Wednesday, March 15, 2017

Mabadiliko katiba ya CCM kwa sura pana

 

By Reginald Miruko, Mwananchi

Mkutano mkuu maalumu wa CCM mbali na ajenda yake ya mabadiliko ya katiba, uliambatana na mambo mengine mengi ambayo yamesababisha mtikisiko na hivyo hayatasahaulika kirahisi.

Mambo hayo mengine, likiwamo la kuwatimua wanachama 12 waliobatizwa “wasaliti” na wengine kadhaa kupewa adhabu ya onyo kali, ndiyo yamechukua nafasi kubwa ya mjadala katika jamii kuliko kile kilichokudiwa.

Tumeona pia kuwa mambo hayo mengine, likiwamo la kubadilisha wajumbe wa sekretarieti ya chama mubashara kwenye mkutano mkuu, yameeleweka zaidi kwa wananchi na kupeleka ujumbe mzito wa kugofya kwa wananchama wa CCM kuliko yale mabadiliko ya katiba yaliyosababisha kuitishwa kwa mkutano huo maalumu.

Lakini ukweli unabaki pale pale, kuwa lengo la mkutano huo, la mabadiliko ya katiba, lilikuwa na umuhimu na linabaki na maana pana zaidi hata kama halijadiliwi sana – athari zake kwa chama na kwa mwanachama mmoja mmoja zitaonekana huko mbele katika utekelezaji.

Hayakuwa mabadiliko ya ghafla, yalikusudiwa, yakapangwa na hatimaye kupitishwa. Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli alianza kueleza nia ya kutekeleza mabadiliko hayo ndani ya chama tangu achukue mikoba ya chama hicho kutoka kwa mtangulizi wake, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Rais Magufuli tangu awali alieleza jinsi anavyokerwa na ubadhirufu unaofanyika kwenye miradi ya chama katika ngazi mbalimbali huku chama kikilazimika kuomba fedha kwa matajiri waliokiweka mfukoni.

Pia alieleza jinsi chama hicho kilivyo matumizi makubwa ya fedha katika vikao na katika ajira, hivyo kuwa na mkakati wa kuweka usimamizi katika eneo hilo.

Ni kutokana na maono na mtazamo huo wa mwenyekiti, kwa kuchanganya na kile alichoeleza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuwa kulikuwa na tathmini inaendelea ndani ya chama kwa mwaka mzima, ndipo kikaitishwa kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) Desemba 13, mwaka jana na kupitisha mapendekezo ya mabadiliko hayo.

Mabadiliko yenyewe

Baada ya vikao vya Kamati Kuu na NEC kubariki mabadiliko hayo ya katiba na kanuni za chama, ndipo likaja jukumu la mkutano mkuu maalumu wa Taifa uliokamilisha kazi hiyo Jumapili iliyopita.

Katika mabadiliko hayo, katiba ya CCM imepunguza utitiri wa wajumbe katika vikao vyake ikianza na Kamati Kuu ambayo sasa itakuwa na wajumbe 24 badala ya 34 wa awali huku NEC wakipunguzwa kutoka 388 hadi 162.

Kamati ya Siasa ya Mkoa, CCM imepunguza wajumbe watatu kwa kila mkoa (sawa na wajumbe 96 kwa mikoa 32), wakati katika Kamati ya Siasa ya Wilaya wamepunguzwa wajumbe wanne wa kila wilaya na kufanya idadi yao kuwa 556.

Kutokana na punguzo hilo, na lile la wajumbe wa mkutano mkuu wa taifa ambalo halijawekwa wazi lakini wakikaribia 1,000 ni dhahiri kuna fedha nyingi zitaokolewa kwenye posho na huduma nyingine za wajumbe wakati wa vikao.

Mbali na fedha, viongozi wakuu wa chama wametetea punguzo hilo wakilinganisha na vyama vya ANC ya Afrika Kusini na CPC cha China, kuwa ni kuwa vikao vya watu wachache wenye tija na kuondoa majungu na umangimeza.

Jambo jingine kubwa lililopitishwa ni kubadili ajira za makatibu wa Jumuiya za chama kuwa chini ya Sekretarieti ya CCM badala ya kuajiriwa na jumuiya zenyewe.

Ingawa makatibu hawa na wasaidizi wao wamekuwa wakiajiriwa na kuwajibika kwa jumuiya, wamekuwa wakilipwa mishahara na CCM, lakini sasa watakuwa wanawajibika kwa chama, hatua inayoelezwa kuwa inalenga kuweka usimamizi wa mali za jumuiya.

Kabla ya mabadiliko hayo, kila jumuiya imekuwa ikisimamia mali zake, zikiwamo shule, viwanja, majengo na miradi mingine, lakini sasa itakuwa chni ya CCM ikitarajiwa kuwa chanzo kikuu cha mapato na kukiondoa chama kwenye utegemezi wa michango ya matajiri.

