Makosa wanayofanya wakulima na wafugaji

Mkulima huyu yupo shambani mwenyewe akiwajibika. Baadhi ya wakulima hasa wafanyakazi mijini, hawana muda wa kwenda shamba japo kwa ratiba maalumu. Picha na chekahfarm.wordpress.com

Muktasari:

KUMBUKA
Siri ya  mafanikio kwenye kilimo ipo katika mambo makuu matatu
1. Maarifa kuhusu kilimo
2. Mtaji wa kuendesha kilimo
3. Menejimenti ya mradi

Watanzania wanakichangamkia kilimo. Wamegundua kuwa zama hizi mtu anaweza kutoka kwa haraka kimaisha kwa kujihusisha na shughuli za kilimo na ufugaji.

Ni hatua nzuri kwa kuwa imebadili fikra za Watanzania kuwa maisha siyo lazima kuajiriwa.

Hata hivyo, uzoefu unaonyesha watu wengi wamekuwa wakikimbilia shughuli hizi pasipo kuwa na maandalizi ya kutosha. Ni kweli kilimo ukikipatia kinalipa, lakini ni kwa wale wanaofuata kanuni.

Makala haya yanaangazia baadhi ya makosa makubwa yanayofanywa na watu walioamua kuchangamkia fursa zilizopo kwenye kilimo na ufugaji.

Kuwapa kisogo wataalamu

Watu wengi wanapenda kulima na kufuga lakini hawapo tayari kuwatumia wataalamu kuanzia mwanzo mwa miradi yao hadi mwishoni.

Wanahofia gharama, lakini hawajui kuwa gharama ya mtaalamu ndiyo faida na tija ya baadaye. Kwa mfano, ukimuona mtaalamu atakushauri aina ya udongo wa shamba lako na mazao ya kulima na menejimenti ya mazao hayo kama matumizi ya mbolea, umwagiliaji na mengineyo.

Kwa sababu ya hatuwatumii wataalamu, kwenye udongo unaofaa kwa mazao ya mbogamboga, mkulima analazimisha kupanda nafaka. Anapopata mavuno kiduchu, anatoa lawama zisizo na mipaka.

Ufugaji pamoja na kuwa unalipa, wafugaji wengi wanafikiria faida. Hawajui kuwa faida kubwa inaweza kupatikana kwa kumshirikisha mtaalamu wa mifugo atakayekushauri namna ya kuchagua vifaranga, ujenzi wa banda, namna ya kuwapa tiba na kinga na hata kukupa maarifa ya soko.

Kulima kwa kufuata mkumbo

Hawa ni wale wanaolima au kufuga kwa sababu wamesikia fulani amelima na amepata mafanikio, hata kama taarifa za mafanikio hayo siyo sahihi kwa asilimia kubwa.

Kuna watu wanalima kwa kuwa wamesikia kuna mashamba ya mpunga yanakodishwa Morogoro  au kwa sababu kuna watu wanalima vitunguu mkoani Manyara.

Kutojifunza kilimo

Siyo lazima usomee  stashahada au shahada ya kilimo, lakini mkulima makini anapaswa kujua  masuala ya msingi kuhusu  kilimo kama aina ya udongo na mazao anayolima, mbolea, utunzaji wa mimea, uvunaji, udhibiti wa magonjwa na wadudu na mengineyo.

 Kwa kuwa wengi hawana maarifa ya msingi kuhusu kilimo, imekuwa rahisi kudanganywa na watu wanaowasimamia mashamba yao.

Elimu ya kilimo pia inahusisha uwezo wa kutafuta masoko, kugundua masoko yaliyopo na yasiyokuwapo.

Elimu hii inapaswa kumwezesha kujua nini afanye soko likiyumba au likikosekana kabisa.

Aidha, elimu ya masoko itakuwezesha kujua nini ufanye ikiwa mazao uliyolima yamejaa  sokoni au wanunuzi wamekosa uwezo wa kununua kwa sababu ya hali ngumu ya maisha.

Kwa mfano, katika ‘usawa huu wa Magufuli’’ je, ni lazima mkulima auze bidhaa zake kwa bei ileile aliyokuwa akiuza wakati wananchi wengi walipokuwa na fedha mifukoni?

Ni elimu ya masoko itakayokuwezesha kujua lini upandishe na lini ushushe bei ya bidhaa zako.

Wasio na elimu ya masoko, ndiyo wale wanaoishia kutupa mazao yao au kuchoma moto, kwa sababu wamekosa mbinu mbadala za kunufaika na bidhaa zao japo kwa nusu hasara.

Kuamini taarifa za mitandao

Hivi sasa kuna tovuti, blogu na makundi mengi kwenye mitandao ya kijamii kama  whatsapp na facebook yanayojihusisha na utoaji wa taarifa kuhusu kilimo na ufugaji

Japo ni hatua nzuri, uzoefu unaonyesha kuna upotoshaji mkubwa unaofanywa kwenye mitandao hii.

Hii inajumuisha masoko, wataalamu feki, taarifa za uongo zikiwamo zinazohamasisha faida za kilimo pasipo kuonyesha uhalisia. Miongoni mwa taarifa hizi ni kama ile isemayo;  ‘ukilima matikiti ekari moja utapata milioni 30!

Kulima kwa simu

Hii inawahusu watu walio mijini waliohamasika kulima lakini kwa kuingia mguu mmoja.

Hawana muda wa kwenda shambani, hivyo wanaishia kutoa maagizo au kupokea maagizo kwa njia ya simu.

Wataalamu wanasema mkulima makini ni yule  anayekwenda shambani. Inawezekana isiwe muda wote hasa ukiwa na shughuli nyingine, lakini lazima uwe na utaratibu wa kutembelea miradi yako mara kwa mara.

Hata hivyo, matumizi ya simu kama chombo cha mawasiliano ya sasa yanawezekana kwenye kilimo, ikiwa shamba lina usimamizi madhubuti wa mtaalamu kama vile meneja anayefanya kazi kwa niaba yako.

Mafanikio ya haraka

Hili ni sawa na donda ndugu, watu wengi hawataki changamoto kwenye kilimo.

Wanataka walime leo wavune kesho, hawa ni wale inapotokea changamoto ya kiufundi au iliyo nje ya uwezo wa kibinadamu, wanakikimbia kilimo na kutoa lawama nyingi. Kilimo kinahitaji uvumilivu.

Ukweli ni kuwa unaweza ukalia kwa miaka mingi  katika kilimo, lakini kicheko cha siku moja kinaweza kukusahaulisha machungu yote uliyopitia. Hii ndiyo falsafa wanayotumia wakulima wanaotaka mafanikio.