Mabadiliko sita usiyopaswa kupuuzia

Mfanyakazi anaweza kutumia fursa ya ofisi kuwa na kompyuta zilizounganishwa intaneti kupanua uwezo wake mahali pakazi kwa kujifunza mambo mbalimbali kulingana na taaluma yake kupitia mitandao mbalimbali. picha ya Maktaba.

Muktasari:

Katika makala haya nitadokeza mabadiliko saba muhimu kuyafahamu na kuyatawala ili usije kujikuta unapoteza furaha ya kweli ya kuishi kwa kuwa mtumwa wa fedha, mapenzi, cheo, uhusiano au mtumwa wa ‘misifa’.

 Pilika zetu za kupata fedha, vyeo, kujenga uhusiano na kukubalika katika jamii zinaathiriwa na mabadiliko yanayoendelea kutokea katika jamii yetu.

Katika makala haya nitadokeza mabadiliko saba muhimu kuyafahamu na kuyatawala ili usije kujikuta unapoteza furaha ya kweli ya kuishi kwa kuwa mtumwa wa fedha, mapenzi, cheo, uhusiano au mtumwa wa ‘misifa’.

Uhuru wa mawasiliano

Uwapo wa mitandao ya kijamii, kushuka kwa bei za simu na kompyuta, teknolojia ya upigaji picha na uandishi kama vile kutumia blogu, ni baadhi ya mambo yanayochochea uhuru wa mawasiliano kukua.

Uhuru huu unaweza kuathiri malezi ya watoto, uhuru pia unaweza kuathiri usiri wa mambo yako na bila shaka unaathiri ufanisi wako kibiashara na kikazi.

Ili kuweza kujitawala na kutawala mabadiliko haya ya uhuru wa mawasiliano, inakupasa ujifunze vyema matumizi ya teknolojia husika au upate mtu wa kukusaidia kusimamia mambo yako ili yasiathirike na uhuru huu wa mawasiliano.

Fahamu yapi unastahili kufanya ukiwa mtandaoni – kwa simu na kwa kompyuta, tambua pia nini watu wanafanya ambayo yanaweza kukuathiri. Mfano mzuri, ni pale unapoweka picha ya mpenzi wako aliyependeza vizuri, ila picha hiyo ukaikuta imewekwa kwenye mitandao ya ngono. Mfano mwingine, usipofuatilia mara kwa mara anachoandika mtoto wako mtandaoni unaweza kushtushwa siku ukawa tagged picha binti yako aliyepo shule ya kulala - ‘boarding school’ akila ‘bata’ kwenye club ya usiku. Au kukuta ameandika status – “Jamani, siwezi kusoma huyu BF (rafiki yangu wa kiume) kila nimfanyiacho haridhiki, nimempa hadi pocket money zangu akae nazo, ila haridhiki”.

Machafuko katika jamii

Hali ngumu ya kiuchumi, mabadiliko katika uwezo wa kifikra wa watu na ukandamizaji uliokithiri katika jamii zetu ni moja ya sababu zinazochochea machafuko ya kila siku yanayoendelea. Hata yale ambayo ulidhani kuwa hayawezi kutokea nchini mwetu, bila shaka utaanza kuyaona yakitokea. Hali hii ni mwendelezo wa mabadiliko katika maisha yetu.

Serikali zinazidi ‘kuchanganyikiwa’ kwakuwa mabadiliko yanatokea kwa haraka sana kwa kasi ambayo haikutazamiwa. Hivyo Serikali kujibu mapigo haya, inabidi zije na mbinu nyingi kali zinazoweza kuonekana kama ni za kidikteta.

Uzalishaji mkubwa wa ushindani wa hali ya juu

Kupanuka kwa fikra za watu wengi, maboresho katika teknolojia, urahisi wa upatikanaji wa taarifa na mijumuiko ya watu kutoka nchi tofauti.

