Malengo ya elimu yaoanishwe na mahitaji ya vijana kujiajiri

Muktasari:

Matamko haya ambayo mengi ni ya kisiasa, yanachochewa na tatizo kubwa la ajira linaloikabili nchi yetu.

       Katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, kundi kubwa la vijana waliohitimu vyuo linaingia rasmi kwenye soko la ajira. Wanasiasa na wadau mbalimbali wa maendeleo hutumia kipindi hiki cha mahafali kuwaasa vijana ‘kufikiri nje ya boksi’ kwa maana ya kutafuta namna wanavyoweza kujiajiri.

Matamko haya ambayo mengi ni ya kisiasa, yanachochewa na tatizo kubwa la ajira linaloikabili nchi yetu.

Inakadiriwa kwa mfano, kila mwaka takribani watu wapya 1,000,000 huingia kwenye soko la ajira wakitafuta ajira.

Katika mazingira ambayo soko hili haliwezi kutengeneza nafasi za kazi kwa watu 100,000 kwa mwaka, ni wazi kwamba watunga sera na wafanya uamuzi wanalazimika kuwaasa vijana ‘kuacha kutegemea Serikali iwapatie ajira.’

Elimu inayowaandaa kuajiriwa

Pamoja na ushauri mzuri kwa vijana kujiajiri, ni vizuri tukijiuliza kama kweli tumewapa vijana elimu itakayowawezesha kujiajiri.

Chukulia kijana aliyesoma sayansi ya siasa. Tunapomshauri ajiajiri, tunakuwa na maana gani? Tunataka afungue biashara gani hasa inayoweza kuendeshwa kwa kutumia elimu yake aliyopata darasani?

Huo ni mfano mmoja. Tunafahamu, kwa mfano, program nyingi zinazotolewa kwenye vyuo vyetu haziwapi vijana mwangaza wa kujiajiri. Programu hizi, wakati mwingine huandikwa kwa lengo tu la kujaza orodha ya shahada zinazotolewa vyuoni, lakini hakuna utafiti wa kina unaofanyika kujua mahitaji halisi ya jamii.

Vijana huchagua kusoma programu hizo wakiwa na matarajio makubwa lakini kimsingi, hawajui watafanya nini na hicho wanachokijua nje ya darasa.

Tunapowaasa vijana watumie elimu yao kujiajiri, ni sawa na kuwadhihaki. Wapo vijana wenye uthubutu wanaoamua kuzitelekeza fani zao ili kufanya ujasiriamali na uchuuzi bila kutegemea ajira. Lakini hata wanapofanya hivyo, bado mazingira ya kazi huwakatisha tamaa tangu hatua za mwanzo.

Mlolongo wa tozo na kodi zisizozingatia mtaji mdogo ambao wakati mwingine analazimika kuazima kwa ndugu, jamaa na marafiki ni moja wapo ya orodha ndefu ya vikwazo anavyokabiliana navyo kijana mjasiriamali. Kwa maana hiyo, pamoja na nia njema ya kuwataka vijana wajiajiri ni vyema tukajiuliza ni kwa kiasi gani tumewaandalia mazingira ya kuitikia wito huo muhimu.

Elimu bora ni mtaji

Namna moja wapo ya kuwawezesha vijana kujiajiri ni kuwapa elimu inayokidhi matakwa ya wakati ulipo. Kijana aliyepatiwa elimu bora anaweza kuitumia kama mtaji utakaomwezesha kujiajiri.

Lakini je, elimu tunayompa kijana inamwandaa kujiajiri kama tunavyomshauri? Je, kijana aliyemaliza shahada ya kwanza anaweza kutumia maarifa aliyoyapata darasani kuendesha shughuli zake bila ajira?

Pamoja na ukweli kwamba dhima kuu ya elimu ni kupanua uelewa wa jumla wa kijana, pengine kuna haja ya kuifanya elimu yetu imsaidie kijana kujenga uwezo wa kuona matatizo yanayoikabili jamii na kuyatafutia ufumbuzi.

