Makundi mapya ya ushirika katika ardhi takatifu Israel

Muktasari:

  • Hali hiyo imeandikwa katika mtando wa Twitter na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Bahrain, Sheikh Khalid al-Khalifa, aliyesema baada ya kutokea kwa malumbano ya kijeshi wiki iliyopita baina ya Israel na Iran, dola ya kiyahudi ya Israel sasa ina haki ya kujitetea. Waziri huyo amesisitiza kwamba Israel inabidi ipigane dhidi ya kiini cha hatari inayokabiliana nayo.

Mzozo unaozidi kushika kasi kati ya Iran na Israel, sasa unadaiwa kuungwa mkono na upande ambao haukutarajiwa.

Hali hiyo imeandikwa katika mtando wa Twitter na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Bahrain, Sheikh Khalid al-Khalifa, aliyesema baada ya kutokea kwa malumbano ya kijeshi wiki iliyopita baina ya Israel na Iran, dola ya kiyahudi ya Israel sasa ina haki ya kujitetea. Waziri huyo amesisitiza kwamba Israel inabidi ipigane dhidi ya kiini cha hatari inayokabiliana nayo.

Dola ya Israel inaungwa mkono hadharani na upande ambao haijautarajia. Bahrain ambayo ni nchi ndogo mara nyingi hujifanya kama msemaji wa nchi kubwa jirani ya Saudi Arabia, tangazo la waziri huyo la kuiunga mkono Israel lilionekana kuwa ni zaidi ya maoni yake binafsi.

Israel na Saudi Arabia zinajongeleana zaidi na bila shaka, hali hiyo inaifurahisha Marekani. Lakini, kukaribiana huko baina ya Tel Aviv na Riyadh kuna mipaka yake.

Kwa macho ya Saudi Arabia ni kwamba Israel sasa inaiona Iran kuwa ndiyo hasimu wake mkubwa katika eneo la Mashariki ya Kati, licha ya kwamba Waarabu hivi sasa, kama walivyokuwa zamani, bado wanakataa kuitambua rasmi dola hiyo ya Kiyahudi. Mrithi wa Mfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, ameikubali haki ya kuweko dola ya Israel, na inadaiwa aliwahi kufanya ziara ya siri katika nchi hiyo.

Alipokutana hivi karibuni na wawakilishi wa Wayahudi wa Marekani inasemekana bin Salman alitoa matamshi ya kuwashushia heshima Wapalestina, jambo ambalo lililaumiwa hadharani na Waarabu.

Awali Israel ilifunga mikataba ya amani na nchi mbili tu za kiarabu za Jordan na Misri, mikataba ambayo bado ingaliko. Ushirika baina ya Israel na Saudi Arabia, unachochewa na serikali ya Marekani ya Rais Donald Trump. Mwana mkwe wa Trump ambaye pia ni mwakilishi wa Marekani katika mzozo wa Mashariki ya Kati, Jared Kushner, mchamungu wa Kiyahudi, ni rafiki binafsi wa Mohammed bin Salman.

Serikali ya Trump pia inaiunga mkono Saudi Arabia katika ugomvi wake na Qatar, nchi iliyoko katika Ghuba la Uajemi na inayolaumiwa kuwa na ushirikiano wa kirafiki na Iran.

Harakati za sasa za kuundwa makundi ya ushirika katika Mashariki ya Kati zinazifanya nchi nyingine nazo zisitulie. Baada ya Rais Trump kuamua kwamba nchi yake irejee kuiwekea vikwazo Iran, nayo Uturuki imeahidi kuiunga mkono Iran.

Katika mabishano baina ya nchi za Kiarabu, nayo Uturuki imesimama upande wa Qatar. Na katika upinzani mpya dhidi ya Iran, yaonesha Trump baada ya uamuzi wake wa kuitoa nchi yake kutoka mkataba wa kinyuklia na Iran, ameshangiriwa sana na Israel, Saudi Arabia na Bahrain. Waarabu wanahisi ushawishi wa Wairani hivi sasa katika Syria utakabiliwa na nguvu za jeshi la Israel.

Hata hivyo, bado haijawa wazi kama Israel na Saudi Arabia zitaendelea kwa pamoja kuwa nguvu mpya katika Mashariki ya Kati. Nchi hizo mbili zina maslahi yanayotafautiana. Siasa za ndani za Saudi Arabia na msimamo wa Israel kuelekea Wapalestina ni mambo yanayozuia kuendelezwa kwa haraka ushirika huo. Saudi Arabia ingependelea Iran ibanwe, lakini Israel inapendelea kushughulika zaidi na kukabiliana na hatari inayotokana na majeshi ya Iran yalioko Syria.

Mohammed bin Salman ana shida nyingine nchini mwake. Ilivyokuwa Wasaudi kwa miongo mingi ya miaka waliliweka suala la kuipinga Israel ndio msingi wa nadharia yao ya kisiasa, ni hatari sasa kuwabadilisha ili waikubali Dola hiyo ya kiyahudi.

