Monday, October 30, 2017

Mafuru ataka mpira wa wavu umtoe

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Ubora wa vikosi vya Jeshi Stars na Magereza kwenye mpira wa wavu ni sawa na Simba na Yanga kwenye soka, kupata nafasi ya kucheza kwenye timu hizo sio jambo jepesi, Joseph Mafuru ni kijana ambaye amewashangaza wapenzi wa mchezo huo kwa kuingia haraka kwenye kikosi cha kwanza cha Magereza.

Vikosi vya Magereza na Jeshi Stars vilikuwa vimezoeleka kusheheni wachezaji wengi wakongwe lakini kwa kipindi cha hivi karibuni vijana nao wanaonekana kuamka.

Spoti Mikiki imezungumza na Mafuru ambaye ameyaweka wazi maisha yake na mchezo huo yalivyo pamoja na alivyoweza kwa haraka kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha timu yake.

“Nilizaliwa April 28, 1996 mkoani Mara wilaya ya Bunda katika kijiji cha Majita kabila langu ni Mjita. Elimu ya msingi niipata shule ya msingi Bwiru iliyopo Mwanza na nikachaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari ya Mnarani iliyopo Mwanza.

“Baada ya kumaliza kidato cha nne, 2011 nikajiunga na chuo cha elimu ya biashara( CBE)mwaka 2012. Safari rasmi ya kuanza kucheza mpira wa wavu ilianza kidato cha nne na nilikua nikiichezea timu ya B.O.T iliyopo jijini Mwanza, niliitumikia timu hiyo kwa miaka miwili na kushiriki katika mashindano mbalimbali.

“Nakumbuka kwenye Ligi ya Mkoa tulitwaa ubingwa na kupata tuzo binafsi ya mtengenezaji bora (best setter) pia nilichaguliwa timu ya chuo na kwenda nayo katika Michezo ya vyuo (SHIMIVUTA) mkoani Tanga,” anasema Mafuru.

Huko ndipo nilipo mvutia kocha wa Magereza, Edwin Masinga ambaye naye aliamua kunijumuisha kwenye kikosi cha Magereza 2014.

“Nilijiunga na timu hiyo na nikabadilishiwa nafasi nikawa mshambuliaji wa pembeni ninashukuru Mungu nimefanya vizuri katika nafasi hiyo na katika ligi ya mkoa wa Dar es Salaam, 2017 nimechaguliwa kuwa mshambuliaji bora na kuiwezesha timu yangu kutwaa ubingwa.

“Mambo yaliyonisaidia kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza ni kujifunza kupitia wengine.Ndoto yangu ni kuwa mchezaji wa kulipwa nje ya nchi na sio vinginevyo,” anasema.

-->