Madudu ya shule za mchepuo wa Kiingereza

Muktasari:

Hawa ni wale wanaojihimu kuhakikisha watoto wao wanasoma katika shule zinazotumia lugha ya Kiingereza kufundishia, maarufu kwa jina la English Medium.

Kasumba kuwa kujua lugha ya Kiingereza, ndiyo kuelimika imewakumba wazazi wengi nchini.

Hawa ni wale wanaojihimu kuhakikisha watoto wao wanasoma katika shule zinazotumia lugha ya Kiingereza kufundishia, maarufu kwa jina la English Medium.

Shule hizi zimejaa kila kona ya nchi hasa mijini. Kiingereza kinatumika kama chambo cha kuwavutia wazazi wengi, wasioona mashaka kulipa viwango vikubwa vya ada zinazotozwa katika shule hizo.

Awali shule hizi zilianzia elimu ya msingi na sekondari, lakini baadaye zikaja shule za chekechea na hata vituo vya kulea watoto wadogo. Navyo vikatumia lugha ya Kiingereza kama chambo cha kuwavuta wazazi na kwa hakika wazazi wengi wamekuwa wakivutika.

Zipo shule za aina hii zilizofanikiwa kuishi kwa miaka kadhaa na hata kujenga jina katika jamii. Nyingine zimekuwa zikianzishwa kila siku.

Hata hivyo, ukweli kuhusu sifa za shule hizi umewekwa bayana hivi karibuni, baada ya mamlaka zinazosimamia elimu hasa katika jiji la Dar es Salaam kuendesha operesheni ya kukagua shule zisizo na sifa.

Madudu shuleni

Godoro hili lilibainika likiwa linatumiwa na watoto kwa ajili ya kulalia.

Ni madudu ndicho unachoweza kusema kama kitu kilichogundulika katika shule nyingi zilizokaguliwa katika Manispaa ya Ilala.

Operesheni hiyo imeibua mambo mengi, ikiwamo shule nyingi kutokuwa na usajili, mazingira duni na hatarishi kwa afya za watoto. Matokeo ya hili operesheni hii ikawa ni kufungiwa kwa shule 198.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hamis Lissu anasema wameamua kufunga vituo ambavyo huitwa shule za mchepuo wa Kingereza, kwa sababu zinaendeshwa kwa ulaghai.

“ Kuna taratibu za usajili wa shule zinazojulikana ikiwamo kuwa na eneo lisilopungua heka tatu na nusu; sasa wapo ambao wameanzisha shule katika nyumba zao, wengine kwenye vyumba vya fremu za maduka. Hii ni miundombinu inayohatarisha maisha ya watoto wanaosoma huko, “ anasema.

Kwa sababu nyingi zimekuwa zikijiendesha kiudanganyifu, anasema wanachofanya viongozi ni kusajili majina ya wanafunzi wanaotakiwa kufanya mitihani ya taifa katika shule zenye usajili.

“ Hii ni hatua mbaya kwa sababu kuna dalili zote kwamba kuna baadhi ya wanafunzi hasa wa darasa la saba wanaweza kushindwa kufanya mtihani, maana kuna msuguano uliojitokeza baina ya vituo hivi na shule zilizowasajili,” anafafanua.

Msuguano uliopo anasama ni pale shule rasmi zinapotaka wanafunzi hao waunganishwe moja kwa moja kwenye shule zao, ili kujiandaa vyema na mitihani, lakini vituo vilivyowapeleka huwang’ang’ania kwa sababu ya kutaka ada zao.

“ Mimi ni mgeni nimehamishiwa hapa kutoka mkoani Mara nikaambiwa hii hali imekuwa ikijitokeza karibu kila mwaka hapa Dar es Salaam. Kuna vituo vina miaka 10 vinajitangaza ni shule huku wengine wakiweka namba bandia za usajili,”anaeleza.