Yapunguza ajira

Mabadiliko hayo mbali na kupunguza idadi ya wajumbe wa vikao, pia yameondoka na ajira zaidi ya 170, hasa makatibu wasaidizi wa mikoa na wilaya na wengine wenye vyeo visivyotambulika katika katiba waliokuwa wakilipwa mishahara, huku ikiondoa mzigo wa posho uliotokana na takribani wajumbe, ikielezwa kuwa kazi zao zitafanywa na makatibu wa jumuiya.

Katika mlolongo huo wamo makatibu wasaidizi wa mikoa ambayo idadi yake ni 32 na wilaya ambazo idadi yake ni 139, wamepoteza ajira zao.

Makatibu hao wasaidizi hawajatajwa kwenye katiba ya CCM, lakini walikuwa wakiajiriwa kuwasaidia makatibu kuweza kumudu majukumu yao kwa kuwa ndio watendaji wakuu wa maeneo hayo.

Vyeo vingine vilivyokumbwa na panga hilo ni vile ambavyo havijatamkwa kwenye katiba ya chama hicho, kama mwenyekiti wa umoja wa wenyeviti wa mikoa, makamanda wa vijana, washauri wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) na walezi wa Jumuiya ya Wazazi katika ngazi zote.

Mabadiliko mengine ni kupunguza wajumbe waliokuwa na kofia mbili kama vile wabunge na wajumbe wa NEC, isipokuwa tu pale ambapo wanalazimika kwa mujibu wa nafasi zao.

Kauli ya Magufuli

Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo, Rais Magufuli alisema lengo la mabadiliko hayo ni kubana matumizi pamoja na kutunza siri za vikao.

Alisema mabadiliko hayo yamelenga katika sehemu kuu tatu ambazo ni muundo, rasilimali na uongozi ili kujenga chama madhubuti kinachoweza kuisimamia Serikali.

“Kuna vyeo hapa vina nguvu lakini havipo katika katiba. Kuna watu wanatviumia kama kinga,” alisema.

“Tunataka chama chetu kiwe kidogo kuanzia ngazi ya chama na jumuiya zake. Tunataka vyeo vyote visivyo katika katiba tuviondoe,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema kutokana na hali hiyo utendaji wa chama unashuka na kusababisha majungu, yanayosababisha watu wenye uwezo lakini hawana fedha kuondolewa.

Pia alisema muundo huo wa uongozi ulisababisha baadhi ya wanachama kuanza kukosa heshima

“Mtakumbuka kikao kilichopita wakati wajumbe waliposimama na kuimba wana imani na mtu gani sijui,” alisema akirejea kitendo cha wajumbe wa Halmashauri Kuu kuimba “tuna imani na Lowassa” kupinga kitendo cha Kamati Kuu kukata jina la waziri huyo mkuu wa zamani kugombea urais. Alisema mabadiliko hayo, pia yanalenga kuwafanya viongozi wawe karibu zaidi na wananchi badala ya kushinda kwenye vikao.

Kinana aya zungumzia

Akifafanua mabadiliko hayo, Kinana alisema mabadiliko ya ndani ya chama yanayofanyika hivi sasa hayamlengi mtu wala kikundi, bali yanalenga katika kukipa uhai, kuongeza ubora na ushindi.

Alisema kuna upotoshaji unaofanyika kuwa mabadiliko hayo yanamlenga mtu jambo ambalo si la kweli. Alisema si mara ya kwanza kwa chama hicho kufanya mabadiliko ya kimuundo na kisera na kwamba yamekuwa yakifanyika mara 15 tangu CCM imezaliwa miaka 40 iliyopita.

“Wapo wenye kasoro. Na kasoro zinaonekana wakati wa uchaguzi. Nimepata taarifa kuwa makatibu mnasaidia katika kupanga safu na kuwabeba watu,” alisema.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda anasema pamoja na mabadiliko hayo chama kinahitaji kufanya jitihada za kuongeza wanachama wapya na kuongeza nguvu ya ushawishi wa kisiasa kupita kundi la vijana la sivyo kinaweza kuporomoka.

“Mabadiliko yaliyofanyika yasiishie tu kwenye hatua za kupunguza vikao, wanachama, posho na kufukuza wanachama lakini wanatakiwa kuongeza uhai wa chama kwa kuwapatia nafasi vijana waanze kuonekana zaidi wenye uwezo ili kuliteka kundi la vijana, vinginevyo haikuwa imesaidia,” anasema.

Pili, anasema nafasi ya CCM kutangaza kujitegemea yenyewe ni jambo linalotia matumaini ya kuwa na matokeo chanya kwa kuwa wachache walikitumia kujinufaisha hatua iliyokipotezea mwelekeo. “Kwa hivyo waanze kuhimiza ulipaji wa ada za uanachama na usimamizi wa miradi yake vizuri,” anasema.