Ni mambo yanayoleta ushindani katika uzalishaji. Mbinu zilizosaidia biashara fulani kuwa kubwa miaka 10 iliyopita, zinaweza zisiisaidie biashara hiyo au nyingine inayofanana nayo kukua.

Wajasiriamali sasa wanazalisha bidhaa mpya, ubora unaboresha, bei zinazidi kuenda chini na mbinu za kufikisha bidhaa kwa mteja zinaboreshwa. Mabadiliko haya, yanahitaji mjasiriamali siyo tuu ajue vyema kuzalisha bidhaa yake, ila aifahamu vyema jamii anayotaka kuiuzia bidhaa, ajenge mtandao mkubwa na wateja wake na zaidi aweze kukusanya na kusimamia taarifa za jinsi ya kuboresha ushindani wake katika soko.

Utitiri wa taarifa

Maboresho katika teknolojia ya habari na mawasiliano, yamechangia siyo tu kuwapo kwa websites na mitandao ya kijamii (social networks) bali yamerahisisha matumizi; hata umiliki wa mitandao.

Mfano kuna blogu kadhaa nchini Tanzania pekee na kurasa maelfu za Facebook. Kuna video za mamilioni kwenye Youtube.

Usipoweza kutawala vyema hali hii ya utitiri huu wa taarifa unaweza kujikuta unakuwa mtu wa kupotoshwa na usiyekuwa na ufanisi katika mambo yako ya kielimu, kikazi na hata kibiashara.

Hakuna wakati unaohitaji ujuzi wa kipekee wa kutawala muda wako na pia kuchambua taarifa unazozipata.

Maboresho makubwa katika teknolojia mbalimbali: Si tu upande wa teknolojia ya habari, bali aina nyingi za teknolojia kama vile teknolojia za uzalishaji wa vyakula na teknolojia za utengenezaji wa mashine.

Mambo haya siyo tu yanaleta bidhaa mpya na kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa mambo mengi, pia yanaleta athari nyingine ambazo inatupasa kuwa makini nazo kama vile, athari za kiafya, athari za malezi (kuporomoka kwa maadili), athari za kiuchumi (biashara nyingi kuporomoka kwa kushindwa kushindana).

Uharaka wa usambaaji wa

mabadiliko

Kwa sasa dunia ni kama kijiji. Mabadiliko yanayoendelea kutokea kiuchumi, kiteknolojia, kisiasa na kijamii, yanaathiri siyo tu taifa moja; ambapo badiliko fulani limetokea, bali mabadiliko hayo husambaa kwa haraka kwa nchi nyingine. Kama ilivyo kwenye usambazaji wa bidhaa mbalimbali unavyoenda kwa haraka – kumbuka matoleo kadhaa ya simu kama iphone, Samsung na kadhalika yanavyofika hapa nchini, tutarajie mabadiliko mengine yanayotokea nchi za Magharibi na Bara la Asia kufika kwa haraka Tanzania.

Hitimisho

Elimu ya darasani pekee haitoshi kukusaidia kupita na kutawala mabadiliko haya makubwa. Unahitaji kupenda kusoma ziada.

Hakikisha unapata taarifa sahihi kwa kufuatalia kuaminika kwa chanzo cha taarifa. Pia, tumia ‘search engine’ kama Google, kutafuta vyanzo vingine vya habari vinasema nini kuhusu taarifa unayodhani ni sahihi. Linda utashi wako kwa kuwa huo pekee ndiyo mali kubwa zaidi kwa maisha yako.

Ukipoteza utashi wako kwa tamaa ya mali, kufuata mkumbo na kadhalika, utajikuta unapotea zaidi. Kuwa tayari kubadilika kuendana na mazingira na hali halisi – elimu, aina ya biashara, aina ya kazi, mahali pa kuishi, mahusiano, malezi ya watoto.

Katika nyakati tulizopo ni muhimu sana kuufahamu na kuuishi msemo huu “Don’t Work Hard, Work Smarter” yaani “Usifanye tu kazi kwa nguvu zako zote, bali fanya kazi kwa akili zaidi.”