Malezi ya vifaranga wanaokua

Muktasari:

Mfugaji anaweza kuweka wasimamizi wa kumsaidia anapokuwa katika majukumu mengine, lakini ahakikishe anatembelea na kukagua mara zote kwani atagundua mambo mengi yatakayomuongezea akili ya kuboresha biashara yake na kumletea faida kubwa.

Katika biashara hakuna mchawi zaidi ya huduma nzuri na usimamizi wa kutosha.

Shamba lolote au mradi wowote usipohakikishwa kwenye kipengele cha usimamizi, mambo mengine hayana nguvu kuleta faida kwenye mradi huo.

Mfugaji anaweza kuweka wasimamizi wa kumsaidia anapokuwa katika majukumu mengine, lakini ahakikishe anatembelea na kukagua mara zote kwani atagundua mambo mengi yatakayomuongezea akili ya kuboresha biashara yake na kumletea faida kubwa.

Makala hizi za ufugaji wa kuku hutoka kila mara na kuelimisha eneo fulani kwenye ufugaji, ni vizuri kwa mtu mwenye uthubutu kufanyia kazi kila kipengele kinachoongelewa.

‘Haba na haba hujaza kibaba’, usiache jambo la ufugaji linalozungumziwa hapa likupite kama unayo nia ya kufanya vizuri au kujiajiri kupitia ufugaji hasa ufugaji wa kuku.

Kimsingi, kila jambo linahitaji kuandaliwa vizuri ili kuleta matokeo mazuri. Kuandaa na kulea vizuri vifaranga wa kuku ni kuandaa mavuno mazuri ya mayai au nyama ya kuku baadaye. Waswahili husema ‘ ukitaka kuzitumia zichange kwanza, lakini mimi nasema ukitaka kufanikiwa kwenye biashara yako jipange kufanana na biashara yako kwanza.

Mtu anayetaka kuwa na ng’ombe wengi kesho anatakiwa kuwa na ndama wengi leo, sawa sawa na mtu anayetaka kuwa na mradi mkubwa wa kuku kesho anatakiwa kuwa na vifaranga wenye malezi bora leo.

Kila kitu ni kushawishika, usiposhawishika na malezi kwenye mradi wako hutashawishika na hatua ya uzalishaji mwishowe ni kusema haijakulipa Tuangalie mwendelezo wa malezi ya vifaranga wenye umri wa wiki nane na kuendelea baada ya kutazama malezi ya vifaranga wenye umri wa wiki sifuri hadi saba katika makala yaliyopita.

Tuliona namna gani vifaranga wanahitaji chanjo za mara kwa mara kipindi wangali wadogo, joto na chakula chao kuwa na ubora kuwapa kinga dhidi ya magonjwa na kukua kwa haraka.

Katika umri wa wiki nane au zaidi vifaranga hufikia hatua ya pili katika malezi na kuhitaji kubadilishiwa huduma za chakula, joto na tiba.

Katika umri huu vifaranga huitwa (growers) badala ya (chicks) walipokuwa na umri wa chini ya wiki nane.

Hapa mambo mengi hubadilika na vifaranga kuwa wamechangamka sana na kuonyesha tabia nyingi mbalimbali ambazo hapo awali hawakuonekana kuwa nazo.

Kwanza hutambuana kwa harufu na rangi ya manyoya kwa kila kifaranga aliyemo kwenye banda. Kila kifaranga hutambua kuwa ana uwezo hivyo huanza kutafuta utawala dhidi ya wengine na fujo nyingi hujitokeza mara kwa mara wakipigana bandani.

Hali hii husababisha vifaranga wadogo kupigwa na kunyanyaswa hasa wakati wa kula chakula.

Katika umri huu mfugaji awe makini tangu wiki ya kwanza ahakikishe kuna vifaa vingi vya kutosha vifaranga wote wapate chakula kwa pamoja na kukua wakiwa wote wana miili yenye ukubwa sawa ili hapo baadaye mapigano yakianza watatoshana nguvu na kuamua kuwa wapole na kuacha kudonoana au fujo zozote za wao kwa wao bandani hukoma.

Pili, nafasi bandani iwe ya kutosha wasibanane tangu wakiwa wachanga. Hali hii huwapa nafasi ya kustarehe na kukimbizana au kufanya michezo inayawajengea urafiki usioleta ghadhabu ya kudonoana kwa nia ya kutafuta uhuru wa nafasi.

Tatu, usichanganye vifaranga wenye rika tofauti waliopishana kwa zaidi ya umri wa wiki moja.

Kuwachanganya vifaranga wenye rika tofauti ni kusababisha vifaranga wadogo kupigwa muda wote bandani na kushindwa kukua vizuri au kufa kutokana na majeraha ya kudonolewa au kutoshiba.

Usichanganye vifaranga wenye rangi tofauti labda itokee vifaranga hao wamechanganyika tangu awali wakiwa hawajapata akili ya kubaguana.

Endapo umepanga kuchanganya vifaranga waliolelewa tofauti wachanganye usiku wakiwa hawana uwezo wa kupigana ili kufikia kesho watakuwa wameambukizana harufu na kuwa sio rahisi kutambuana na kupigana.

Pia hakikisha banda lako sio kubwa sana kiasi cha kuruhusu vifaranga wageni kujitenga sehemu yao na wenyeji sehemu yao kwani mapigano yataendelea.

Katika umri huu vifaranga hujifunza kila kitu ambacho hushindwa kusahau hadi wanafikia umri wa kutaga kama ni kuku wa mayai.

Tabia ambazo husababisha hasara kwa mfugaji hukomeshwa kwa namna mbali mbali ikiwamo kukatwa midomo ili kukomesha kudonoana na kuuana.

Ukataji wa midomo ufanyike kwa kuzingatia kanuni za afya kwa vifaranga, kwani vifaranga wanaweza kuvuja damu nyingi na kufa endapo mkataji atatumia mkasi, kisu au wembe.

Tumia kitu cha moto kukata na kuunguza mdomo dawa isivuje. Ikumbukwe kila tabia inayojitokeza kwa vifaranga husababishwa na kitu fulani ambacho mfugaji hakukigundua mapema.

Vifaranga wakibanana au kupungukiwa na lishe kwenye chakula husababisha kudonoana.

Mfugaji afuatilie kila hatua kwa kutoa huduma zinazotakiwa kulingana na umri wa kuku wake.

Mbali na huduma hizi kwa vifaranya wenye umri huu, chakula chao hubadilika kutoka chakula cha kuanzia (chickmash) na kupewa chakula cha kukuzia (growers mash).

Chanjo za mara kwa mara huachwa na kufuata kalenda ya chanjo ya kideri (Newcastle disease vaccine) ya kuku wakubwa ambayo hutolewa kila baada ya miezi miwili hadi mitatu.

Pia, katika umri huu vifaranga huanza kupimiwa chakula wanachokula kila siku kwa kipimo ambacho huongezwa kila wiki kulingana na umri unavyo kwenda na mahitaji ya mwili, ili wasinenepe na kujaa mafuta na kushindwa kutaga hapo baadaye.