Mafanikio ya mradi wa gesi asilia yatakuwa kivutio cha uwekezaji

Muktasari:

Kuimarika kwa usafirishaji wa bidhaa nje utakaochangiwa na miundombinu ya imara inayoendelea kuwekezwa ni miongoni mwa mambo mtambuka yanayotarajiwa kujitokeza endapo azma hiyo itafanikishwa.

Serikali imekuwa ikizungumzia dhamira yake ya kuwa na maendeleo ya viwanda kwa kuweka kipaumbele katika uzalishaji wa bidhaa, kuongeza ajira kwa wananchi na mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa.

Kuimarika kwa usafirishaji wa bidhaa nje utakaochangiwa na miundombinu ya imara inayoendelea kuwekezwa ni miongoni mwa mambo mtambuka yanayotarajiwa kujitokeza endapo azma hiyo itafanikishwa.

Hata hivyo, kwa nchi yoyote yenye matamanio ya kuwa na uchumi imara, kupata uwekezaji mkubwa, uwe wa ndani au kutoka nje ni jambo muhimu.

Tanzania kama zilivyo nchi nyingine zinazoendelea inatakiwa kuwashawishi wafadhili kusaidia utekelezaji wa miradi mikubwa yenye manufaa ya muda mrefu kuongeza kasi ya kufanikisha malengo yake.

Nguvu ya nishati

Mradi wa gesi asilia na iliyosindikwa Tanzania (TGP) ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya ujenzi wa miundombinu katika historia ya Tanzania na bila shaka utakuwa wenye ushawishi mkubwa zaidi.

Matumizi ya hazina kubwa ya gesi iliyopo nchini kutaongeza uwezo wa nchi wa kusafirisha nje rasilimali hiyo muhimu na kuboresha miundombinu ya ndani.

Mradi wa TGP ni mkubwa zaidi kujengwa Tanzania wenye fursa zitakazogusa maeneo mengi na kubadili maisha ya wananchi. Hata hivyo, maendeleo ya miradi mingine, dhana na mawazo inaweza kuwa inategemea kustawi kwa mradi huu wa TGP.

Kichocheo

Tanzania ni nyumba ya maajabu mengi ya asili duniani. Kwa juu juu unaweza ukafikiria mvuto wa Serengeti, Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro. Lakini, pamoja na kuwa ni vivutio vinavyopendeza, baadhi ya maumbile ya asili ya Tanzania yaliyo na umuhimu wa kipekee yanaweza kutumika kuzalisha nishati kuwatosheleza maelfu ya wananchi.

Utafiti wa watalaamu wa uhandisi na teknolojia unasema Tanzania inaweza kuzalisha megawati 480 za umeme wa maji kutokana na maporomoko peke yake.

Wakati miradi ya umeme wa maji mara nyingi inakuwa vigumu kuitekeleza, inakuwa na uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii nyingi za vijijini na kubadilisha maisha kwa kuongeza muda na ubora wa uzalishaji mali na huduma. Kuwa na chanzo cha nishati kinachoaminika, kisichotetereka na ambacho ni rafiki wa mazingira, biashara katika eneo husika na wananchi wake wanaweza kunufaika.

Inaweza pia kuvutia kampuni kutoka nje ya eneo husika hata kushawishi mashirika kutoka kuwekeza kwenye fursa watakazoziona kutokana na mabadiliko yatakayojitokeza.

Hata hivyo, miradi ya nishati kama hiyo hugharimu kiasi kikubwa cha fedha na kupata uwekezaji kwa ujumla kunahitaji uhakika wa kurudisha mtaji utakaotuika. Hapa ndipo ustawi wa mradi wa TGP unapoingia.

Kuna fursa nyingi za kuboresha miradi ya sasa ya viwanda nchini kutoka vinavyosindika mazao ya kilimo hata ufugaji, nishati na ujenzi, mawasiliano na tekonolojia.

Kuimarika kwa maeneo hayo yote kutaonyesha na kudhihirisha manufaa ya mradi wa TGP kwenye uchumi wa Taifa na dunia kwa ujumla.

Taarifa za hivi karibuni zimeeleza kuwa Kiwanda cha Dangote kinatarajia kuanza kutumia gesi asilia kuzalisha saruji jambo litakaloshusha bei ya bidhaa hiyo nchini.

Hili linamaanisha vitu vingi kidogo. Kushuka kwa bei ya saruji kutarahisisha ujenzi wa makazi na miradi mingine inayotumia bidhaa hiyo. Kutokana na hilo, uchumi utatanuka.

Kushuka kwa gharama kutaongeza uzalishaji hivyo kuiruhusu sekta hiyo kutafuta soko la nje kwa bei shindani baada ya wazalishaji kuongeza ubora kukidhi mahitaji mapana ya bidhaa hiyo.

Mradi wa TGP utafanya zaidi ya kuchakata gesi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, viwandani na kusafirishwa nje ya nchi. Utaitangaza Tanzania kuwa na fursa za kuaminika za uwekezaji hivyo kutoa fedha ya kufadhili miradi mingine itakayoleta mabadiliko makubwa kwa nchi.

Kama tunataka kuuchukulia mradi huu kuwa ushindi, hautajenga tu viwanda vya gesi nchini bali utaweka viwango kwa miradi ya baadaye ya Tanzania kwenye sekta mbalimbali.

Uchumi

Shabaha ya mradi wowote wenye ukubwa wa TGP ni kuzalisha fursa za kiuchumi zinazoonekana ambazo zitawashirikisha wananchi wengi kuimarisha kipato chao.

Ni lazima utayarishwe kwa kuzingatia matakwa ya nchi mwenyeji na utoe manufaa yanayoenda zaidi ya kuivuna gesi asilia hiyo peke yake.

Kwa Tanzania, kwa uhakika hakuna uhaba wa matarajio au dira linapokuja suala la maboresho endelevu na mapana hata hivyo, kuwa na uchumi imara ni muhimu ili kufanikisha maendeleo ya viwanda.

Kuna fursa nyingi ambazo zinasubiri watu wa kunufaika nazo lakini kuvutia uwekezaji mkubwa ama kutoka ndani au nje ni muhimu mradi wa TGP ukaonyesha uwezo wa Tanzania kufanikiwa katika kutekeleza miradi yenye changamoto nyingi za kiteknolojia.

Kuna uwezekano mkubwa mradi wa TGP ukawa na mchango katika mageuzi ya kiuchumi nchini katika miongo kadhaa ijayo hivyo kuhakikisha mafanikio yake ni jambo muhimu kuliko yote.