda Guinea ya Ikweta/Gabon watarudi na kombe.

Sinkala alikuwa akisema hayo kwa sababu mbili, kwanza alikuwa ana uhakika wa wachezaji wa Zambia wanaotumia akili, uzalendo na wenye lengo moja la kuleta ushindi, lakini pia alikuwa ametoka nchini Botswana, ambapo tulikuwa naye pamoja na Elias Chipepo tukishuhudia Zambia ikitwaa ubingwa wa vijana chini ya miaka 20 kwa nchi za Kusini mwa Afrika (COSAFA) huku Tanzania iliyokuwa timu alikwa ikitolewa katika hatua ya makundi.

Zambia ni majirani zetu tunaopakana nao, lakini ukiacha wao kupata nafasi ya kushiriki Fainali za Afrika mara 15, Zambia imetwaa ubingwa wa Afrika 2012 na wachezaji wao kupata mafanikio na maisha mazuri.

Wachezaji wa Zambia hawana tofauti na wachezaji wa Tanzania, ila wachezaji wetu wanakosa umoja, uzalendo, akili ya mchezo, shauku ya ushindi na wanataka njia ya mkato.

Wachezaji wa Tanzania wana vipaji, hata hivyo siku zote wachezaji wenye vipaji vikubwa na hawafanyi jitihada hawaendelei, ila wale wasiojaliwa kuwa na vipaji, lakini wanafanya jitihada, watakwenda mbele na kupata mafanikio.

Ikumbukwe kwamba tunapozungumzia mchezo wa soka tunaongelea wachezaji soka na siyo siasa zinazouzunguka mchezo wa soka na ndiyo maana siku zote wachezaji wetu ndiyo wamekuwa tatizo la maendeleo ya soka letu.

Inavyoonekana ni kwamba wachezaji wa Tanzania hawaoni umuhimu wa kujituma, juhudi, hawana dhamira ya dhati ya kufanikiwa katika soka, hawana uzalendo wa kulipigania Taifa, hawataki kuacha ubinafsi na kutafuta ushindi kwa lengo moja ili tufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika au Fainali za Kombe la Dunia. Ni wazi kuwa wachezaji wetu wa Tanzania wanasahau kwamba soka ya Afrika mazingira yake yanafanana, hakuna mtoto wa waziri anayecheza soka, wala hakuna mtoto wa mwanasheria au mfanyakazi wa benki ambaye anacheza soka, soka inachezwa na watu wanaotoka kwenye familia duni na hilo ndiyo daraja la kuelekea maisha mazuri kama waliyopata Zambia 2012 na kama itakavyopata nchi itakayotwaa ubingwa wa Afcon 2017.

Ninasema hivyo kwa sababu Fainali za Afrika (Afcon 2017) zinaanza mwishoni mwa wiki hii Januari 14 na zinatarajiwa kumalizika Februari 5 huku Ukanda wa Afrika Mashariki ukiwakilishwa na Uganda.

Tunawashuhudia jirani zetu Uganda wakiwania ubingwa wa Afrika wakati sisi tumekuwa tukifanya vibaya.

Wachezaji wetu wanatuangusha na sisi tunaona ni sawa wakati tunatakiwa kujiuliza mengi. Mimi nitazishangilia Senegal, Algeria na Uganda katika AFCON 2017.

Ushauri na maoni piga na sms simu: 0652 254845