Makamba atumia dakika 30 kupangua hoja kuhusu kero za Muungano bungeni

Muktasari:

  • Katika mjadala huo wabunge walihoji juu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kutokuwa na dhamira ya kuisaidia Zanzibar kiuchumi, vikwazo vya kupeleka bidhaa kutoka upande mmoja kwenda mwingine, Zanzibar kutopata mikopo, utozwaji wa kodi, usajili wa meli na magari.

Licha ya wabunge hasa wa upinzani kuchachamaa kuhusu kero za Muungano, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba ametumia dakika 30 kujibu hoja hizo walizozieleza wakati wa mjadala wa bajeti ya ofisi hiyo kwa mwaka 2018/19.

Katika mjadala huo wabunge walihoji juu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kutokuwa na dhamira ya kuisaidia Zanzibar kiuchumi, vikwazo vya kupeleka bidhaa kutoka upande mmoja kwenda mwingine, Zanzibar kutopata mikopo, utozwaji wa kodi, usajili wa meli na magari.

Makamba baada ya kutoa ufafanuzi wa kero hizo na jinsi zinavyoshughulikiwa na pande zote mbili, alilazimika kutumia mifano ya jinsi Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume walivyounda Muungano, akiwashawishi wabunge kuridhia kupitisha kwa bajeti hiyo ya Sh21 bilioni.

Akizungumzia kuhusu madai kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano haina dhamira ya kuisaidia Zanzibar kiuchumi na kubana fursa ya biashara na uchumi wa Zanzibar, amesema kihistoria hata kabla ya uhuru, mahusiano kati ya Bara na Zanzibar msingi wake mkuu ulikuwa biashara.

“Muungano umekuja kurasimisha mambo yaliyokuwepo tangu zamani. Watu wengi wa Bara ambao wapo Zanzibar, miaka mingi walikwenda kule kwa sababu ya biashara na hata watu wa Zanzibar waliokaa Bara sababu kubwa iliyowaleta ni biashara,” amesema.

“Fursa za biashara tunazozizungumza sasa hivi ziko za aina mbili, kwanza ni uwezo na urahisi wa kusafirisha bidhaa kati ya pande hizo mbili, pili ni uwezo na urahisi wa mtu yeyote kutoka upande wowote kwenda kuishi upande wowote kwa urahisi zaidi na kuanzisha biashara.”

Amesema tunapotafakari mchango na hatua za Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuwezesha ukuaji wa uchumi na ustawi wa watu wa Zanzibar ni lazima kutazama suala la pili la fursa za biashara.

“Huwezi kuuondoa Muungano katika ustawi wa watu wa Zanzibar, unaotokana na urahisi wa watu wa Zanzibar kuja Bara kufanya biashara na kushamiri. Tunafurahi kuona Wazanzibari wengi zaidi wanakuja kuishi Bara na kustawi na kusaidia Zanzibar,” amesema.

“Wazanzibari walioko Bara sasa hivi ni wengi zaidi kuliko Wazanzibari wote walioko kisiwani Pemba. Miaka 20 ijayo Wazanzibari wanaoishi Bara wanaweza kuwa wengi kuliko Wazanzibari wote wanaoishi Zanzibar. Huo ndio Muungano na hilo ni jambo jema, katika mazungumzo ya ustawi wa Muungano tusisahau fursa ya biashara.”

Kuhusu vikwazo vya kupeleka bidhaa katika pande zote mbili, Makamba amesema jambo hilo lina changamoto zake zinazotokana na taasisi za udhibiti zikiwemo, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Jambo hili Serikali tumeanza kulifanyia kazi kwa kukutana na taasisi za udhibiti za pande zote mbili. Anaposimama mbunge na kusema hatujafanya lolote katika jambo hili nasikitika sana,” amesema Makamba.

“Suala la biashara kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, Serikali ya Muungano inalijua inalishughulikia na inaendelea kulishughulikia.”

