Mabango ya Kiingereza Ubungo kwa ajili ya nani?

Muktasari:

  • Akiwa amevalia miwani yake yenye lenzi nzito, anahangaika kusoma maandishi katika mabango yenye matangazo yanayohusiana na shughuli ya ujenzi wa barabara. Anaamua kumuuliza kijana anayepita karibu naye ili kupata ujumbe unaopatikana.

Nikiwa Ubungo, kandokando ya barabara ya Morogoro, eneo maarufu kama ‘Ubungo Mataa’, namwona mzee yapata umri wa miaka 70 hivi.

Akiwa amevalia miwani yake yenye lenzi nzito, anahangaika kusoma maandishi katika mabango yenye matangazo yanayohusiana na shughuli ya ujenzi wa barabara. Anaamua kumuuliza kijana anayepita karibu naye ili kupata ujumbe unaopatikana.

Kijana huyo anaangalia maandishi, midomo yake inashikana anaanza kugugumiza... halitoki neno!

Katika eneo tajwa, shughuli za ujenzi wa barabara zinaendelea. Kuna mabango mbalimbali ya kutoa hadhari kwa watumiaji wa barabara kama ilivyo ada. Hata hivyo, mabango mengi yameandikwa kwa lugha ya Kiingereza.

Asilimia kubwa ya Watanzania wanakijua vizuri Kiswahili. Mabango yaliyosimamishwa katika eneo hilo kwa ajili ya kuwasaidia kuwa makini na hali ya eneo hilo si msaada kwao.

Mengi yameandikwa kwa Kiingereza ambacho wengi hawakijui kama mzee aliyetaka kupata ujumbe unaopatikana katika mabango hayo, lakini asifanikiwe kutokana na ugeni wa lugha iliyotumika.

Kiasi kikubwa cha mabango hayo yana ujumbe ambao hauna tafsiri ya Kiswahili isipokuwa machache. Baadhi ya mabango yanasomeka hivi: Caution Deep DANGER Excavation (hakuna tafsiri ya Kiswahili); Road Closed (hakuna tafsiri ya Kiswahili); Pass Right (yaliko maneno hayo hakuna tafsiri ya Kiswahili isipokuwa nyuma ya bango hilo); Pass Left (ni kama ilivyo katika Pass Right). Mengine yana maneno: Men at Work (yapo yenye tafsiri na yasiyo na tafsiri ya Kiswahili).

Halikadhalika, tatizo hili linajitokeza katika maeneo mengine mengi jijini Dar es Salaam yakiwamo ‘Simu 2000’, Kariakoo, Posta na kwingineko.

Ukiwa unaingia katika kituo cha mabasi cha Simu 2000, utalakiwa na bango kubwa la rangi ya buluu lenye maneno SINZA BUS TERMINAL bila tafsiri yake.

Aidha, katika kituo hicho eneo lenye huduma ya vyoo, kuna kibao kilichoandikwa TOILET. Nikiwa kituoni hapo siku moja, niliwahi kushuhudia watu kadhaa wake kwa waume wakiuliza vyoo vilipo, huku bango hilo likisomeka vizuri kutoka walipo.

Maneno mengine ya Kiingereza yanayopatikana kwenye mabango jijini ni kama vile ‘Don’t block the gate’, ‘Danger-dont sit here’, Male/Female; Men/Women (kwenye vyoo), Bus Stand, Humps ahead na mengineyo.

Maneno hayo hutumika katika baadhi ya maeneo bila tafsiri ya Kiswahili ambacho takriban asilimia 90 ya walengwa wa ujumbe huo wanakifahamu.

Mbalamwezi ya Kiswahili inajiuliza, ikiwa tumo ndani ya Tanzania ambamo wananchi wengi wanakijua Kiswahili, kwa nini kunawekwa mabango yenye lugha ya kigeni ambayo wengi hawaijui?

Sheria inaeleza kuwa, utoaji wa ujumbe kwa umma hauna budi kuzingatia kundi kubwa la watumiaji wa lugha ya mahali husika.

Kwa sababu hiyo, sehemu zote mabango yanapaswa kutumia lugha ya Kiswahili na kwa kuwa kuna wageni wachache ambao wengi wao hutumia Kiingereza, basi chini ya maneno ya Kiswahili, ujumbe huo ufasiriwe kwa Kiingereza na si kinyume chake.

Ujumbe unaotolewa katika mabango aghalabu ni muhimu. Ikiwa lugha iliyotumika haieleweki kwa walengwa basi ni kazi bure!

Katika maeneo ya Ubungo ambapo ujenzi wa barabara unaendelea, mtu anapaswa kuelewa ujumbe uliotolewa katika mabango hayo, ili aweze kuchukua hadhari.

Kwa hivyo, mamlaka husika ziwe makini pindi zinapoandaa matangazo hayo. Hazina budi kuzingatia kanuni za lugha katika uandaaji wa matangazo kwa umma.