Wananchi wa Saudi Arabia hawako tayari kusikia lolote juu ya wazo la kutaka wageuke na kuipendelea Israel. Hicho ni kitu ambacho kwa sasa ni shida kufikiriwa, hasa miongoni mwa wananchi wa kawaida wa ufalme huyo, na pia na mashehe ambao wana ushawishi mkubwa katika jamii. Maneno haya aliyasema Bilal Saab wa Taasisi ya Mashariki ya Kati ilioko Washington. “Na viongozi wa Saudi Arabia wanalitambua vilivyo jambo hilo“.

Iran inafanya kila inaloweza kuutumia upinzani huo wa wananchi wa Saudi Arabia dhidi ya Israel. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ali Khamanei, huitaja Saudi Arabia, mlinzi wa mwahala patakatifu kwa Waislamu (Misikiti ya Makkah na Madinah), kuwa ni “mtumwa“ wa Marekani. Kwa hivyo, mwanamfalme bin Salman angependa kupatikane suluhu baina ya Israel na Waarabu ambapo Israel ingekubali kuregeza kamba katika suala la kujengwa makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Wapalestina na katika masuala mengine ya mabishano. Pindi suluhisho hilo likipatikana basi yeye bin Salman ataweza kuwa na sababu ya nchi yake kuzidi kujongeleana na Israel. Lakini, hadi sasa serikali ya Benjamin Netanyahu haioneshi kuwa na hamu ya kulikubali wazo hilo.

Lakini, mambo sasa yanazidi kuvurugika katika wizani wa nguvu kati ya mahasimu huko Mashariki ya Kati. Uamuzi wa karibuni wa Rais Trump kuitoa Marekani kutoka Mkataba wa kinyuklia na Iran (uliotiwa saini pia na nchi nyingine zilizo wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa- Uingereza, Ufaransa, Urusi na China- pamoja na Ujerumani) umetia mafuta katika cheche za moto zilizokuweko.

Zaidi ya hayo, Trump ameshatia saini amri kwa nchi yake kurejea kuiwekea vikwazo Iran. Amezitaka pia nchi zinazofanya biashara na Marekani zisite kufanya biashara na Iran, ama sivyo kampuni za nchi hizo ambayo zinafanya biashara na Iran zitaadhibiwa na serikali ya Marekani.

Uamuzi huo wa Trump unaweza siku moja ukapelekea kutokea maafa makubwa katika eneo la Mashariki ya Kati kama ule uamuzi uliokwenda kinyume na sheria za kimataifa wa kuvianzisha Vita vya Iraq, jambo lililotekelezwa na Rais George W Bush wa Marekani mwaka 2003. Kama alivyofanya Bush wakati huo, mara hii Trump naye anatoa sababu za uongo ili kuhalalisha hatua zake dhidi ya Iran. Na pia kama alivyofanya na kusambaza uongo huo wa propaganda waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, siku chache zilizopita.

Madai ya Trump kwamba Tehran bado inaendelea na programu yake ya kinyuklia itakayopelekea siku moja kuwa na silaha za kinyuklia, yanakwenda kinyume na matamshi aliyoyatoa aliyekuwa mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na ambaye ni waziri wa mambo ya kigeni wa sasa, Mike Pompeo.

Kwa hakika, uamuzi wa Trump kuhusu Iran ni sawa na ule aliouchukua Bush kuhusu Iraq- nao ni kuzibadilisha tawala katika nchi hizo mbili. Nia ya Bush ilikuwa kumuondosha kutoka madarakani Rais Sadam Hussein wakati huo, na sasa Trump anataka kuuondosha kutoka madarakani utawala wa mashehe huko Tehran. Kwa kuiwekea vikwazo vya kiuchumi, lengo ni serikali ya Tehran iporomoke.

Trump ameitoa Marekani kutoka Mkataba wa kinyuklia, licha ya kwamba Iran imeuheshimu mkataba huo kwa kila hali, na licha kwamba nchi nyingine zilizotia saini mkataba huo zimethibitisha kwamba Iran imeyatekeleza vilivyo hadi sasa masharti yote iliyowekewa. Wacha ya Marekani, nchi nyingine zilizotia saini mkataba huo zimesisitiza kwamba zitabakia zinauheshimu mkataba huo.

Na cha kushangaza ni kwamba Marekani haijautangaza mkakati wowote wa kutaka kuufanyia marekebisho mkataba wa sasa. Inavyoonesha ni kwamba mkondo wa mambo huenda unaelekea Marekani na Israel kuanzisha vita dhidi ya Iran; bila shaka Israel ikiwa mbele upande wa Marekani ikisaidiwa na Saudi Arabia na nchi nyingine za Ghuba.

Vita hivyo, vitakuwa vikali na Marekani haitapata ureda kama ule wa Iraq. Hisia za kizalendo na za kidini za Wairani zitawafanya wapigane kufa na kupona, na huenda Marekani ikabidi itumie majeshi yake ya nchi kavu- hivyo Iran ikageuka kuwa kaburi kubwa lingine la Wamarekani kama zilivyokuwa Afghanistan na Iraq. Trump anadai kwamba uamuzi wake wa kujitoa kutoka mkataba wa kinyuklia ni kwa maslahi ya Wairani. Lakini ukweli ni kwamba Wairani walifurahi pale mkataba huo ulipotiwa saini mwaka 2015.

Wengi wao walitarajia kwamba mkataba huo utawaletea neema kwa vile nchi yao itaondoshewa vikwazo vya kibiashara.