Makamba pia alizungumzia hoja ya mbunge wa Magomeni (CCM), Jamal Kassim Ali aliyehoji sababu za ucheleweshwaji wa kutoa kibali cha mkopo wa miradi ya kimkakati Zanzibar, ukiwepo uendelezaji wa jengo la Terminal II katika uwanja wa ndege visiwani humo.

“Ni kweli kuna changamoto ya kuongeza mkopo mwingine wa kumaliza ujenzi wa jengo la uwanja wa ndege. Mchakato wa kutoa mikopo serikalini una hatua mbalimbali. Moja ya hatua za mwisho ni mkopo kupitishwa na kamati ya madeni ya Taifa,” amesema.

“Mapema mwezi huu kamati hiyo ilipitisha na kukubali Serikali ya Jamhuri ya Muungano ikope Dola 58milioni za Marekani kumalizia ujenzi huo, jambo hilo litakwisha na halitakuwa hoja tena. Kuhusu mradi wa bandari ya Mpigaduri ni kwamba bado kuna maelezo ya kitaalamu yanahitajika ili kujenga hoja zaidi tunakokopa fedha.”

Amesema mikopo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayokwenda kufanya miradi Zanzibar bado marejesho ya fedha yanalipwa na Serikali ya Muungano.

Kuhusu watu wanaotoka Zanzibar kuja Bara kutozwa kodi amesema, “Ni kweli kuna usumbufu na tunapaswa kuwa na mfumo mmoja wa forodha kwamba ukiingiza bidhaa kituo cha forodha cha Zanzibar kutoka Dubai iwe sawa ukiingiza gari Tanga kutoka Dubai.”

“Tumeweka mfumo wa pamoja wa kuthamini kodi lakini hatujaanza kuutumia, Mfumo huu una database ya thamani ya bidhaa zote duniani. Lengo ni kodi kuthaminishwa kwa pamoja ii usilazimike kuonekana umelipa mara mbili ukija Bara. Kuna baadhi ya mambo madogo ya kitaalamu yamebakia tuna kikao mwezi huu kuhusu hili.”

Amesema mbali na hilo katika vituo vya forodha kuna ukorofi wa wahusika kuwasumbua wananchi, “inawezekana mtu akili hana lakini hata macho hana kuona mizigo binafsi na si biashara. Mchango wa watu kuharibu mambo ni mkubwa sana.”

Makamba amezungumzia suala la usajili wa meli na kubainisha kuwa si kweli kuwa Zanzibar imenyang’anywa kusajili wa meli.

“Kinachofanywa zoezi la usajili wa meli liwe shirikishi maana wengi tunajua meli zimekamatwa na mihadarati, silaha na kutia nanga katika bandari zilizozuiwa. Katika hili tumetishiwa kuwekewa vikwazo vya kiuchumi kama nchi, meli zingekutwa na watu wakisafirishwa (biashara ya kusafirisha binadamu) ndio ingekuwa shida zaidi,” amesema.

“Mamlaka ya kusajili meli za nje ni ya nchi, lakini huko nyuma kulikuwa na makubaliano kuwa Zanzibar itafanya kwa niaba ya Tanzania na itabaki na mapato, kilichofanyika ni sahihi iendelee kuwa ya waziri wa Zanzibar, lakini vyombo vya usalama vishiriki, meli zinazoomba bendera ya Tanzania tuzijue, zinatoka nchi gani, zinataka kufanya shughuli gani ili kulinda sifa ya nchi yetu.”

Amesema kutokana na makosa ya meli hizo Tanzania ingenyang’anywa usajili wa meli hizo na kukosa mapato.

“Kuhusu usajili wa vyombo vya moto. Sisi tunataka gari ikisajiliwa Zanzibar iwe sawa na imesajiliwa Bara na ikisajiliwa Bara iwe sawa imesajiliwa Zanzibar. Tulifikisha suala hili serikalini, lakini jambo hili linahusisha kodi. Katika mabadiliko ya sheria mchanganyiko suala hili litaingizwa ili kubadili sheria,” amesema.

“Nakubaliana na wabunge ni aibu gari ya Zambia kutembea kwa urahisi Tanzania kuliko gari ya Zanzibar. Jambo hili tutalirekebisha.”