JICHO LA MWALIMU: Mambo saba ya kufanya unapokaa na watoto

Malezi bora ndiyo msingi wa kumpata kijana atakayetimiza malengo yake.

Msingi mkuu wa malezi na makuzi ya mtoto, unaanzia kwa wazazi kisha wanafuatia  wadau wengine kama jamii inayowazunguka na mifumo mbalimbali ya elimu rasmi.

Wazazi wasiokuwa tayari kulea watoto wao, ni vema wakaahirisha kuzaa mpaka hapo watakapokuwa tayari.

Hii ni kwa sababu wajibu huu wa malezi wanaopewa na taifa lolote ni mkubwa kuliko hata ujira wanaoutafuta.

Inasikitisha mno kuona katika jamii zetu kluna watoto wengi ambao pamoja na kuwa na wazazi tena wote wawili, watoto hao hawana mwelekeo wowote wa kimaisha.

Hawa wanatokana na wazazi wasiotambua wajibu wao. Wazazi wenye mtazamo wa kujua kuzaa pekee, lakini sio kulea. Mzigo wa malezi unaachiwa kwa jamii na ulimwengu, mwishowe tunakuwa na watu  wenmye tabia za ovyo katika jamii.

Zamani, familia nyingi zilijengwa na zikawa imara kwa sababu ya mfumo wa malezi imara ambapo mama (mama wa nyumbani), alikuwa na jukumu la kulea. Baba alihakikisha mahitaji muhimu ya familia yanatimizwa.

Katika kipindi hicho, iliwezekana mama kuacha kazi kwa utashi wake na kuwekeza katika kulea familia.

Mambo saba ya mzazi au mlezi kufanya anapopata wasaa wa kuketi na mtoto au watoto ni ushauri ili kuvunja ule ukuta wa baadhi ya wazazi na walezi kukosa cha kutenda pale wanapopata muda wa kuketi pamoja na watoto wao.

Moja, kusimulia hadithi au ngano, zenye kujenga kwa kusoma katika vitabu. Kwa kupitia hadithi watoto wanajengwa katika stadi za lugha, umahiri wa kufikiri na maadili mema.

Pia, hujifunnza neno la Mungu, ushairi, ngonjera, vichekesho, kuimba na kutumia ala za muziki.

Kipindi cha zamani hili lilisaidiwa sana na bibi na babu au shangazi na mjomba ama ndugu wengine waliotembelea familia husika.

Lakini kwa sasa mambo yamebadilika pengine ni kutokuwapo kwa watu hao kwa sababu za kiuchumi, kutojali umuhimu wa wazee au uchoyo tu wa watu wa sasa wasiotaka kuwa na familia kubwa nyumbani.

Familia kubwa hasa zinazojumuisha watu wenye umri mkubwa kama vile babu, bibi, wajomba, zina faida ya kuwa na watu  wanaoweza kukaa na watoto kwa minajili ya kuwapa miongozo mbalimbali ya maisha ambayo wazazi wasingeweza kuwapa kwa sababu ya kutingwa na shughuli za kimaisha.

Mbili, kuwatia moyo watoto na vijana badala ya kuwalaumu na kuwakatisha tamaa, hasa pale wanapoona hawajafanya vizuri kimasomo, kimichezo, kiubunifu au katika uwezo ambao walipaswa kuuonyesha wakiwa na umri husika.

Badala ya kuwadharau na kuwadunisha ni vema kutumia wasaa huo kuwapa mifano ya walioanguka na waliofaulu katika kutimiza ndoto za maisha bora.

Tatu, kuwafundisha fikra za uzalendo na kuipenda nchi yao. Makosa ambayo wazazi wengi wamekuwa wakifanya ni kusifia nchi za wenzetu na kubeza nchi yao.

Ikumbukwe wao walikuwa na jukumu la kuleta mabadiliko ya hali iliyopo bila hofu na ubinafsi wa kuwa mabubu.  Hiyo ni dhambi kubwa. 

 Ni lazima watoto na vijana wajengewe  morali wa kuiamini nchi yao, kuwasimulia uzuri na umuhimu wa kuzitambua, kuzithamini, kuzitunza na kuzilinda rasilimali zao tangu wakiwa watoto na vijana.

Wazazi, walezi na watu wazima wanaposhindwa kuzungumza haya mbele ya watoto na vijana wao, inawezekana kujengeka taswira hasi ya kuwa hakuna jema wala kesho njema kwa nchi yao.

Pia, watu wazima wasijisahau kuwa wao ni sehemu ya mojawapo ya walioruhusu unyonge huo wa kifikra, hivyo wasiendeleze mkufu huo wa matatizo kwa kizazi chao.

Nne, kuwashauri pale kunapokuwa na dalili za kutaka kukengeuka. Ikibidi mzazi atumie mifano halisi ya watu walioharibikiwa kimaadili na jinsi maisha yao yalivyogeuka kuwa mabaya.

Tafiti za wanasaikolojia zinaonyesha kuwa watoto pia huamini fikra zao zaidi. Hivyo, anaposhauriwa ni vema akapewa na sababu za umuhimu wa ushauri ili aache njia mbovu.

Tano, kuwasikiliza watoto kwa umakini ili kugundua ni wapi pengine mzazi au mlezi umetofautiana naye ili uweze kubuni suluhisho ya tofauti hizo mapema.

Watoto huweza kujenga uasi wa kudumu katika fikra zao na mitazamo yao pale ambapo huvunjwa moyo na wazazi au walimu wao kwa kudharauriwa na kuvizwa ndoto ‘maono’ na fikra zao.

Sita, kuwakumbusha vyanzo muhimu vya kujipatia maarifa na taarifa. Ni wakati mwafaka wa kujadili nao vipindi vya runinga au redio vyenye maadili.

Pia, kusoma vitabu, majarida na magazeti yenye habari na maarifa safi kulingana na umri wao.

Jamii inaweza ikawalaumu bure watu wazima wasiosoma au kufuatilia mambo katika vyombo vya habari, lakini ikasahau kuwa hawakujengewa misingi tangu wakiwa watoto na vijana.

Saba, kuwafurahisha kwa kadri iwezekanavyo kwa kucheza nao. Pia, mzazi au mlezi anaweza kufanya shughuli za nyumbani za kumwagilia bustani, kupika, kufanya usafi wa mazingira, kupaka rangi na kutengeneza mpira au baiskeli kwa kuwashirikisha watoto na vijana.

Mambo haya saba ni baadhi ya mambo ya ushauri wa msingi kwa  wazazi na walezi ambao husema kwamba wapatapo fursa ya kuwa na watoto au vijana,  hawachelewi kuwapiga makofi kutokana na kutokuwa na ‘vionjo’ vya kukaa nao chini na kuzungumza pamoja.

 Jamii kwa ujumla inapaswa kukumbuka kuwa watoto na vijana ambao hawajapata malezi na makuzi bora, hushindwa maisha na mwishowe hufanya matendo mabaya kama vile wizi, umalaya, uvutaji bangi na unywaji pombe uliokithiri.

Mawasiliano:  0658 423 258