Thursday, January 12, 2017

Mambo matano yaliyoshangaza na kushtusha uchaguzi wa Gambia 2016

Wananchi wa Gambia wakishangilia ushindi wa

Wananchi wa Gambia wakishangilia ushindi wa kiongozi wa upinzani nchini humo, Adama Barrow Desemba mwaka jana baada ya kumshinda Rais Yahya Jammeh aliyeongoza kwa zaidi ya miaka 20. Picha na AFP 

By Deus M Kibamba,Mwananchi

Mwishoni mwa mwaka jana 2016, kulifanyika uchaguzi katika nchi ndogo ya Afrika Magharibi ya Gambia, uchaguzi ambao kwa yake unafanana na sifa za uchaguzi barani Afrika.

Katika uchaguzi huo, Rais anayemaliza muda wake kisheria, Alhaji Yahya Jammeh alichuana vikali na mshindani wake wa muungano wa vyama vya upinzani, Adama Barrow ambaye ni mfanyabiashara maarufu jijini Banjul hususan katika sekta ya udalali wa nyumba na viwanja.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo, Barrow amekuwa Rais Mteule baada ya kumshinda Rais aliyeko madarakani, Yahya Jammeh kwa kupata asilimia 45.5 ya kura zote zilizopigwa dhidi ya asilimia 35 aliyoipata Rais anayeondoka.

Hata hivyo, nini hasa kinafanya uchaguzi wa Gambia kufanana zaidi na uchaguzi wa Afrika?

Kwa kuutazama uchaguzi wa Gambia wa Desemba Mosi, 2016, kuna mambo matano yaliyoleta mshtuko wakati na baada ya uchaguzi huo.

Kwanza, ilishangaza kwamba nchi hiyo yenye takriban watu milioni mbili ilipata hamasa kubwa ya ajabu katika uchaguzi huu. Ikumbukwe kuwa Rais Jammeh alichukua nchi kwa mapinduzi yaliyofanyika mwaka 1994.

Kama kawaida ya Waafrika wengi, ilimchukua miaka miwili kabla ya kuanza kujisimika rasmi Ikulu kama Rais wa Gambia.

Kama alivyofanya Rais Jammeh, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alichukua nchi kwa njia ya kijeshi akitokea mwituni mwaka 1986 na taratibu alianza kujisimika na kujihalalisha kupitia uchaguzi kila baada ya miaka mitano.

Kwa namna hiyo hiyo, Rais Joseph Kabila wa DRC Congo aliingia Ikulu ya Kinshasa kwa mtindo kama huo mwaka 2001 kabla ya kuanza kujisimika rasmi kwa mujibu wa Katiba ya DR Congo ya mwaka 2006.

Jambo la kwanza lililoshangaza na kushtusha ni kuhusu mfumo wa uchaguzi. Ikifuata mfumo wa mwenye wingi wa kura ameshinda (maarufu kama first- past the Post), Gambia imekuwa ikishuhudia ushindi wa Rais Jammeh tangu mwaka 1996 hadi sasa.

Kwa uhakika kuwa angeshinda kila uchaguzi mpaka Mungu atakapomchukua, Rais Jammeh aliwahi kutamba kwa kusema kuwa yeye ‘ni Rais wa miaka bilioni moja kwa rehema za Allah’.

Hii iliwashangaza na kuwashtua wengi waliochukulia maneno ya Rais kuashiria nia yake ovu ya kukaa madarakani milele.

Hata hivyo, binafsi nilichukulia kuwa maneno yake yaliashiria uhakika aliokuwa nao kushinda uchaguzi wowote utakaokuja kwa kutumia mfumo wa uchaguzi ambao ni mwasisi wake na kwa hivyo anaufahamu vyema.

Kwa taarifa, Rais Jammeh ni Rais wa pili tu tangu nchi hiyo ipate uhuru wake mwaka 1965. Imenishangaza kwamba mfumo ule ule wa uchaguzi aliojivunia Rais Jammeh ndiyo uliomdondosha kwenye uchaguzi huo.

Laiti Jammeh angepata fursa nyingine ya kushiriki uchaguzi nchini Gambia, nina uhakika angepigania kuwa mfumo wa uchaguzi nchini mwake ubadilishwe ili mshindi wa kiti cha urais alazimike kupata angalau asilimia 51 ya kura zote zilizopigwa ili ndiyo atangazwe kuwa mshindi.

Nje ya hapo, mfumo huo unataka kuwe na duru ya pili ya upigaji kura ambayo ingemsaidia Rais Jammeh katika madai yake ya kutaka uchaguzi urudiwe.

Sambamba na mfumo wa uchaguzi, ilishangaza watu wengi kwamba ipo nchi duniani na barani Afrika ambayo bado inatumia goroli katika upigaji wa Kura.

Matumizi ya goroli

Nilizungumza na watu kadhaa kuhusu matumizi ya goroli katika upigaji kura nchini Gambia na waliuliza maswali mengi juu ya sababu zake.

Kwa maoni yangu, matumizi ya goroli yamechochewa na sababu mbili. Kwanza, idadi kubwa ya Wananchi wa Gambia kutokujua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (yaani KKK).

Hiyo inafanya uwezekano wa kuandaa karatasi za upigaji kura kuwa na ugumu kwa wengi kwani hawataweza kuzitumia.

Pili, hali ngumu ya kiuchumi nchini Gambia imechangia katika kukosa bajeti ya kuchapisha vitabu vya karatasi za kisasa za kupigia kura kama zile zinazotumika kwingineko Afrika.

