Madhara ya kiuchumi ya matumizi ya Dola za Marekani nchini

Muktasari:

  • Hali hii haipo Tanzania tu bali ipo katika nchi nyingine kama vile Zimbabwe, Kenya na kwingineko. Hali ya kutumia Dola ya Marekani katika miamala ndani ya Tanzania na nchi nyingine inaonekana kwa njia mbalimbali.

Matumizi ya Dola ya Marekani ndani ya uchumi wa Tanzania siyo jambo geni. Sarafu hii imekuwa ikitumika katika miamala kadhaa sambamba na Shilingi yetu.

Hali hii haipo Tanzania tu bali ipo katika nchi nyingine kama vile Zimbabwe, Kenya na kwingineko. Hali ya kutumia Dola ya Marekani katika miamala ndani ya Tanzania na nchi nyingine inaonekana kwa njia mbalimbali.

Njia kuu ni kwa bei za baadhi ya huduma na bidhaa kuwekwa katika Dola hiyo. Hata hivyo malipo hufanywa katika Shilingi kufuatana na kiwango cha kubadili fedha kilichopo sokoni kwa muda husika. Hali nyingine ni ulipaji wa baadhi ya huduma na bidhaa kutakiwa kufanywa kwa kutumia Dola ndani ya Tanzania.

Sheria

Hakuna sheria inayokataza kuweka bei katika sarafu ya nje kama vile Dola ya Marekani. Kinachokatazwa ni kukataa kupokea malipo halali kwa Shilingi. Sheria hairuhusu muuzaji wa bidhaa na huduma kumlazimisha mnunuzi kutoa Dola au sarafu nyingine ya nje.

Hivyo siyo kinyume cha sheria kuweka bei ya bidhaa au huduma kwa Dola. Kinachokatazwa ni kwa muuzaji kumlazimisha mnunuzi kutoa Dola badala ya Shilingi.

Licha ya sheria kutaka wauzaji kutolazimisha kudai malipo kwa Dola, matumizi yake kwa uchumi wa Tanzania unaleta changamoto.

Ukubwa wa tatizo

Matumizi ya Dola katika nchi ambazo siyo sarafu zao umeenea katika nchi mbalimbali. Ni changamoto ya kiuchumi, kisiasa na kijamii duniani kwa muda mrefu.

Hali hii imeonekana katika nchi nyingi kama vile Amerika ya Kusini ambako Panama inaitumia tangu mwaka 1904. Nafasi ya sarafu ya Panama iitwayo Sucre ilichukuliwa na Dola ya Marekani rasmi katika mzunguko.

Peso ya Argentina ilifanya hivyo pia. Baadhi ya nchi zilizokuwa zinajenga Shirikisho la Urusi nazo zilitumia Dola katika mzunguko.

Kwa Afrika, hali hii imeonekana Zimbabwe, Zambia, Kenya, Sudan Kusini na Tanzania, kutaja baadhi.

Tanzania

Matumizi ya Dola nchini yanaonekana kwa namna tofauti na sehemu mbalimbali. Yanaonekana katika bei za bidhaa na huduma ikiwa ni pamoja na baadhi ya bei za tiketi za ndege hata kwa safari za ndani ya nchi.

Nyingine ni bei za baadhi ya huduma katika hoteli kubwa hasa malazi au kukodi kumbi za mikutano. Nyingine ni bei za viwanja, mashamba, majumba, pango la nyumba, ada za baadhi ya shule, sekondari na vyuo.

Bei nyingine zinazowekwa katika Dola ni pamoja na baadhi ya tozo na ada kama vile ushauri elekezi na baadhi ya ada na tozo za Serikali kwa baadhi ya taasisi.

Zipo bidhaa katika baadhi ya maduka makubwa na viwanja vya ndege ambazo bei zake huwekwa katika Dola ya Marekani.

Kwanini Dola

Kuna sababu nyingi za kutumia Dola ya Marekani kwenye nchi ambazo zina sarafu zake zinazojitegemea. Sababu za kuweka bei katika Dola ndani ya Tanzania ni ndefu, suala la msingi ni uimara wa Shilingi inapolinganishwa na Dola.

Kama ilivyowahi kujadiliwa katika safu hii, uimara wa Shilingi kulinganisha na Dola ya Marekani unategemea uwapo wa Dola za kutosha sokoni. Zikiwapo Dola nyingi kulinganisha na uhitaji, basi Shilingi huwa imara.

Baadhi ya wanaouza bidhaa na huduma ambazo bei zake zipo katika Dola wanataka kulinda thamani ya biashara zao. Baadhi hununua bidhaa na huduma husika kwa Dola nje ya nchi. Watakapoziuza hapa nchini kwa Shilingi lazima wafidie gharama zao zote na kuweka faida juu.

Hata hivyo ni muhimu kujua kuwa mauzo haya yaliyopo katika sarafu ya Shilingi yatabadilishwa kuwa Dola kusudi wahusika waweze kwenda kununua mizigo mingine nje ya nchi ambako Dola inakubalika.

Hivyo ili kujilinda na kupoteza fedha na thamani ya biashara kama Shilingi inashuka thamani, wahusika hulazimika kuweka bei katika Dola. Hii inawasaidia kupata Shilingi ambazo wakizibadili kuwa Dola huwawezesha kununua bidhaa nyingine nje ya nchi bila kupoteza thamani.

Hivyo nia kuu ya kuweka bei katika Dola ni kulinda thamani ya biashara. Hata hivyo, hii inakuwa lazima kwa sababu ya kuyumba kwa thamani ya Shilingi kulinganisha na Dola.

Tatizo

Matumizi ya Dola yanaweza kusababisha matatizo kadhaa katika uchumi wa taifa husika. Mojawapo ni kupoteza thamani kwa sarafu ya ndani na kujitokeza kwa tabia ya kuthamini Dola ya Marekani kuliko sarafu ya ndani mfano Shilingi katika baadhi ya miamala. Hii siyo heshima kwa nchi huru yenye sarafu yake.

Tatizo jingine ni nchi kutoweza kusimamia sera zake za fedha vizuri kwa sababu fedha za nchi nyingine ndizo zinatamalaki katika mzuguko na miamala hivyo nchi husika. Ndiyo maana ni lazima kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo hili.

Cha kufanya

Kuna mambo mengi yanayopaswa kufanyika ili kuwa na suluhu endelevu katika hali hii ya kutumia Dola katika miamala ndani. Kuzuia hali hii kwa sheria siyo suluhu.

Suluhu ya kudumu ni kuimarisha thamani ya Shilingi. Hii itawezekana kwa nchi kuingiza fedha nyingi za kigeni hasa Dola baada ya kuuza bidhaa na huduma nyingi nje ya nchi, kupata fedha za kigeni kutoka kwa watalii, wawekezaji, wafadhili na diaspora. Kusudi yote haya yafanyike, mazingira rafiki na wezeshi yanahitajika.

Mwandishi ni mtaalamu, mtafiti na mshauri elekezi wa masuala ya uchumi na biashara Chuo Kikuu Mzumbe.