Maajabu ya mkojo wa sungura shambani

Mkulima akitumia mashine ndogo kumwagilia mkojo wa sungura katika eneo la mazao. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Hivi sasa mabanda ya kisasa yanayojengwa  kwa ajili ya kufugia sungura, yamewekewa miundombinu mizuri kwa ajili ya kuvuna na kuhifadhi mkojo wa mnyama huyo.

Mkojo wa sungura hutumika kama mbolea ya maji katika mimea na unasemekana kuwa na virutubisho vingi muhimu kwa ajili ya mimea hasa  katika mazao ya mbogamboga.

Pia, mkojo huo unatumika kama kiuatilifu asili kwa ajili ya kufukuza wadudu hatari kwa mazao.

Hivi sasa mabanda ya kisasa yanayojengwa  kwa ajili ya kufugia sungura, yamewekewa miundombinu mizuri kwa ajili ya kuvuna na kuhifadhi mkojo wa mnyama huyo.

Mkojo huo huweza kuhifadhiwa katika mapipa. Unaweza kuandaa keni au solo pia kwa ajili ya kumwagilia.

Jinsi ya kuandaa na kuutumia

Mkojo ukishapatikana huweza kuhifadhiwa katika solo na unakuwa tayari kwa matumizi. Kinachoweza kufanyika ni kuchuja mkojo huo na kuondoa uchafu, kisha unakuwa tayari kwa matumizi.

Mkulima atamwagilia maji asubuhi,  kisha kwenye saa tatu asubuhi atachukua mkojo huo na kuuweka katika solo tayari kwa kupiga kwenye mimea.

Atapiga katika maeneo yaliyoathirika au katika majani ya mmea husika, shina la mmea husika. Lakini pia katika udongo wa shamba husika.

Mkojo wa sungura unasifika kuongeza virutubisho kwa mmea lakini pia unasaidia  katika kuondoa wadudu hatari kama wadudu mafuta, inzi weupe, utitiri na kuukinga mmea na magonjwa ya fangasi na bacteria.

Majani ya mwarobaini na mkojo wa ng’ombe

Dawa nyingine ya asili ya kuua wadudu shambani ni mchanganyiko wa majani ya mwarobaini na mkojo wa ng’ombe. Mchanganyiko huu ni nzuri na una matokeo mazuri  katika kufukuza wadudu hatari shambani.

Jinsi ya kuandaa

1. Chukua majani ya mwarobaini kiasi cha kujaza ndoo nne.

2. Chukua mkojo wa ngombe kama lita 20

3. Tafuta kifaa maalumu cha kutwangia majani ya mwarobaini

4. Tafuta mifuko ya saflet inayohifadhia unga ya kilo 25 kisha andaa keni au solo kwa ajili ya kumwagilia kwenye mimea yako.

Baada ya maandalizi haya, chukua majani ya mwarobaini (weka mengi  kiasi cha kujaza ndoo nne za lita 20). Kisha yatwangwe mpaka yawe laini kabisa kiasi cha kutoa maji.

Baada ya hapo, weka majani hayo katika mifuko ya kilo 25 yakiwa yametwangwa vyema. Kisha mfuko huo ukiwa na majani yaliyotwangwa yatatumbukizwa katika ndoo yenye mkojo wa ngombe kama lita 20.

Utaacha kwa siku saba mfuko huo ndani ya mkojo huo, vyote vinaweza kukaa katika ndoo kubwa ya lita 20. Siku ya kutoa majani yatakuwa yamejichuja katika mkojo wa ngombe na kutengeneza harufu kali.

Hapo utachuja kama kuna baadhi majani yameingia katika mchanganyiko huo.

Kisha mchanganyiko unachanganywa na lita 20 za maji masafi tayari kwa matumizi.

Jinsi ya kutumia

Utaweka katika solo mchanganyiko huo kisha utamwagia katika shamba lako. Kama kwenye mmea palikuwa na wadudu utapiga hapo katika wadudu. Piga katika majani ya mmea, shina la mmea na katika udongo kwa ujumla.

Pia, ondoa majani yalioathirika katika mmea mara baada ya kupiga dawa husika.