Makubaliano na Barrick mwanzo wa kuamka usingizini kama Taifa

Muktasari:

  • Mbali na malipo hayo, Barrick pia imekubali kutoa Dola za Kimarekani 300 milioni kama malipo ya nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kutokana na biashara ya kampuni hiyo.

Hatua ya kampuni ya Barrick Gold kukubali kuilipa Serikali ya Tanzania hisa ya asilimia 16 na mgawo wa asilimia 50 ya mapato ya mauzo ya dhahabu kutoka migodi 3 inayoimiliki imechukuliwa kama ushindi kwa Rais John Magufuli aliyeapa kumbana katika vita ya uchumi nchini.

Mbali na malipo hayo, Barrick pia imekubali kutoa Dola za Kimarekani 300 milioni kama malipo ya nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kutokana na biashara ya kampuni hiyo.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo,Profesa Thornton amesema Barrick Gold Corporation watazingatia makubaliano haya na wanaamini kuwa yamefungua ukurasa muhimu utakaowezesha kufanya biashara kisasa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya kuchunguza mchanga wa madini maarufu kama Makinikia 1 iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma, Tanzania imepoteza takriban Sh188 trilioni (dola bilioni 84 za Marekani ) katika kipindi cha miaka 19 kati ya mwaka 1998 na mwaka 2017 kupitia usafirishaji wamakinikia ya dhahabu na shaba.

Kwa upande wake Rais wa Tanzania John Magufuli alisema makubaliano hayo yataisaidia nchi kuzalishaji ajira zaidi, kupata manufaa mbalimbali yanayostahili ikiwemo fedha za kugharamia huduma za kijamii kwa wananchi na yanajenga msingi imara ambao utaiwezesha Tanzania kunufaika na rasilimali zake za madini.

Katika taarifa yake ya Septemba 22 mwaka huu, kampuni hiyo ilieleza kusudio lake la kuanza kuchenjua mchanga wa dhahabu nchini, ikiwa ni kutii amri ya serikali kuwataka wasitishe kusafirisha makinikia nje ya nchi maana ilikuwa marufuku.

Kampuni hiyo pia ilikiri kuwa sehemu kubwa ya madini yaliyokuwa katika makinikia yale, yaliyokuwa yakisafirishwa nje ya nchi, ilikuwa ni dhahabu tofauti na kauli yao ya awali waliyosema na mabaki ya dhahabu kiasi kisichopungua 0.2.

Makubaliano hayo yamekuja baada ya Serikali kuishutumu Acacia kwa kufanya kazi ya uchimbaji nchini Tanzania kinyume cha sheria na kusema kuwa kampuni za uchimbaji madini zimekuwa yakikwepa kulipa kodi.

Kutokana na malalamiko hayo, Rais John Magufuli aliunda kamati mbili za madini ambapo ya kwanza iliongozwa na Profesa Abdukarim Mruma ikichunguza mchanga wa madini uliokuwa ukisafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya kuchenjuliwa.

Kamati ya pili iliyoongozwa na Profesa Nehemia Osoro ililenga kuchunguza upotevu wa mapato ya madini ya dhahabu tangu ilipoanza kuchimbwa mwaka 1998.

Baada ya kamati hizo kutoa ripoti zake kwa nyakati tofauti, Serikali iliialika kampuni ya Barrick Gold kuja kwenye mazungumzo ya kupitia upya mapato ya madini ikiwa pamoja na kuridhia mabadiliko ya sheria ya madini.

Mazungumzo hayo yaliyodumu kwa zaidi ya miezi miwili ndiyo yamekuja na taarifa za matumaini ya Tanzania kulipwa Dola 300 milioni kama malipo ya uaminifu, kugawana asilimia 50 kwa 50 ya faida na Serikali kuwa na hisa ya asilimia 16 kwenye migodi.

Akieleza manufaa ya kiuchumi kwa Tanzania kupitia makubaliano hayo, Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humphrey Moshi anasema huo ni ushindi kwa Rais John Magufuli na Watanzania kwa ujumla.

“Huo ni ushindi mkubwa kwa Rais John Magufuli na anapaswa kupongezwa na nishindi kwa Watanzania kwa Watanzania wote. Hata nchi zilizotuzunguka zilizokuwa zimelala sasa zitaamshwa na ushindi huo katika sekta ya madini,” anasema Profesa Moshi.

Anataja mambo yaliyoleta ushindi huo kuwa pamoja na kuwa na gawiwo la asilimia 50 katika faida itakayopatikana na uchimbaji wa madini pamoja na ubia wa asilimia 16 kwenye umiliki wa migodi.

