Mabegi mazito ya wanafunzi ni vizuri yatafutiwe suluhu

Kutokana na wingi wa masomo siku hizi,wanafunzi hulazimika kubeba mabegi makubwa yenye madaftari na vitabu kila siku.Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Wazanzibari walipenda kuutumia wakiwatania Wanyamwezi waliofika visiwani kufanya kazi za kilimo na ufugaji nje kidogo ya mji, katikati ya Kisiwa cha Unguja na katika mashamba ya viazi vitamu katika Kijiji cha Makangale, Kaskazini Pemba.
  • Kwa kiasi mambo yamebadilika siku hizi. Nimesikia mara nyingi watu wa mjini na hasa vijana wakisema ‘mzigo mzito mpe mwanafunzi.’

Waswahili wanao usemi maarufu wa utani: “Mzigo mzito mpe Mnyamwezi”, ni usemi unaotokana na mambo mengi ikiwamo sifa ya kuchapa kazi hasa shambani, uaminifu na uadilifu ambao watu wa ukanda wa pwani ya Afrika ya Mashariki waliiona katika miaka ya nyuma kutoka kwa watu wa kabila hili la mkoani Tabora.

Wazanzibari walipenda kuutumia wakiwatania Wanyamwezi waliofika visiwani kufanya kazi za kilimo na ufugaji nje kidogo ya mji, katikati ya Kisiwa cha Unguja na katika mashamba ya viazi vitamu katika Kijiji cha Makangale, Kaskazini Pemba.

Kwa kiasi mambo yamebadilika siku hizi. Nimesikia mara nyingi watu wa mjini na hasa vijana wakisema ‘mzigo mzito mpe mwanafunzi.’

Hii inatokana na wanafunzi wengi, hata wanaosoma shule za chekechea kubeba mkoba mzito wa vitabu na vifaa vya masomo wanapokwenda na kurudi shule kuliko uwezo wa migongo yao kuhimili uzito huo.

Kwa bahati mbaya suala hili limekuwa likifumbiwa macho kama vile halina athari na hatari zake kwa maisha hapo baadaye hazizungumzwi hadharani.

Hata madaktari ambao wanaelewa vizuri athari za mwenendo huu wamebana kimya kama vile hawalioni tatizo lililopo.

Kumuona mwanafunzi amebeba mkoba mzito hata kushindwa kukimbia imekuwa ndiyo mtindo wa kisasa. Wachache wanaokwenda na mikoba mepesi huonekana kama hawajaendelea.

Badala yake kinachosikika katika jamii na kupigiwa kelele katika vyombo vya habari ni kuporomoka kwa ubora wa elimu; mada kubwa ya mjadala kila baada ya matokeo ya mtihani.

Tunachosikia kwenye mijadala mingi ya elimu ni kuwapo kwa walimu wachache ambao wengi hawana ujuzi wa kufundisha kwa viwango vinavyokubalika, msongamano madarasani, uchache wa madawati na mazingira yasiyo rafiki.

Unapoitafakari kauli ya mzigo mzito mpe mwanafunzi unaona wazi inaelezea hali halisi juu ya mikoba inayobebwa siku hizi.

Kama utakaa nje ya jengo la shule wanafunzi wanapofika au kutoka na ukaweza kumimina kwenye lori kila kilichokuwemo katika mikoba yao, si ajabu shehena ya vitu viliyobebwa na wanafunzi 500 ikajaza gari hilo. Zamani, wanafunzi wengi walitumia mikoba ya ukili lakini siku hizi wengi huwa na mikoba ya kisasa wanayobeba mgongoni. Wataalamu wanasema uzito wa mikoba hiyo husababisha viungo na misuli ya mwili kufanya kazi ya ziada kuuhimili.

Utafiti umeonyesha mzigo mzito unasababisha maumivu ya shingo, mabega au mgongo. Madaktari wanashauri mtoto abebe mkoba wenye uzito kati ya asilimia 10 na 15 ya uzito wa mwili wake lakini ni vizuri zadi ikiwa si zaidi ya asilimia nane.

Vilevile, zipo njia zinazopendekezwa kubeba mkoba. Mfano, madaktari wanasema si vizuri kwa uzito wote wa mkoba kuwekwa juu ya bega moja kwa sababu kufanya hivi kunaweza kusababisha maumivu ya bega na shingo.

Uchunguzi katika nchi nyingi nyingine unaonyesha wanafuzi wanaobeba mikoba mizito hubadili hata mwendo wao wa kawaida na kuwaweka katika hatari ya kuanguka wanapopanda ngazi au wanapopita kwenye utelezi.

Tatizo lililopo ni kukua kwa teknolojia na kubadilika mfumo wa maisha hivyo kusababisha wanafunzi kuwa na vitabu vingi vya masomo na kubeba vitu vyengine.

Hivi ni pamoja na vifaa vya muziki, kompyuta ndogo za michezo, chakula na maji au juisi na kuifanya mikoba yao kuwa na uzito mkubwa.

Kwa Zanzibar tatizo jengine ni wanafuzi wengi kutojua ratiba ya masomo ya kila siku, tofauti na ilivyokuwa zamani kulikuwapo ratiba inayojulikana ambayo haibadiliki kwa muda mrefu.

Utaratibu huu ulimuwezesha mwanafunzi kuwa na uhakika wa masomo yatakayofundishwa siku husika hivyo kuchukua vitabu na madaftari yanayohitajika tu kwa siku hiyo.

Hii ilisaidia mwanafunzi kuacha nyumbani vitabu ambavyo somo lake halitofundishwa siku ile na kupunguza uzito wa mkoba wake.

Suala hili linafaa kuangaliwa kwa umakini na kurudisha utaratibu wa zamani wa kuwa na ratiba ya uhakika ya masomo ili kupunguza mzigo wa mkoba wa mwanafunzi.

Wazazi wanaweza kusaidia kwa kuangalia ratiba ya masomo na kuhakikisha watoto wanabeba vitabu watavyohitajika kwa siku husika.

Tafiti zinaonyesha kuwa katika miaka ya karibuni, mikoba ya wanafunzi katika nchi mbalimbali ina uzito wa zaidi ya asilimia 20 ya mwili wa mwanafunzi.

Hii ina athari nyingi kwa mwanafuzi kiasi cha baadhi ya nchi kutunga sheria na kuweka miongozo ya kiwango cha mwisho cha uzito wa mkoba kulingana na umri na uzito.

Katika kuhakikisha sheria inafanya kazi kama inavyotarajiwa, mkoba wa kila mtoto huwa unapimwa uzito kila mwanafunzi anapofika shule kabla ya kuingia darasani.

Vilevile wanafunzi wanapewa elimu ya athari za kiafya wanazoweza kupata kama watabeba mikoba mizito na kuelekezwa njia nzuri na salama za kubeba mikoba yao.

Wakati umefika kwa wataalamu wa wizara za elimu na afya kuliangalia suala hili kwa undani na kutoa muongozo juu ya uzito wa mkoba wa mwanafunzi kwa kuanzia na wale wa chekechea.

Watakaoshughulikia suala hili wafanye utafiti utakaowapa mwanga mzuri wa namna nchi nyingine walivyolishughulikia.

Kwa kufanya hivyo kutaisaidia Tanzania kuondokana na usemi wa mzigo mzito mpe mwanafunzi.

Shime, tutafute njia ya kuwasaidia watoto kwa kuwapunguzia mzigo huu mzito.