Mabalozi wa Tanzania wapewe somo la diplomasia ya uchumi

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini (kushoto) akiwa na mwenyeji wake Rais John Magufuli baada ya Rais Zuma kufanya ziara nchini.

Muktasari:

Viongozi wa mataifa makubwa waliotembelea Tanzania hivi karibuni ni wakuu wa nchi za Uturuki, Morocco, India, China na Marekani. Ziara ya Rais wa Misri inapaswa kutazamwa na kutafsiriwa sawa na za viongozi hawa wengine.

Ujio wa Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi katika juma la pili la Agosti ni moja ya ziara za viongozi wa ngazi hiyo kutoka nchi mbalimbali kwa miaka ya karibuni.

Viongozi wa mataifa makubwa waliotembelea Tanzania hivi karibuni ni wakuu wa nchi za Uturuki, Morocco, India, China na Marekani. Ziara ya Rais wa Misri inapaswa kutazamwa na kutafsiriwa sawa na za viongozi hawa wengine.

Shabaha kuu ya ziara hizi ni diplomasia ya uchumi na biashara kuliko siasa. Ziara hizi hazianzii na kuishia Tanzania, hufanywa katika nchi za kimkakati kwa mataifa haya yanayojua yanataka nini Afrika na Tanzania kimahususi

Biashara

Tanzania na Misri zimekuwa na uhusiano wa kibiashara kwa muda mrefu. Tanzania imekuwa ikiuza zaidi malighafi na mazao ya kilimo, huku ikinunua bidhaa za viwandani.

Aina hii ya biashara imeifanya Misri kuwa muuzaji mkubwa kwa Tanzania na Tanzania kuwa mnunuzi kuliko muuzaji. Mizania ya biashara inaangukia upande wa Misri kwa maana Tanzania imepeleka fedha nyingi za kigeni Misri kuliko ilivyopata kutoka huko. Tanzania ingenufaika zaidi kama ingeuza zaidi kuliko kununua.

Uhusiano wa kiuchumi na biashara utakuwa na manufaa zaidi kama kampuni za Misri zitawekeza Tanzania, badala ya kuuza kutoka kwao. Kiuchumi, uwekezaji utachukua nafasi ya biashara na ni jambo jema.

Uwekezaji

Wawekezaji hasa wa nje hutafuta mambo matatu katika kutekeleza miradi yao ambayo ni masoko, malighafi na ufanisi. Mazingira rafiki ya kuvutia na wezeshi ni muhimu katika nchi yoyote ikiwamo Tanzania.

Mwekezaji huangalia faida za kiuchumi atakazopata. Kwa anayetafuta soko, mambo makuu ni ukubwa, ukuaji na uwezo wa walaji kununua bidhaa na huduma atakazozalisha.

Kwa anayetafuta ufanisi mambo makuu ni mazingira na vitendea kazi wakiwamo watu wenye ujuzi wa hali ya juu. Pia, uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma.

Kwa mwekezaji anayetafuta malighafi huzingatia uwapo wa malighafi husika kama vile madini. Mambo mengine muhimu ni miundombinu, kutokuwapo mazingira ya ukiritimba na rushwa, kuwapo rasilimali watu kwa kiasi na ubora. Wawekezaji wanaoambatana na viongozi katika ziara hizi watazingatia mambo haya kabla ya kuamua kuwekeza mitaji yao.

Diplomasia ya uchumi

Ziara za viongozi mbalimbali nchini akiwamo Rais wa Misri ni kufanikisha diplomasia ya uchumi. Hii ni diplomasia ya kutafuta masoko na uwekezaji. Hata inapotolewa mikopo na misaada kunaweza kuwa na jicho la kiuchumi nyuma ya pazia.

Ujio wa viongozi hawa unatufundisha kwenda katika nchi za kimkakati kwa uchumi wetu kutafuta masoko na kuvutia uwekezaji. Kusubiri wafanyabiashara na wawekezaji waje bila kuwafuata vya kutosha si mkakati.

Mabalozi wa Serikali waliopo nje lazima wafundishwe na kulielewa vizuri somo la diplomasia ya uchumi.

Mto Nile

Kati ya mambo makuu katika ziara ya Rais wa Misri pengine ni maji ya Mto Nile. Huu ni muhimu kwa uchumi wa Misri. Upo usemi kuwa Nile ni Misri na Misri ni Nile.

Chanzo chake kipo katika mito kadhaa inayoanzia Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania. Maji yake huelekea Misri kutoka Ziwa Victoria. Sehemu kubwa ya ziwa hili ipo Tanzania. Kati ya mijadala ya matumizi ya maji ya ziwa hili kimataifa ni athari za kiuchumi kwa Misri iwapo nchi zilizopo kwenye chanzo zitavuna na kutumia kwa wingi maji ya mto huu.

Makubaliano ya enzi za ukoloni, ni nchi hizi kutoyatumia maji haya na kuiathiri Misri. Msimamo wa Tanzania ni tofauti. Umejijenga katika mtazamo, ina haki ya kutumia maji haya itakavyo na haiwajibiki kubanwa na makubaliano ya kikoloni.

Miaka 10 iliyopita mwandishi wa makala haya alitafiti na kuandika kitabu kuhusu matumizi ya maji ya Mto Nile kwa maendeleo ya uchumi wa Tanzania. Kitabu hiki kimeandikwa na wataalamu kutoka nchi kumi unapopita mto huu mrefu kuliko yote Afrika.

Mustakabali

Rais wa Misri amekuja Tanzania baada ya viongozi wengine kufanya hivyo. Hii ni dalili ya Tanzania kuhitajika na nchi hizi. Lakini lazima Tanzania ijiweke kimkakati ili ipate inachotaka kutoka kwa mataifa makubwa yanayoonyesha kuihitaji.

Misri, Uturuki, China, Marekani, India na nyinginezo zinatazama faida za kiuchumi kutoka Tanzania. Zitashindana kuona nani anapata faida kubwa zaidi. Ushindani huu unapaswa kuwa wa manufaa kwa Tanzania ikijiweka kimkakati na kufahamu ukubwa na nafasi yake, kinyume chake itavunwa badala ya kuvuna.