Tofauti na Mbunda, Profesa Abdalah Safari anasema mabadiliko hayo ni pengo linalotengeneza fursa kwa vyama vya upinzani.

Anasema amefurahishwa na mabadiliko hayo kwa kuwa yamefanyika kwa hasira bila kutazama athari za mchezo wa kisisa.

“Siasa ni mchezo kama soka, mwenzio anapoharibu, wewe unatumia fursa, mwaka 2015, CCM ilifurahi sana walipoondoka Zitto Kabwe, Profesa Kitila Mkumbo ingawa hawakwenda kwao,” anasema.

Profesa Safari ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema (Bara) anasema Kikwete alisoma alama za nyakati na kuamua kuwaacha wanachama waliobainika kutaka kujitenga, akiwamo marehemu Samuel Sitta, Mpendazoe na wengine wengi akijua athari zake zingekuwa mbaya kwa chama.

Hata hivyo, Profesa Safari anasema kuwapokea wanachama hao ndani ya Chadema kunategemeana na vigezo walivyo navyo.

“Kwanza uamuzi wa kupokea unafanywa na vikao vya chama, lakini lazima kuangalia ushawishi wake, uzoefu wake kisiasa, wawe ni ‘thinkers’, hatuchukui tu kwa kukurupuka, kwa mfano angefukuzwa Msukuma, Nchimbi, Bashe ni vijana wana mvuto,” anasema.

Mengine yaliyofanyika

Mbali na mabaduiliko ya katiba, Rais Magufuli alifanya mabadiliko ya pili kwenye sekretarieti ya chama na kuomba yabarikiwe na mkutano mkuu, jambo ambao si la kawaida, bali hufanywa na NEC.

Katiba mabadiliko hayo, aliwaondoa, Naibu katibu mkuu Zanzibar, Vuai ali Vuai, Katibu wa uchumi na fedha, Zakia Maghji na Katibu wa oganaizesheni, Seif Mohammed Khatib na kuwateua Abdallah Juma, ambaye anakuwa naibu katibu mkuu (Zanzibar), Pereira Silima (oganaizesheni) na Frank Haule (uchumi).

Wasaliti wafukuzwa

Siku moja kabla ya Mkutano mkuu maalumu, Kikao cha NEC kilifanyika Dodoma na kupitisha pamoja na mambno mengine, mapendekezo ya kamati ya Maadili ya kuwatimua viongozi 12 na wengine kuwapa onyo kali kwa usaliti wakati wa uchaguzi mkuu 2015.

Waliotimuliwa uanachama

Baada ya kikao hicho kilichokutana kwa sasa tatu, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Hamphrey Polepole aliwataja viongozi waliofukuzwa uanachama kuwa ni Sophia Simba, mwenyekiti wa UWT na mjumbe wa kamati kuu na wenyeviti wa mikoa Ramadhani Madabida (Dar es Salaam), Erasto Kwilasa (Shinyanga), Jesca Msambatavangu (Iringa) na Christopher Sanya (Mara).

Pia ilitimua wenyeviti wa wilaya ambao ni Omari Awadhi (Gairo), Ally Msuya (Babati Mjini), Makoko Laizer (Longido), Salum Madenge (Kinondoni) na Wilfred Molel (Arusha Mjini). Kwa upande wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa(Nec) waliofukuzwa uanachama ni Ally Sumaye (Babati Mjini) na Erasto Manga (Arumeru).

Waliovuliwa uongozi

Wenyeviti wa wilaya waliovuliwa uongozi ni Abeid Kiponza (Iringa Mjini), Assa Simba (Ilala), Hamis Nguli (Singida Mjini), wakati wajumbe wa Halmashauri Kuu waliopewa adhabu kama hiyo ni Ajili Kalolo (Tunduru). Wajumbe wengine wa halmashauri Kuu waliovuliwa uongozi ni Hassan Mazala (Singida Mjini) na Valerian Burreta (Kibaha Mjini).

Waliopewa onyo kali

Polepole aliwataja wanachama waliopewa onyo kuwa kali ni pamoja na Josephine Gezabule, ambaye ni mbunge wa viti maalum na mwenyekiti wa UWT mkoani Kigoma, Muhaji Bushako (mwenyekiti, Muleba), Ali Mchumo (mjumbe Nec, Kilwa) na Emmanuel Nchimbi (Balozi Brazil). Wanachama waliopewa onyo watakuwa chini ya uangalizi kwa kipindi cha miezi 12 na katika kipindi hicho hawaruhusiwi kugombea nafasi yoyote.

Nyongeza na Kelvin Matandiko

-->