Mambo muhimu uteuzi, utenguzi wa wabunge

Aliyekuwa mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango akichangia hoja bungeni mjini Dodoma mwaka 2014. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Kwa kuzingatia kuwa nilifanya uchambuzi uliorushwa kupitia vituo vingi vya redio na hasa runinga, kwa kuzingatia kuwa teknolojia ya ving’amuzi imepunguza idadi ya Watanzania wanaomudu kutazama kituo hiki au kile cha televisheni kutegemeana na aina ya king’amuzi anachokimiliki.

Katika kipindi cha wiki moja, nimeombwa kufanya uchambuzi wa mambo makuu yaliyojiri kufuatia uteuzi na kumteua mbunge kwa nafasi ya ubalozi nje ya nchi alioufanya Rais John Magufuli kwa nafasi zake 10 za wabunge kikatiba.

Kwa kuzingatia kuwa nilifanya uchambuzi uliorushwa kupitia vituo vingi vya redio na hasa runinga, kwa kuzingatia kuwa teknolojia ya ving’amuzi imepunguza idadi ya Watanzania wanaomudu kutazama kituo hiki au kile cha televisheni kutegemeana na aina ya king’amuzi anachokimiliki.

Nimeona nitoe japo kwa ufupi hoja kuu nilizozitoa kuhusiana na sakata la uteuzi wa wabunge wanaofikia watatu katika muda wa wiki moja iliyopita. Msimamo wangu ni kuwa uteuzi huo wa wabunge ulikaribia kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika maeneo mawili.

Kwanza, uteuzi wa wabunge wanaume wawili yaani Profesa Palamagamba Kabudi na Abdallah Bulembo ulinishtua. Ingawa nilifurahia kuwa Profesa Kabudi, gwiji wa sheria nchini akijulikana hapa nchini kama mhadhiri mahiri wa sheria na mchambuzi aliyesheheni historia ya Katiba na ukatiba nchini na duniani, nilianza kubashiri kinachotaka kutendeka juu yake.

Kama wengi walivyoibuka na kueleza hisia zao, nilipata picha na bado picha hiyo ipo kichwani mwangu kuwa mabadiliko katika baraza la mawaziri Tanzania yako mbioni. Katika mabadiliko hayo, Profesa Kabudi atapewa nafasi muhimu inayohusiana na taaluma yake ya sheria na masuala ya Katiba.

Aidha, nilielewa uteuzi wa Bulembo, mwanasiasa ambaye ndiye alimvusha Rais Magufuli katika safari ya urais akiwa meneja wake wa kampeni.

Kwa mambo yalivyokwenda, uteuzi wa wabunge hao haukuwa habari kubwa. Kilichofanya habari hiyo kugonga vichwa vya habari katika magazeti, runinga, redio pamoja na mitandao ya kijamii ilikuwa ni tafsiri kuwa uteuzi huo ulikuwa umevunja ibara ya 66 (1) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, kama ilivyorekebishwa hadi mwaka 2005.

Hili lilinijia akilini baada ya kutangazwa kwa majina ya wanaume wawili kuteuliwa katika nafasi hizo ambazo mojawapo haikuwa yao (wanaume) kikatiba.

Kwa utamaduni wa wachambuzi, niliamua kuacha kuhamaki na kujikita katika kupitia na kuchambua vifungu vinavyohusu uvunjifu huo wa Katiba, vile vinavyotoa mwelekeo wa nini kinaweza kufanyika na nikaanza kushauri juu ya nini cha kufanya.

Kwa kusema ukweli, nilijaribu kushauriana na watu mbalimbali kuhusu namna ya kutatua utata na sintofahamu iliyokuwa imeletwa na uteuzi huo. Kwa hakika nilithibitisha jambo moja kuwa endapo hali ingeachwa hadi wabunge wateule wawili Profesa Kabudi na Bulembo wakala kiapo bungeni na kuwa wabunge wa Tanzania, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ingekuwa kwenye utata. Kwa sababu hiyo, ushauri wangu ulijikita katika kupendekeza hatua za haraka na zile za muda mrefu. Katika mambo ya muda mfupi na haraka niliyopendekeza, kulikuwapo suala la Rais ambaye kwa mamlaka aliyonayo ya uteuzi, ana mamlaka ya utenguzi wa mbunge ambaye hajaapishwa na Bunge la Tanzania na kuwa mbunge, angeweza kutengua uteuzi wa mmojawapo kati ya Bulembo au Profesa Kabudi kwa mtiririko huo.

Yalifanyika makosa?

