Maeja; Kutoka uchungaji hadi Mwenyekiti Stand United

Muktasari:

Nini kilimsukuma kuwania uenyekiti wa Stand United, Dk Maeja anasema baada ya kuona inasuasua, baadhi ya wadau walimshauri kujitosa kugombea wadhifa huo klabu hiyo uchaguzi utakapoitishwa.

Dk Ellyson Maeja, siyo jina geni masikio mwa wadau wa soka, huyu ndiye mwenyekiti wa Stand United ambaye uongozi wake uligubikwa na mizengwe sanjari na kuifanya klabu hiyo kugawanyika.

Nini kilimsukuma kuwania uenyekiti wa Stand United, Dk Maeja anasema baada ya kuona inasuasua, baadhi ya wadau walimshauri kujitosa kugombea wadhifa huo klabu hiyo uchaguzi utakapoitishwa.

“Waliona umuhimu wangu na uwezo wangu wa uongozi, kwani kabla niliwahi kuwa kiongozi wa timu ya RCC ambayo baadaye ilibadilishwa jina na kuitwa Biashara kisha Shinyanga Shooting Stars.

“Shinyanga Shooting Stars ilikuwa na mafanikio makubwa, tuliweka mikakati ya kila Sh1 kwenye lita moja ya petroli itakayonunuliwa Shinyanga itakwenda kuisaidia Shinyanga Shooting Stars.

“Tulishirikiana na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa wakati huo na ofisa biashara wa mkoa, Shinyanga Shooting Stars ikawa tishio, hivyo kumbukumbu ile haikuwa imeondoka kwa wadau wa soka, Shinyanga ndiyo sababu walinishahuri nigombee kuinusuru Stand United,” anasema.

 

Asimulia alivyoacha uchungaji

Wakati anagombea Stand United, Dk Maeja anasema alikuwa mchungaji wa mtaa katika Kanisa la Waadventista Wasabato mkoa wa Shinyanga kwa miaka 10.

“Niliingia kuongoza Stand kwa sababu napenda soka, nilikuwa mchungaji wa Wasabatho baada ya kuingia katika soka nikaomba nipumzike na uchungaji sababu ni kazi inayohitaji muda zaidi,” anasimulia.

 

Aanika mgogoro wa Stand

Dk Maeja anasema wakati anaingia kuwa mwenyekiti ndipo figisu figisu zikaanza na uongozi wao kushinda kesi.

“Tukiwa tunajipanga sasa kuanza kazi, wadhamini wa Stand United wakajitoa, kiukweli tulikuwa katika wakati mgumu. “Hatukuwa na namna zaidi ya kuendelea na safari yetu kiugumu, likaibuka suala la mishahara ya wachezaji na kocha.

“Viongozi waliopita waliingia mkataba na mdhamini bila kuwa na mwanasheria, sasa baada ya mdhamini kujitoa tukarudi kwenye mkataba, ikaonekana malipo yote ya makocha na wachezaji yanafanywa na klabu na si mdhamini.

“Hicho kikawa kinatufunga, hatuna jinsi wala uwezo wa kumlipa kocha Mzungu Sh15 milioni kwa mwezi.

“Pale ndipo tabia ya uswahili ilipoanza katika timu yetu, kocha Mzungu hakuvumilia malipo ya ahadi, hatukuwa na jinsi zaidi ya kuvunja naye mkataba kwa kuwa hatuwezi kumlipa, lakini kiukweli ni kocha mzuri na tumeishi naye vizuri,” anasimulia historia yake nje ya soka.

Dk Maeja alizaliwa miaka 52 iliyopita Ukerewe mkoani Mwanza akiwa mtoto wa kwanza kati ya tisa .