Ikiwa ndivyo hivyo, elimu inaweza kutumika kama mtaji.

Hivi sasa mwelekeo wa jumla wa elimu nchini ni ya kuchuja wanafunzi ili kupata wataalamu wachache watakaofikia ngazi ya juu zaidi ya elimu. Tunafikiri tija ya elimu inapatikana kwa kufika chuo kikuu. Mtazamo huo kwa bahati mbaya hauwezi kutatua tatizo kwa sababu kuu mbili.

Kwanza, wanafunzi wengi wanachujwa katika ngazi za chini na kuachwa bila ujuzi wowote wa maana.

Watu hawa ambao ndiyo wengi, wanalazimika kutafuta namna nyingine ya kuishi bila kutumia kile walichojifunza darasani.

Kadhalika, wale wachache wanaoendelea na elimu ya juu, wanajengewa mtazamo kwamba wao ni kundi maalumu katika jamii linalostahili ajira yenye hadhi.

Lakini bahati mbaya wengi wao humaliza shahada ama wakiwa na ujuzi nusu au hukosa kabisa ujuzi huo unaowezesha kufanya shughuli bila kuajiriwa lakini matokeo yake nao kama wale waliochujwa katika ngazi za chini, wanalazimika kutafuta nafasi za kazi kwa sababu msamiati wa kujiajiri hautekelezeki.

Elimu ya kujitegemea

Tunahitaji kubadili mwelekeo wa elimu yetu kutoka kumwandaa kijana kufanya kazi za mwajiri mpaka kujiajiri. Tangu mwanafunzi anapoanza masomo, aandaliwe kutumia hicho anachojifunza kama njia ya kujiongezea kipato hata pale anapojikuta nje ya mfumo wa ajira.

Mwalimu na mwanafunzi kwa pamoja wafanye kazi ya kutafsiri maudhui ya mitalaa yetu ili ngazi yoyote ya elimu imsaidie mwanafunzi kuona fursa katika mazingira yake bila kulazimika kupatiwa mafunzo mengine ya ziada.

Kijana anayejengewa uwezo wa kuona na kutatua changamoto, mkononi mwake anakuwa amekabidhiwa ufunguo unaobeba thamani yake. Kwa kuutumia ufunguo huo, kijana huyu hawezi kukosa kazi ya kufanya akirudi kwenye jamii.

Ili hilo liwezekane, mamlaka za elimu zinawajibika kufanya utafiti utakaowezesha kutengeneza programu zinazojibu matatizo halisi yanayoikabili jamii.

Ni kweli kwamba mahitaji ya jamii yana tabia ya kubadilika. Kinachoonekana muhimu leo, si lazima kiwe muhimu kesho. Maana yake ni kwamba, mwanafunzi hapaswi kutegemea kupata maarifa yaliyo tayari kwa matumizi.

Kazi ya kuyafanya maarifa hayo yatumike kutatua changamoto za kila siku zinazoikabili jamii inabaki kuwa ya mwanafunzi mwenyewe. Ni wajibu basi wa mwanafunzi mwenyewe kuhakikisha anajua kwa hakika kile anachokitaka ili aweze kuchagua eneo la kitaaluma linalokidhi wito alionao ndani yake.

Aidha, ipo haja ya kufanya jitihada za makusudi kuoanisha mazingira halisi ya kazi na ujuzi unaotolewa darasani. Ufundishaji ulenge kuwafanya wanafunzi waione jamii yao wakiwa darasani badala ya kuwafundisha mambo ya kufikirika wasiyoyaona katika maisha yao ya kila siku.

Sambamba na hilo, tutafakari sababu iliyotufanya tupanue elimu ya juu na kupunguza uzito wa vyuo vya kati na vyuo vya ufundi. Kasumba kwamba kufika chuo kikuu ndiyo kipimo cha kuelimika, inachangia kukuza tatizo la ukosefu wa ajira.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754870815