Mambo sita ya kishindo katika taarifa ya CAG

Muktasari:

Kwa mujibu wa matakwa ya sheria hiyo, CAG lazima awasilishe taarifa ya ukaguzi wa hesabu za wizara, idara na taasisi zote za umma kwa Rais ifikapo Machi 31 ya kila Mwaka.

        Nilialikwa, nikakubali na kushiriki kikamilifu mjadala uliochambua taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2015/16 ambayo ilikabidhiwa kwa Rais John Magufuli na baadaye bungeni, kwa mujibu wa Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya Mwaka 2008.

Kwa mujibu wa matakwa ya sheria hiyo, CAG lazima awasilishe taarifa ya ukaguzi wa hesabu za wizara, idara na taasisi zote za umma kwa Rais ifikapo Machi 31 ya kila Mwaka.

Kama ilivyo ada, Mkaguzi aliwasilisha taarifa yake kwa wakati mwishoni mwa Machi, 2017 kama sheria inavyomtaka. Kutokana na kuwasilishwa kwa taarifa hiyo, Rais Magufuli amekwishaiwasilisha kwa Spika wa Bunge la Tanzania kwa ajili ya kujadiliwa na wabunge.

Kihistoria, ripoti hiyo hujadiliwa katika mkutano wa Bunge unaofuata ambao utakutana Oktoba, 2017.

Kabla ya kufika kwa muda wa kujadiliwa rasmi kwa taarifa hiyo bungeni, ilionekana kuwa ni vyema kuichambua ripoti hiyo kwa umakini mkubwa na kubainisha mambo muhimu yaliyojiri kwa mwaka huu na ambayo yanahitaji jicho la kipekee la wabunge na Watanzania.

Taasisi mbili za kiraia za Wajibu na FCS ziliwezesha matokeo ya uchambuzi huo kuwasilishwa katika mkutano nilioshiriki katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Kutokana na mawasilisho katika mkutano huo na ufukunyuzi wangu mwenyewe, nimebaini hoja sita za kishindo ambazo ninazijadili katika safu hii kwa lengo la kuwashirikisha Watanzania wenzangu ambao hawakupata fursa ya kufika Serena na ambao hawana uwezo kama mimi wa kuzama katika taarifa ndefu namna hiyo.

Aidha, uchambuzi huu utachangia kuhamasisha waheshimiwa wabunge kusubiri mjadala wa taarifa ya CAG kwa hamu zaidi.

Ulinzi wa CAG

Kwa bahati nzuri, CAG kama taasisi ana ulinzi mkubwa wa kikatiba na kisheria. Ibara ya 143(1) ya Katiba ya Tanzania inaanzisha ofisi ya CAG na kumpa majukumu makubwa mawili ya kuidhinisha utolewaji wa fedha kutoka mfuko mkuu wa Hazina kwa ajili ya matumizi ya umma [ibara ya 143 (2) (a)] na kukagua na kutolea taarifa juu ya ukaguzi wa hesabu za umma angalau mara moja kila mwaka [ibara ya 143 (2) (c) na 143 (3)]. Aidha Katiba inaweka utaratibu wa namna CAG atakavyowasilisha taarifa ya ukaguzi kwa Rais ambaye naye ataiwasilisha bungeni kwa ajili ya kujadiliwa.

Jambo moja ya kishindo ni kwamba Rais hana hiari katika kuiwasilisha taarifa ya CAG bungeni, hata kama itakuwa imeibua ufujaji wa kutisha wa fedha za umma katika ofisi yoyote ikiwamo Ikulu.

Jambo la muhimu na la kishindo zaidi ni kwamba endapo Rais atasita au kuchelewa kuiwasilisha taarifa hiyo bungeni, basi CAG atachukua jukumu la kuiwasilisha yeye mwenyewe kwa mujibu wa ibara ya 143 (4), kwa Spika wa Bunge kwa ajili ya kujadiliwa na Bunge la Tanzania.

Aidha, itawashangaza wengi kufahamu kuwa CAG anateuliwa, lakini hawezi kufukuzwa na Rais kwa sababu yoyote ile isipokuwa atalazimika kuacha kazi yeye mwenyewe atakapotimiza umri wa kustaafu wa miaka 60 au umri mwingine wowote utakaotajwa na Sheria ya Bunge (ibara ya 144 (1)).

Mambo pekee yanayoweza kumfanya CAG aondoke kazini kabla ya muda wa kustaafu ni kwa sababu za maradhi au uvunjifu wa sheria ya maadili ya umma na kwamba ili hilo litokee, ataundiwa Tume Maalumu na Rais.

Tume hiyo itakuwa na mwenyekiti na wajumbe wengine wasiopungua wawili ambao wote watakuwa ni majaji au watu waliowahi kuwa majaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani katika nchi yoyote ya Jumuiya ya Madola.

Tume hiyo ndiyo inaweza kupendekeza kuwa CAG husika aondolewe au abaki kazini pamoja na tuhuma alizonazo.

Kwa ujumla, CAG hawezi kutumbuliwa na Rais kirahisi rahisi kama wateule wake wengine wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya wanavyotumbuliwa.