Nashukuru kuwa dhana ya utenguzi ilifikiriwa ingawa ikafanyika isivyo. Kwa bahati mbaya, tulitaarifiwa juu ya kuteuliwa kwa Dk Abdallah Possi kuwa balozi, kitendo ambacho kikatiba au kisheria hakimwondolei ubunge wake.

Nafahamu kuwa kwa uzito wa wateule takribani wote wa Rais bungeni, Ikulu iliingia katika ugumu mkubwa juu ya nani ambaye uteuzi wake ungeweza kubatilishwa pasipo mtikisiko wa kisiasa. Kwa bahati mbaya, chaguo la Dk Possi lilikuwa si sahihi kisiasa na kijamii.

Kwanza, Dk Possi ni msomi nadra katika jamii ya watu wenye ulemavu wa ngozi na ulemavu kwa ujumla ambaye amekwishakonga mioyo ya Watanzania wengi kutokana na ujenzi wa hoja za makundi maalumu na za wanyonge kwa ujumla.

Pili, Dk Possi ambaye ni mwanasiasa chipukizi akitokea katika taaluma ya sheria angefaa aachwe katika nafasi hiyo kwa miaka yote mitano ili ajengeke vya kutosha kuweza kumfanya agombee na kuchagulika mwaka 2020.

Kumteua kuwa balozi ambaye anaweza kupangiwa kituo cha kazi DRC Congo au Gambia au kwingine kokote duniani lilikuwa ni kosa la kisiasa kwa upande wa wanaomtakia mema Dk Possi.

Sintofahamu nyingine iliyoibuka katika hili ilikuwa ni hisia kuwa kwa uteuzi huo wa Dk Possi kama balozi, Rais alikuwa ‘ametengua’ ubunge wa Possi. Ingawa jambo hili lilifanywa kwa nia hiyo, ili kuua sintofahamu ya uteuzi wa wabunge wanaume wanafikia sita na hivyo kuzidi watano wanaoruhusiwa na ibara ya 66 (1) (e), ilikuwa ni bahati mbaya kuwa ilichelewa kufahamika kuwa Rais hana mamlaka ya utenguzi kwa mbunge aliyekwishaapishwa na kuwa mbunge wa Tanzania.

Namna ya kumwondoa mbunge hata kama ni wa kundi la kuteuliwa na Rais kama Dk Possi ni kupitia sababu zinazotolewa katika ibara ya 71(1) ya Katiba ya Tanzania pekee.

Kwa mujibu wa ibara hiyo, mbunge anaweza kupoteza ubunge kwa sababu ya kujiuzuru mwenyewe, kupoteza sifa kwa njia ya kubainika kuwa alipochaguliwa hakuwa na sifa za kuchaguliwa kuwa mbunge au kwa kufariki dunia.

Aidha, Mahakama inaweza kumuondolea mtu ubunge endapo kesi iliyofunguliwa mahakamani itampa ushindi mtu tofauti na yeye. Aidha, mbunge anaweza kupoteza ubunge wake kwa kutohudhuria mikutano mitatu mfululizo pasipo sababu inayojulikana na kukubalika kwa spika. Vinginevyo, mbunge anaweza kupoteza ubunge kutokana na chama cha siasa kilichomdhamini kumpoka kadi kama ishara ya kumfuta uanachama.

Nje ya sababu hizi, hakuna mamlaka yoyote yenye uwezo wa kumfuta ubunge mtu yeyote aliyechaguliwa au kuteuliwa kuingia bungeni, isipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye anaingia bungeni kwa nafasi yake kama Mwanasheria Mkuu na hivyo kubadilishwa kwake na Rais kutamaanisha kuwa atakoma kuwa mbunge.

Ingawa ilinishangaza kuwa haikugundulika mapema kuwa Dk Possi anapaswa kujiuzulu mwenyewe kwa barua anayomwandikia Spika wa Bunge, hatimaye hilo limefanyika.

Kwa habari zilizopo ni kwamba Spika amekwishakubali kujiuzulu kwa Dk Possi ili kuruhusu kupatikana kwa nafasi ya uteuzi wa mbunge mpya kama ilivyo katika matakwa ya ibara ya 66. Yaliyobaki si historia tu, bali kuna mafunzo muhimu.

Anne Kilango

Kwanza, kunahitajika umakini zaidi katika uteuzi na utenguzi wa viongozi wa kisiasa na wale wa umma nchini. Tazama sasa, baada ya sakata hilo lote, Anne Kilango Malecela ndiye aliyeokoa jahazi la uteuzi mpya.

Deus Kibamba ni mtafiti, mhadhiri na mchambuzi aliyebobea katika masuala ya uhusiano wa kimataifa, katiba na demokrasia ya uchaguzi. Mawasiliano: +255 788 758 581; email: [email protected]