Maajabu ya biashara ya maandazi, vitumbua darasani

Muktasari:

  • Japo biashara hizo ndizo anazotegemea kimaisha, lakini hafurahishwi nazo, kwani anaamini kama angepata fursa ya kusoma hadi chuo kikuu, pengine leo hii asingekuwa muuza maandazi na vitumbua.

Kwa Adelina Stephano, mkazi wa Bukoba vijijini mkoani Kagera, upishi wa maandazi na vitumbua na wakati mwingine kuchoma mahindi, ndizo biashara zinazomwingizia kipato cha kila siku.

Japo biashara hizo ndizo anazotegemea kimaisha, lakini hafurahishwi nazo, kwani anaamini kama angepata fursa ya kusoma hadi chuo kikuu, pengine leo hii asingekuwa muuza maandazi na vitumbua.

“ Elimu yangu ni darasa la saba siyo kwamba sikupenda kuendelea na masomo lakini wazazi wangu hawakuwa na uwezo wa kunilipia ada, hivyo nimejikuta naishia kumudu shughuli hizi ndogo ndogo,” anasema.

Uzoefu wa maisha aliopitia Adelina ambaye pia ni maarufu kwa jina la Kokushubila, umempa hamasa ya kuwekeza katika elimu ya watoto wake watatu.

Unaweza kushangaa biashara anazofanya, lakini ari na hamasa ya kuwekeza kwenye elimu, vimemfanya awe tayari kulipa ada ya Sh1,612,000 kwa mwaka ili mwanawe Derick Mbezi asome katika shule anayosema inafanya vizuri kitaaluma.

Alifikia uamuzi huo baada ya kutambua kuwa elimu ni mtaji, hivyo amekuwa akihangaika kusaka ada kupitia shughuli zake za biashara ndogondogo.

Matokeo yampa furaha

Kama Wahenga wanavyosema; “penye nia pana njia” ndivyo ilivyotokea kwa Adelina, kwani nia yake imeanza kufanikiwa. Sasa ana furaha baada ya mwanawe huyo anayesoma katika Shule ya Msingi Rweikiza kupata wastani wa alama A.

Shule hii ni miongoni mwa shule 10 bora kwa mujibu wa matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).

“ Mwanangu alikuwa anasoma Shule ya Msingi Makonge ya Serikali, iliyopo kata ya Kanyangereko wilayani Bukoba. Wakati huo shule hizo waliziita yeboyebo, hazikuwa na matokeo mazuri kwenye mitihani ya taifa hivyo niliamua kumhamishia shule binafsi ya Rweikiza,” anaeleza.

Anasema kuwa uamuzi wa kumhamisha ulisababishwa na mambo kadhaa, ikiwamo ufaulu mzuri katika shule binafsi.

Anasema pia alibaini kuwa mazingira ya shule hiyo aliyokuwa akisoma mwanaye awali, ilikuwa inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwamo uhaba wa walimu, ambao ulisababisha watoto kutojifunza vyema hivyo kushindwa kumudu ushindani wa kimasomo na wenzao kutoka shule binafsi.

“Kufeli kwa wanafunzi wengi wanaosoma kwenye shule za serikali, hakumaanishi kwamba wao ni bongo lala, bali wamekosa fursa za kujifunza vyema ikilinganishwa na wenzao,” anasema mama huyo.

Kwake anaona ni vigumu kwa shule za Serikali kutatuliwa changamoto zinazozikabili, kwa sababu viongozi ambao wangepaswa kuzisimamia wengi wanasomesha watoto wao kwenye shule binafsi, hivyo hakuona matumaini kama shule hizo zitaboresha.

Jinsi alivyomudu kulipa ada

Anasimulia kuwa mwanzoni, alikusanya kiasi cha Sh500,000 kama mtaji wa kufanya biashara kubwa. Hata hivyo, akabadili uamuzi na kuamua kuzitumia fedha hizo kulipa ada ya mwanawe.

“Bahati nzuri utaratibu wa ulipaji wa ada uliopo katika shule hii ni mzuri, kwa sababu wanaruhusu kulipa kwa awamu nne; unaruhusiwa kulipa Sh403,000. Lakini kama wangetaka za mkupuo naamini isingewekana maana kulipa Sh 1,612,000 sio jambo jepesi kwangu,” anaeleza.

Huo ukawa mwanzo wa kumsomesha mtoto wake katika shule aliyoiamini kuwa ni bora kwa taaluma. Anasema kwa kupitia biashara ndogondogo anazofanya na mikopo kutoka vikundi vya vikoba, akajiwekea utaraibu wa kutunza fedha kwa ajili ya ada kila muhula unapofika.

Anavyojiandaa kumsomesha elimu ya sekondari

Pamoja na kuwa na furaha ya ufaulu mkubwa wa mwanawe, Adelina anaomba mwanawe achaguliwe kujiunga na shule bora ya Serikali, shule anayosema itamwepushia na mzigo wa kulipa ada kubwa kama ilivyokuwa awali.

Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, inatamka kuwa Serikali itahakikisha elimu ya awali hadi kidato cha nne inakuwa ya lazima na ya bure katika shule za umma. Kwa Adelina, sera hii inampa ahueni kuwa angalau mzigo wa ada kubwa sasa hautomwelemea.

“Kwa kweli asipochaguliwa huko alipoomba nitaumia, kwa sababu sasa nimeyumba kibiashara. Niliugua uvimbe gharama za matibabu zikala sehemu ya mtaji wangu, nitashindwa kumudu kumlipia ada,”anaeleza.

Anasema hali ilipokuwa ngumu alilazimika kumtoa mwanaye bweni na kuingia kutwa shule akitembea umbali mrefu, hivyo anashukuru mwanaye alimuelewa na amefanya vyema kama wenzie.

Adelina Stephano akiwa nan mwanawe Derick Mbezi aliyepata wastani wa A katika mtihani wa darasa saba. Na Mpigapicha Wetu

Mwanawe azungumza

Derick anasema ndoto yake ni kuwa rubani na ameomba kuchaguliwa katika shule za sekondari za wavulana Ilboru, Mzumbe na Mpwapwa, kuendeleza safari ya ndoto yake hiyo.

“Nashukuru nimefaulu sikumbuki kukwazwa na chochote nilipokuwa shuleni,’’ anasema mwanafunzi huyo.

Maendeleo ya taaluma Shule ya Msingi Rweikiza

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Rweikiza, Baraka Mwambinga anaeleza kuwa wamefanikiwa kushika nafasi ya tisa kitaifa, kwa sababu ya mambo mengi ikiwamo walimu kujituma ipasavyo.

Anasema walimu walikuwa na ari kwa kuwa walijengewa mazingira mazuri ya kazi kama maslahi bora, hatua ambayo imeiwezesha shule hiyo kuwa ya kwanza katika Wilaya ya Bukoba Vijijini na ya nne kimkoa.

Kwa upande wa wanafunzi, anasema walijawa na utayari wa kujifunza, huku wakipata huduma ya mahitaji yote muhimu.

“ Hii ni shule ya bweni, hivyo tulikuwa huru kuwapanga wanafunzi kujisomea na kufanya mitihani kila wiki,’’ anasema.