Ili kuhakikisha kuwa nafasi ya CAG inabaki kuwa huru, Katiba inazuia mtu aliyewahi kuwa CAG asiteuliwe au kuchaguliwa kushika madaraka ya kazi nyingine yoyote katika utumishi wa umma baada ya kustaafu kwake.

Ndiyo maana hakuna CAG mstaafu aliyewahi kuteuliwa au kuchaguliwa kutumikia Serikali kwa namna na nafasi yoyote ile. Ludovick Utouh mwenyewe ameamua kuendelea kutumikia Taifa kama mkurugenzi wa asasi ya Kiraia ya Wajibu na si vinginevyo.

Masharti hayo ya kazi ya CAG yamefafanuliwa zaidi katika Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya Mwaka 2008 (kama ilivyorekebishwa), pamoja na kanuni zake za mwaka 2009. Aidha, majukumu ya CAG kufanya ukaguzi wa hesabu za umma pia yanatajwa katika Sheria ya Manunuzi ya Umma Na. 20 ya Mwaka 2011 hasa katika kifungu cha 48 (3).

Taarifa yenyewe

Kuhusu taarifa ya CAG kwa mwaka 2015/6, kuna mambo mengi ya kushtua. Awali, CAG anaanza kwa kurejea mambo kadhaa yatokanayo na taarifa zake za miaka iliyopita.

Katika hilo, taarifa inabainisha kwa masikitiko makubwa kuwa utekelezaji wa mapendekezo ya CAG na maagizo ya Bunge kupitia kamati za kudumu za masuala ya fedha za umma kwa Serikali Kuu (PAC) na Serikali za Mitaa (LAAC), umekuwa mdogo na wa kusuasua.

Kwa mfano, taarifa inabainisha kuwa kati ya mapendekezo ya CAG kwa mwaka 2014/5, wizara na mashirika zilitekeleza asilimia 18 ya mambo yaliyopendekezwa.

Mbaya kuliko hilo, kati ya mapendekezo 79 ya CAG kwa mamlaka za tawala za mikoa na Serikali za mitaa ni asilimia nne pekee ilitekelezwa huku asilimia 35 ikiwa kwenye utekelezaji kwa sasa.

Kwa hesabu zangu mwenyewe, hilo linamaanisha kuwa zaidi ya nusu ya mapendekezo na maagizo yote kwa mamlaka za Serikali za mitaa hayakutekelezwa, jambo ambalo ni la kuudhi na kushtua.

Hata katika ngazi ya Bunge, maagizo na mapendekezo yapatayo 290 yalitolewa na Kamati ya PAC kwa wizara, idara na mashirika ya umma katika mwaka wa ukaguzi uliopita, lakini kwa ni asilimia 35 pekee yametekelezwa hadi sasa.

Taarifa ya CAG inaonyesha kuwa asilimia 30 ya maagizo ya PAC yalikuwa katika hatua za mwanzo kuanza kutekelezwa huku asilimia 35 yakiwa hayajaguswa kabisa na wizara, idara, mifuko, vyama na tawala za mikoa ambazo kwa ujumla zilifikia 253.

Kuhusu matokeo ya ukaguzi na hati zilizotolewa, pia kulikuwa na mambo ya kushtua. Kwa mfano, taarifa inaonyesha kuwa jumla ya hati safi zinazotolewa na CAG zinapungua badala ya kuongezeka kwa kadri miaka inavyosonga.

Katika mwaka wa ukaguzi wa 2013/14 kiwango cha hati safi (unqualified opinion) zilizotolewa na mkaguzi kilifika asilimia 94 huku mwaka uliofuatia zikipungua na kufikia asilimia 91.

Kwa mshangao, hati safi kwa ukaguzi wa mwaka 2015/2016 zimeporomoka zaidi na kufikia asilimia 86.

Wakati huohuo, Kiwango cha hati chafu au zisizoridhisha kimezidi kupanda. Kwa miaka mitatu mfululizo, hati zisizoridhisha zimekuwa zikiongezeka kutoka tano (2013/14), nane (2014/15) hadi 11 (2015/16).

Hiyo peke yake inatisha na kuleta picha kuwa heshima kwa mapendekezo ya taarifa ya mkaguzi pamoja na maagizo na maelekezo ya Bunge vyote haviheshimiwi na watendaji wa Serikali.

Labda itakuwa vema kwa Bunge na wabunge kujiuliza watakapokuwa wanajadili taarifa ya CAG kwa mwaka wa ukaguzi 2015/6 baadaye mwezi Oktoba mwaka huu.

Je, kwa nini mapendekezo, maagizo na maelekezo ya CAG na Bunge kupitia kamati za PAC na LAAC hayaheshimiwi na Serikali? Je nini kinaweza kufanyika ili kuongeza heshima ya Serikali kwa mapendekezo, maagizo na maelekezo hayo?

Deus M Kibamba ni Mtafiti, Mhadhiri na Mchambuzi wa Masuala ya Siasa za Kimataifa na Demokrasia ya Katiba. Anapatikana kwa simu: +255 788 758581 au barua pepe: [email protected]