Thursday, April 20, 2017

Maji ya mvua yakivunwa yatapunguza majanga

Joseph Alphonce  ni Mtakwimu na Ofisa Mipango.

Joseph Alphonce  ni Mtakwimu na Ofisa Mipango. Anapatikana kwa 0685214949/0744782880. 

By Joseph Alphonce jmalphonce@gmail.com

Kwa mujibu wa Shirika la Mazingira Duniani (Unep), takriban watu bilioni mbili duniani watakuwa hawana uhakika wa kupata maji ya kutumia ifikapo mwaka 2050. Mwaka huo maji yatakuwa bidhaa adimu katika mataifa mengi duniani.

Takwimu za mwaka huu zinaonyesha takriban watu bilioni 1.5 duniani, hawapati huduma ya maji safi na salama. Idadi hiyo ni kubwa kuliko ya watu wote waliopo Afrika wanaokadiriwa kuwa bilioni 1.2 sawa na asilimia 16 ya dunia nzima.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kiwango cha uchafuzi wa maji kimekuwa kikubwa, upungufu wa maji na mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuisumbua dunia katika karne ya 21.

Ukweli kuwa tupo kwenye janga la ukosefu wa maji kuanzia sasa na miaka ijayo haliwezi kupuuzwa. Kila Mtanzania kwa sasa anapata wastani wa mita 1,952 za ujazo kwa mwaka ambacho ni juu ya kiwango cha chini cha mita za ujazo 1,700 kimataifa.

Kiwango hicho kinatarajiwa kupungua hadi wastani wa mita 883 za ujazo kwa kila Mtanzania mwaka 2035, kama jitihada na mikakati ya kushughulikia changamoto zilizopo hazitachukuliwa.

Kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na majanga ya asili na shughuli za binadamu kwenye vyanzo vya maji, maeneo mengi yamekuwa yakipata mvua chini au juu ya kiwango kilichotarajiwa. Ukame na mafuriko yamekuwa sehemu ya maisha ya binadamu wa leo.

Teknolojia ya kuvuna maji ya mvua ni rahisi isiyo na gharama kubwa, ambayo inaweza kuleta usawa kati ya maeneo yanayopata mafuriko na yale yenye ukame. Ripoti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji mwaka huu wa fedha, inaonyesha kuwa Serikali imetoa miongozo kwa taasisi zake kuangalia uwezekano wa kuvuna maji.

Miongozo hiyo inazielekeza halmashauri kutunga sheria ndogo zitakazozitaka taasisi za jamii, asasi za kiraia na watu binafsi kujenga miundombinu ya uvunaji maji ya mvua kwenye majengo na maeneo yao.

Ujenzi wa matangi ya kuvunia maji ya mvua yajengwe vituo vyote vya kutolea huduma za afya, taasisi za elimu, mahakama, ofisi zote za Serikali na miradi ya sekta binafsi. Pamoja na maelekezo hayo, kila halmashauri inatakiwa kila mwaka kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa angalau bwawa moja la kuvunia maji ya mvua.

Kama maelekezo haya yatazingatiwa na kutekelezwa, uwezekano wa kupata maji safi na salama kwa ajili ya binadamu, wanyama na mimea kipindi chote cha mwaka utakuwa mkubwa. Wataalamu wa sekta ya maji wanatabanaisha kuwa, uvunaji wa maji ya mvua ni salama na rahisi zaidi kuliko uchimbaji wa maji ardhini.

Wakati mwingine uchimbaji wa maji ardhini husababisha uwiano usio sawa wa mfumo wa maji (hydrological imbalance), au kupata maji yenye ubora hafifu na uhitaji wa nishati ya umeme kwa ajili ya kuvuta.

Uvunaji maji ya mvua umekuwa ukifanyika tangu miaka mingi ya nyuma kwa kutumia teknolojia rahisi na isiyohitaji gharama kubwa. Hata sasa mvua inaponyesha, kaya hutoa vifaa na kuvuna maji yanayodondoka kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Changamoto iliyopo, ni kwamba hufanyika kwa kiwango kidogo.

Badala ya kuyaacha maji yakatiririka na kupotea, yakivunwa na kuhifadhiwa yanaweza yakatumika kwenye maeneo yenye ukame au baadaye masika yakiisha. Uvunaji huu huisaidia Serikali kuokoa fedha nyingi ambazo zingeelekezwa kwenye uchimbaji wa visima na kutibu magonjwa yatokanayo na maji yasiyo safi na salama.

Ngazi ya familia inaweza kuwekewa mazingira wezeshi, ikiwamo elimu ya uvunaji na uhifadhi wa muda mrefu wakati jamii inaweza kuchagua eneo maalumu na kuliwekea miundombinu ya uvunaji maji hayo.

Serikali ijenge mabwawa makubwa ya kuvunia maji. Kuna faida kadhaa za kuvuna maji haya ikiwamo uhakika wa upatikanaji maji hasa masika, kuepuka mafuriko, kujaa kwa udongo au mchanga mtoni, ziwani na baharini.

Hii ni njia ya kuepuka uchafuzi wa maji ardhini na kuongeza ubora wa maji, hivyo kuyafanya yasiwe na kemikali nyingi. Uvunaji huu hauhitaji umeme kuufanikisha.

Faida nyingine ni kupunguza uwezekano wa kutokea mmonyoko wa udongo. Kuna kila sababu ya Tanzania kuwekeza kwenye teknolojia hii nyepesi ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua. Watafiti wengi wameandika juu ya uhaba uliokithiri wa maji miaka michache ijayo.

Tuwekeze sasa kwenye uvunaji maji ya mvua. Utashi wa kisiasa unahitajika ili kutekelezwa, kwani ni suala linalomgusa kila raia bila kujali cheo, dini, kabila, wala chama. Tuvune maji ya mvua yatufae baadaye.

Umuhimu wa kutekeleza miradi ya namna hii inatokana na ukweli kwamba, mmaeneo tofauti nchini hukumbwa na mabadiliko tofauti.

Wakati Dar es Salaam kukikumbwa na mafuriko, kwa mfano, mikoani huwa kukavu hivyo kutoa fursa ya kuvuna maji ya mvua na kuyapeleka sehemu yenye uhitaji.

Iwapo umakini utakuwapo, hakuna mahali patakapokuwa na ukame wala mafuriko, jambo litakalofanikisha kilimo cha uhakika mwaka mzima.

Mwandishi ni mtakwimu na ofisa mipango wa wilaya.

-->