“Barrick Gold wamekubali kuwa na ubia na Watanzania, wamekubali kujenga kile kiwanda cha kuchenjua madini nchini. kumbe ukiwa na timu nzuri ya majadilinao mambo yanakwenda vizuri . inaonyesha zamani hatukuwa na timu nzuri za majadiliano ndiyo maana hayakwenda vizuri. Hiyo ndiyo faida ya kuwatumia wasomi vizuri kwa manufaa ya Taifa,” anasema Profesa Moshi.

Akizungumzia kauli iliyotolewa na kampuni ya Acacia kupinga malipo ya Dola 300 milioni yaliyokubaliwa na Barrick, Profesa Moshi anasema hana wasiwasi kwa sababu kampuni iliyoamua ndiyo kubwa.

“Acacia ni kampuni tanzu ya Barrick Gold, baba akishaamua mtoto hawezi kukataa. Kwa hiyo mimi sina wasiwasi, watalipa tu.”

Mkurugenzi wa taasisi ya Fordia, Bubelwa Kaiza alisema hatua iliyofikiwa ni mwelekezo mzuri kwa Serikali ukilinganisha na hatua zilizopita.

“Katika awamu zilizopita kulikuwa na kamati sita zilizoundwa ikiwemo ya Mboma, masha, Kipenka na nyinginezo. Lakini zote hazikutoa suluhisho la kudumu kama kamati za sasa, kwa sababu zilikuwa zikishughulikia matatizo madogo madogo yaliyotokea wakati ule,” anasema Bubelwa.

“Kamati alizounda Rais Magufuli kwanza zililenga kutuandoa hofu ya kiasi cha madini yanayoibiwa na kweli ikatuonyesha na kamati ya pili ikaonyesha hasara tunayopata katika madini tangu yalipoanza kuchimbwa mwaka 1998. Matokeo yake yamekuwa mazuri kwani zimeundwa sheria Na.5,6,7 na Rais aliridhia mapendekezo yote ya kamati zote,” anasema.

Bubelwa anaongeza kuwa makubaliano kati ya Serikali na kampuni ya Barrick Gold ni kiashiria kwa kampuni nyingine za madini nchini kwani hakuna iliyo kubwa kuliko hiyo.

“Hii sasa ni Tanzania mpya na imetoa mwongozo kwa dunia nzuma,” anasema Bubelwa.

Kwa upande wake mchambuzi wa masuala ya uchumi Silas Olang anasema japo makubaliano yote hayajafikiwa lakini mwelekeo mzuri.

“Bado hatuwezi kusema kuwa tyumefika pale tunatakiwa kuwa, japo kwa kweli makubaliano ya msingi yamekubaliwa. Kwa mfano yale makubaliano ya kugawana faida 50 kwa 50 ni mazuri lakini bado hayajakamilika hasa ukimsikiliza Mkurugenzi wa barrack na Profesa Palamagamba Kabudi walisema ni mpaka ya kuwahusisha wanahisa. Tunajua Barrick ndiyo wenye hisa nyingi hivyo watakubali tu,” anasema Olang na kuongeza:

“Tunaelekea kama walikofika wenzetu Botswana, japo changamoto itakuwepo kwenye miradi mipya. Lakini kwa ujumla mmwelekeo mzuri,” anasema Olang.

Hata hivyo, wakati Tanzania ikijipiga kifua kufanikisha dili lake, Ofisa mkuu wa kitengo cha Fedha cha kampuni ya Acacia, Andrew Wray amesema kampuni hiyo haina uwezo wa kulipa Dola 300 kama ilivyokubaliwa.

Akizungumzia mkanganyiko huo, Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe anasema Serikali imefanya makosa kutangaza ushindi kwenye mazungumzo kati yake na kampuni ya Barrick Gold.

“Ni kawaida kwa kampuni ya Barrick kutoa ahadi ambazo wamezitoa jana (juzi). Mwaka 2006 walitoa kauli kama hiyo kwenye misamaha ya kodi walipokuwa wamebanwa bungeni na wamefanya hivyo kwa nchi kama Chile, Ecuador na Bolivia. Nishangaa sana kuona tunajazwa upepo,” anasema Zitto.

Anasema Serikali ilikosea kuzungumza na mmiliki wa kampuni badala ya kampuni yenyewe ambapo kwa mujibu wa sheria za kampuni, kila upande unaseimama kivyake.

“Jana taarifa ya Makamu Rais wa Barrick inaonyesha watatoa kishika uchumba cha Dola 300 milioni na jana hiyo hiyo jioni tukasikia Acacia wakasema lazima iende kwenye bodi yao na leo (jana) tunasikia wanasema hawana uwezo wa kulipa. Tunachezewa shere na haya ni makosa tuliyoyafanya kwa kutokutumia maarifa ya namna gani ya kushughulika na kampuni za kigeni,’ anasema Zitto.