UCHUMI BINAFSI: Malengo makini yatakupa uhuru wa kipato

Thursday November 9 2017Adam Ngamange

Adam Ngamange 

By Adam Ngamange

Nazungumza na mabilionea. Kama si wa sasa, basi ni wa baadaye.

Inawezekana umeanzisha biashara yako au mradi wowote ila ajabu fedha hazikai. Kila ukipata zinapotea baada ya muda mfupi. Unashauriwa kukopa wakati ukitafuta mtaji na ukipata faida unatakiwa uitumie kujiinua kutoka ulipo.

Kupata hela na kupoteza ni hali ya kawaida. Wengi wanakutana na hali hiyo. Hata mabilionea wakubwa walishawahi kukutana na hali hiyo. Wapo mabilionea waliwahi kufilisika.

Wewe kama walivyo wengine, unaweza kupata fedha na kufilisika. Hapa nawazungumzia wenye  biashara ndogo. Nataka biashara yako ikue. Utoke ulipo na usonge mbele zaidi. Ufanikiwe na siku moja uitwe bilionea.

Ili kufika huko unapaswa kuachana na mchecheto wa mafanikio;  hali ya kutaka kufanikiwa kwa haraka hasa unapojiona umechelewa. Unapofikiri umri wako umeenda na ukijilinganisha na  rafiki zako waliopiga hatua kwa kasi.

Mara nyingi hutokea unakutana na watu wanaokupa hesabu ya biashara yenye faida kubwa ila usiyokuwa na uzoefu nayo. Unaanza kujiona tajiri kabla hujaanza kuifanya.

Kuna sababu mbili zinazowafanya watu wasifanikiwe katika maisha yao. Moja ni kutokutenda licha ya kujua namna ya kufanya kitu fulani jingine ni kufanya kitu bila kuwa na maarifa za kutosha.

Mara nyingi watu wanaopata mchecheto wa mafanikio wanafanya vitu vingi kwa wakati mmoja hivyo kufeli.

Ili kujijua kundi ulilopo  angalia kwa ufupi tangu mwaka uanze umeshajiingiza kufanya mambo mangapi ambayo hayajafanikiwa hata kidogo.

Hakuna anayefanikiwa kwa kutapanya nguvu zake, muda wake na rasilimali chache alizonazo kwenye safari ya ubilionea. Wasiozingatia ubora na uhakika, huwa hawafanyi vizuri maishani.

Ni rahisi kwa matajiri wakubwa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja na wakafanikiwa kwa sababu hawatumii nguvu zao bali mifumo imara waliyonayo.  Wengi tunapoanza tunapaswa kutumia rasilimali zetu kwa uangalifu wa hali ya juu kabla ya kufanikiwa.

Wapo baadhi wakisikia habari za waliofanikiwa huwa na mchecheto usio wa kawaida na kuyatamani. Kuna watu, kwa sababu wamesikia kilimo cha mchaichai au ufugaji sungura unalipa tayari wameshakimbilia huko. Ukifuatilia unakuta hakujiandaa kabisa kimaarifa. Unaweza kumkuta mtu ana mtaji wa shilingi milioni moja ila anafanya biashara tano. Huku ni kupoteza nguvu, muda na pesa.

Siku zote mafanikio ya biashara au kilimo hayatokani na ukubwa wa mtaji wa fedha pekee bali kiwango cha maarifa na uzoefu juu ya unachokifanya. Ili ufanikiwe katika jambo lolote, iwe biashara au kilimo, bila kutumia mtaji mkubwa wa fedha, ni lazima uzingatie mambo haya mawili. Maarifa na uzoefu.

Tafuta kwanza ujuzi au maarifa kuliko unavyotafuta mtaji wa fedha. Watu wengi huwa wanafeli katika wayafanyao kwa sababu hawana ujuzi au maarifa ya kutosha, licha ya mtaji waliowekeza.

Unakuta mstaafu ambaye hajawahi 100 za mafao anaenda kununua daladala na kuisimamia mwenyewe. Ataugua ugonjwa wa moyo kabla hajafeli kwasababu hana ujuzi.

Ujuzi unaotakiwa ni wa kufanya kwa vitendo. Kama unataka kunielewa zaidi, kakusanye maprofesa na madokta wanaofundisha ujasiriamali vyuo vikuu halafu waulize kama kuna biashara yoyote wanayoifanya, utashangaa. Hawafanyi chochote zaidi ya kufundisha.

Ujuzi wa mafanikio unapatikana kwa vitendo. Usilime miti Iringa kwa meseji na kupiga simu, utachekwa. Nenda shambani kawatafute waliotangulia jifunze kutoka kwao kisha weke ratiba ya kwenda mara kwa mara.

Kuna maarifa huwezi kuyapata kwa masomo ya mbali, unatakiwa uwepo eneo la tukio kwa wakati husika. Jambo la pili, ni jinsi ya kufanya maamuzi. Maamuzi ni zao la uchaguzi unaotokana na taarifa uliyonayo. Basi jitahidi sana kupata na kukusanya taarifa za ndani na za uhakika.

Tofauti tuliyonayo ni taarifa. Mara nyingi taarifa za mafanikio huwa zinatiwa chumvi nyingi ili uone kuwa ni rahisi kuyafikia. Wengi watakuonyesha urahisi wa biashara na mafanikio makubwa bila kukuonyesha changamoto. Wapo waliokata tamaa kwa sababu hawakujiandaa kukabiliana na changamoto walizokutana nazo baada ya kutamanishwa.

Kama hutaki kukata tamaa kutokana na changamoto utakazokutana nazo basi fahamu mapema kuwa kila fursa kubwa unayopewa na kuambiwa inachangamoto zake. Kumbuka, hakuna fursa isiyo na changamoto na kadri inavyoonekana kubwa ndivyo changamoto zake zilivyo pia. Jipange kuzitatua. Ukiambiwa twende vitani utakuwa mfalme, ujue kuna Goliath wa kumkabili.

Unaweza kutimiza ndoto zako kwa kuanza bila mtaji ila kabla  hujaamua kupiga hatua jiulize; haya maamuzi ni thabiti au mchecheto wa mafanikio. Na kama unataka kuepuka kufeli punguza mchecheto.

0656 143 785
[email protected]

Advertisement