Anasema mkoa umeanzisha utaratibu wa kuingiza wanafunzi wa kuanzia shule za awali hadi darasa la saba kwenye mfumo maalum utakaosaidia kujua idadi yao, hivyo kuweza kuwafuatilia kwa karibu na kuepusha usumbufu katika kuwahudumia.

Operesheni wilayani Ilala

Unaweza kusema ilikuwa kama sinema wahusika wakiwa watendaji wa Serikali na viongozi wa shule.

Kwa mfano, Ofisa Elimu wa Wilaya ya Ilala Elizabeth Thomas anasema katika baadhi ya shule wamiliki walikuwa wakifuta maandishi yaliyoandikwa na watendaji wa Serikali kuwa shule hizo zimefungiwa.

Mdhibiti ubora wa shule wa Manispaa ya Ilala, Fredric Mtaita anasema operesheni hiyo ilitanguliwa na barua kwa vituo hivyo, lakini wamiliki wale walionekana kutojali kuchukua hatua walizoelekezwa.

Mtaita anasema watoto wa shule za awali waliokuwa wanasoma kwenye baadhi ya vituo hivyo wamekuwa wakirundikwa na kulazwa kwenye vyumba vidogo visivyo na madirisha ya kuingiza hewa.

“ Tumeshuhudia mambo ya ajabu na kuhuzunisha kuna kituo tulikwenda watoto wanakohoa karibu wote, wamelala kwenye vigodoro vichafu vina mavumbi, ni vyema wazazi wakajenga utamaduni wa kujiridhisha na mazingira ya shule wanasoma watoto wao,” anasema

Uchunguzi wa Mwananchi katika kituo cha Gefan ulishuhudia hali mbaya kwani licha ya kuwa na wanafunzi 92, hapakuwapo darasa hata moja, isipokuwa vyumba vidogo ambavyo vilivyokuwa na joto kali ndani.

Mmiliki wa kituo hicho Geofrey Mwendapole anaeleza kuwa alikuwa safarini lakini amelazimika kurejea ghafla, baada ya kusikia kituo kinafungiwa kutokana na kukosa sifa.

“ Mimi nilipoondoka niliacha wanafunzi 56 lakini nimerejea nimekuta wapo 96, kweli ni makosa yametokea majengo haya ni madogo hayalingani na idadi ya wanafunzi, eneo hili nimekodi nalipia Sh200,000 kwa mwezi, nina walimu watano na mlezi mmoja,” anasema Mwendapole.

Mmiliki wa kituo hiki akaamua kufuta maandishi yalotaka kifungwe.

Wasemavyo wamiliki wa shule

Msimamizi wa kituo cha Gracian Nursery School ambacho ni miongoni mwa vilivyofungiwa, Grace Deogratius anasema hatua hiyo imechukuliwa ghafla hivyo imewaweka katika wakati mgumu.

“ Walipita na gari la matangazo na kuja kuandika kuwa wamefunga, imetusababisha usumbufu kuna ada za watu tulishachukua. Tulikuwa na wanafunzi 40 wa shule ya awali na sita wa darasa la kwanza, labda wangetupa muda hadi Januari mwakani tujirekebishe,”anasema.

Kwa upande wake, mmiliki wa kituo cha Planet Earth Day care Edda Mwaipyana anasema alikatishwa tamaa ya kusajili kituo chake baada ya kuombwa rushwa.

“ Kituo hiki nimekianza tangu mwaka 2012, kuna siku walikuja madiwani hapa kunitembelea, wakaridhika na hali waliyoikuta ikiwamo ukubwa wa eneo langu, hivyo wakanishauri niende kwenye ofisi husika ili nisajili,”anasema.

Anaeleza kuwa alianza kuufanyia kazi ushauri huo, lakini alishtuka siku moja kiongozi mmoja wa kata akiwa ameongozana na mtu mwingine walipofika na kumtaka awape rushwa ya Sh 2.5 milioni ili apate usajili.