Makosa saba ambayo huwagharimu watawala wapya na serikali zao

Muktasari:

MWANGWI WA KAMPENI

Lazima kufahamu kuwa kipindi cha kampeni na baada ya kula kiapo cha utumishi ni nyakati mbili zenye utofauti mkubwa. Watawala wengi wapya wakishaingia madarakani huendelea kuteswa na mwangwi wa kampeni.

Kipindi cha kampeni ni cha kujiuza ili ukubalike na uchaguliwe, ukishakula kiapo tayari unakuwa mtoa huduma. Hivyo basi, hutakiwi tena kuendelea kuzungumza badala yake unatakiwa kuyafanya maneno yaonekane kuwa kweli.

Watawala wengi wapya husumbuliwa na mwangwi wa kampeni, matokeo yake huendelea kuzungumza katika sura ya kutaka kuungwa mkono na wananchi. Mtawala akishakabidhiwa ofisi hatakiwi kuzungumza, bali hupaswa kutafsiri maneno yake kwa vitendo.

Wakati wa kampeni mgombea hutoa ahadi ya yale ambayo atayafanya. Mtawala akishakula kiapo na kukabidhiwa ofisi hutakiwa kutenda kwanza. Baada ya utekelezaji ndipo mtawala anatoa ripoti ya mafanikio ya utendaji wake. Mtawala akipenda kuzungumza, maana yake anakuwa bado yupo kwenye kampeni.

Kila mtawala huingia madarakani akiwa na ndoto kubwa. Ari ya kutaka aonekane kiongozi wa mfano ni sababu ambayo imewagharimu wengi. Bahati mbaya kuna makosa yenye kufanana ambayo yamekuwa yakifanywa mara kwa mara.

Kutoka utawala mmoja hadi mwingine katika nchi mbalimbali duniani, kila mabadiliko ya uongozi yanapofanyika kutoka kwa Serikali kupata kiongozi mpya mambo huwa yaleyale.

Kwa kusikiliza hotuba ya Rais wa 45 wa Marekani, Donald Trump kisha kuunganisha uamuzi ambao aliufanya baada ya kumaliza kukagua gwaride la kumtambulisha kama Amiri Jeshi Mkuu mpya wa nchi hiyo, inajenga picha dhahiri kuwa kiongozi huyo amejiandaa kukosea.

Hotuba ya Trump ilikuwa inajenga picha kuwa Marekani imepata ukombozi. Utadhani nchi haikuwa huru. Alitengeneza tafsiri kuwa kikundi kidogo cha watu kimekuwa kikifaidi mkate wa uongozi kutoka Washington DC, kwa hiyo yeye ndiye anaingia kubadili hali hiyo.

Trump ameahidi kuwa sasa Serikali ni kwa ajili ya watu. Kwamba raia wote wa Marekani ndiyo watakuwa watawala katika Serikali ambayo anaiongoza. Amewajengea matumaini na matarajio wananchi.

Mwaka 1994, Rais mzalendo wa kwanza Afrika Kusini, Nelson Mandela, baada ya kushinda urais na kumaliza utawala wa kikaburu, aliahidi kujenga nyumba milioni moja za bei nafuu ili ziwasaidie wananchi wa taifa hilo kumudu makazi.

Ahadi hiyo aliitoa baada ya kuwepo watu wengi wasio na makazi. Mandela aliahidi kuwa nyumba hizo zingejengwa ndani ya miaka yake mitano ya uongozi. Aliahidi kuongoza kwa miaka mitano tu, kwa hiyo akasema mwaka 1999, nyumba hizo zingekuwa zimekamilika.

Mandela alitoa ahadi hiyo bila kujua ugumu wa utekelezaji wake. Aliamini ukishakuwa Rais kila kitu kinawezekana. Mwaka 1999 wakati anaondoka madarakani, Mandela aliweza kujenga nyumba 40,000 tu. Na aliacha zaidi ya watu milioni sita hawana makazi.

Ahadi nyingine ambayo Mandela aliitoa ni kugawa asilimia 30 ya ardhi kwa wananchi. Baada ya kukaa madarakani na kuuona ugumu wa kazi ya Rais ulivyo, aliona ahadi hiyo haitekelezeki na kweli hakuitelekeza.

Si kwamba Mandela alikuwa na nia mbaya, la hasha! Dhamira ilikuwa njema mno, tatizo ugeni wake ofisini ndiyo ulimfanya aahidi mambo makubwa yaliyomshinda. Ni kama ambavyo Trump alivyoahidi. Ugeni wa ofisi unamsumbua, atakapoanza utekelezaji ndiyo makosa yataonekana.

Kuna makosa saba ambayo watawala wengi wapya huyafanya kutokana na ugeni wao kisha baada ya muda hujikuta wameharibu ofisi au hata kutenda chini ya matarajio.

Msukumo wenye papara

Katika kampeni unaweza ukaahidi mambo mengi lakini baada ya kushinda na kuapishwa hutakiwi kuwa na papara ya utekelezaji. Mtawala mpya hutakiwa kwanza atulie aisome ofisi aone ugumu na urahisi wake.

Watawala wengi wakishaingia madarakani huwa na moto wa kufanya mabadiliko. Moto huo ndiyo huwafanya wazungumze au wafanye uamuzi wa papara. Hasara ya papara hiyo hujionesha baadaye.

Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama, Agosti mwaka jana alipokuwa anamwombea kura aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Democrats, Hillary Clinton, alisema: “Huwezi kuujua ugumu wa kazi ya Rais mpaka uwe umeshakalia dawati la ofisi ya Rais, The Oval Office.”

Tafsiri ni kuwa ukishakuwa Rais ndiyo unajua urais ulivyo. Kumbe hata yeye Obama kuna mambo alijua ni rahisi na aliyatamka lakini baada ya kulizoea dawati la Rais ndipo akagundua ugumu wake. Obama aliahidi angeifunga Guantanamo Bay ‘Gitmo’, lakini amemaliza miaka nane ya uongozi wake bila kutekeleza hilo.

Papara ya kuzungumza na kufanya uamuzi wa haraka, husababisha watawala wengi washindwe mapema. Ni mwongozo kwa mtawala akishakula kiapo, awe mtulivu na awahudumie wananchi bila papara.

Ahadi za ukombozi

Watawaka wapya wengi kutokana na ugeni wao, huamini kuwa wanaweza kubadili kila kitu. Hali hivyo, huwafanya wakosoe mambo mengi na kuahidi zama mpya.

Kosa kubwa ambalo watawala wapya hufanya ni kujenga matarajio makubwa ya kiukombozi, kwamba wao kwa miaka yao ya uongozi watabadili kila kitu kisha kuijenga nchi mpya.

Zingatia kuwa muhula mmoja wa uongozi ni kati ya miaka minne mpaka mitano. Kutahamaki nusu muhula unamalizika wananchi hawaoni mabadiliko ya haraka ambayo walihubiriwa.

Unapokuwa mtawala mpya, ingia kama kiongozi unayepokea kijiti kisha ujitume kuwahudumia wananchi wako kwa nguvu zako zote. Maneno mengi ya kujitambulisha kama mkombozi mpya, huwagharimu wengi.

Juhudi za watangulizi

 Trump alipoketi kwa mara ya kwanza kwenye dawati la Rais wa Marekani, alianza kurekebisha mpango wa Serikali wa bima ya afya, maarufu kama Obamacare. Alifanya hivyo kwa sababu ilikuwa ahadi yake kwenye kampeni.

Trump alipaswa kujipa muda kidogo ili ajielimishe kuhusu Obamacare. Je, ni kwa nini Obama aliona umuhimu wa Serikali kubeba mzigo wa bima ya afya kwa ajili ya kuwasaidia Wamarekani hata maskini hupata huduma bora za afya bure?

Mtawala mpya anapoingia madarakani hupaswa kuheshimu juhudi za watangulizi wake. Anatakiwa kufahamu kuwa anakwenda kuanza pale ambapo wenzake waliishia. Siyo kufika na kutaka kuanza upya kila eneo.

Lazima kusoma na kujua mambo mazuri yaliyofanywa na watangulizi kisha kuyaendeleza, vilevile kung’amua mabaya na kuyafanyia marekebisho. Watawala wapya hukosea kwa kuwaweka mbali watangulizi wao.

Ni busara kwa mtawala mpya kushauriana na watangulizi wake mambo ya uongozi, maana nao watampa uzoefu wao kwa maeneo waliyokwama na walipofanikiwa na njia walizotumia.

Kusafisha Serikali nzima

Hili ni kosa ambalo hubeba pia gharama kubwa. Watawala wengi kwa kuvutwa na hamasa ya kufanya mabadiliko na kutenda tofauti na waliopita, huamua hata kujaza sura mpya serikalini.

Vizuri kufahamu kuwa unaweza kubadili sura zenye kutekeleza utashi wa kisiasa lakini siyo watendaji wa Serikali. Watawala wapya husahau kuwa Serikali ni moja isipokuwa utawala ndiyo hubadilika.

Watendaji wa Serikali katika tawala za nyuma ni muhimu kusaidia mambo mengi kwa uzoefu wao. Wakitumiwa vizuri watasaidia kutorudia makosa yaliyofanywa kabla na ni washauri wazuri.

Ukibadili mpaka watendaji wakuu wa Serikali, maana yake Serikali itakuwa na muda mrefu wa kujifunza kazi kabla ya kushika kasi. Miaka mitatu watu wanajifunza kazi, wakianza kushika kasi ni miaka miwili na uchaguzi unakuwa umewadia, hapo ahadi nyingi hazijatekelezwa.

Wasaidizi wawania urais

Watawala wapya hupaswa kufahamu kuwa kufanya kazi na watu ambao wana ndoto za urais ni gharama kubwa. Serikali inatakiwa kujikita kwenye kuhudumia watu, wakati mwenye kuupigia hesabu urais huitumia Serikali hiyohiyo kujisafishia kwa wananchi.

Hali hiyo husababisha mgongano wa maslahi. Rais anataka Serikali ihudumie wananchi, msaidizi wake mwenye kuutaka urais atataka huduma zitoke katika sura ya kumbeba kwenye mbio zake.

Watawala wanapokula kiapo, wakati wanapokuwa wanaandaa safu zao za uongozi, hutakiwa kuwabaini wenye ndoto za urais na kuwaweka pembeni ili wajiandalie mazingira nje ya Serikali.

Luqman Maloto ni mwandishi wa habari, mchambuzi na mshauri wa masuala ya kijamii, siasa na sanaa. Ni mmiliki wa tovuti ya Maandishi Genius inayopatikana kwa anwani ya mtandao www.luqmanmaloto.com