Ilinishangaza kwamba wabunifu na wataalamu wa mifumo ya kimtandao walishindwa kutumia fursa ya changamoto za elimu nchini Gambia kuingiza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Teknohama) katika uchaguzi huo. Hivi kweli kusoma hawawezi, lakini Wagambia wangeshindwa hata kusoma picha? Imenishangaza na kunishtua.

Pia, imenipa mshtuko wa furaha kubaini kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Gambia, Alieu Mauarr Njai amesimamia sheria kikamilifu kiasi cha kumtangaza mgombea wa muungano wa upinzani kuwa mshindi.

Aidha, mshtuko mwingine ni ule uliompata Njai pale alipopigiwa simu na Rais Jammeh akimjulisha kuwa ameshindwa uchaguzi na kwamba tayari amempigia kumpongeza Barrow kwa ushindi wake wa kishindo.

Kilichomshangaza Njai ni kwamba, wakati akipokea simu, alikuwa hajakamilisha hata kazi ya kuhesabu goroli na kujumlisha matokeo kumjua aliyeshinda uchaguzi.

Sasa swali ambalo Njai hakujiuliza lilikuwa ni; je, Rais amepata wapi taarifa za kushindwa kwake? Kilichomshtua Mwenyekiti na Tume yake ilikuwa ni mambo mawili.

Kwanza, uharaka wa Rais Jammeh kukubali kushindwa. Pili, ni kwa nini hakugusia lolote kuhusu kuitaka Tume ifanye lolote jambo matokeo yageuke ili yeye ndiye awe mshindi?

Katika nchi ya Kenya, hali kama hii iliwahi kujitokeza baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Samuel Kivuitu alishangaa kupokea mwaliko wa kwenda kushiriki hafla ya kumwapisha Rais wakati tume ikiwa bado kukamilisha hata kazi ya kuhesabu kura na kujumlisha matokeo.

Kwa maneno yake mwenyewe, Kivuitu aliwahi kusema hata baada ya kuapishwa Rais kuwa hajui mshindi wa uchaguzi ule alikuwa nani na kuongeza: “Kama suala hili litakwenda kortini na liende kwa haraka ili kama itabainika ni Raila Odinga ndiye mshindi basi na iwe hivyo”. Hiyo ndiyo Afrika.

Vinginevyo, imenishangaza na kunishtua jinsi Serikali ilivyoamua kuzima huduma za mtandao na mawasiliano wakati wote wa uchaguzi kwa sababu walizoziita za ‘kiusalama’.

Hivi kuna sababu gani za kiusalama ambazo zinaweza kufanya kuzimwa kwa mawasiliano wakati wa uchaguzi ndiyo iwe tiba?

Katika hili, Jamhuri ya Gambia imefanana na nchi za Afrika kama Uganda, Zimbabwe na Burundi ambako Serikali imekuwa na visingizio kadha wa kadha kabla na mara baada ya uchaguzi katika kuhalalisha uingiliaji wa mawasiliano ya kimtandao na simu kwa kuyakata.

Kwa mshangao, uzuiaji wa mawasiliano ndani ya Gambia umeshindwa kumsaidia Rais Jammeh ‘kushinda’ tena uchaguzi.

Katika hali ya kushangaza, mawasiliano yote yalirejeshwa nchini Gambia na kuifanya nchi hiyo kuwasiliana tena na dunia. Kilichonishtua na kuendelea kunishangaza ni kuhusu gharama za mitambo ya kudhibiti mawasiliano wakati wa uchaguzi zinatoka wapi katika nchi yenye uchumi duni kama Gambia?

Hitimisho

Mwisho, nikiri wazi kuwa nimeshangazwa na utegemezi mkubwa uliopo katika nchi ya Gambia kiasi cha kushindwa kujitegemea kwa nyanja takriban zote za kimaisha.

Kwa mfano, wakati Rais Jammeh akijaribu kufungua shauri katika Mahakama ya Katiba nchini Gambia, taarifa zilizopo ni kwamba kesi hiyo ambayo inapaswa kutajwa kwa mara ya kwanza wiki hii imekumbwa na changamoto ya kutokuwepo jopo la majaji katika mahakama hiyo ya juu kabisa nchini humo.

Hayo yametokea baada ya kufutwa kazi kwa majaji wawili mwaka jana ambao pamoja na Jaji Mkuu wangetimiza idadi ya majaji watatu wanaoweza kusikiliza shauri kama hilo.

Pia, imenishangaza kuwa mpaka mwaka 2017, bado ipo nchi duniani inayopewa msaada wa Jaji Mkuu kutoka nchi nyingine.

Nchini Gambia, kumekuwa na Jaji Mkuu wa msaada kutoka nchi nyingine kwa miaka takriban 10 sasa ikiwamo Jaji Mkuu wa sasa, Emmanuel Fagbenle, ambaye ni raia wa Nigeria.

Kabla yake, kulikuwapo na Jaji Mkuu, Ali Nawaz Chowhan, raia wa Pakistan ambaye alichukua nafasi hiyo kutoka kwa raia wa Ghana, Mabel Agyemang.

Sambamba na majaji, hata Mkurugenzi wa Mashtaka Gambia kwa sasa ni raia wa Nigeria. Ni ajabu na kweli!

Deus Kibamba ni mtafiti, mhadhiri na mchambuzi wa masuala ya siasa za kimataifa na demokrasia ya Katiba. Anapatikana kwa: Simu +255 788 758 581 au email: dkibamba1@gmail.com

-->