Maridhiano ndiyo suluhisho la kudumu Z’bar

Muktasari:

Baada ya uchaguzi huo mpasuko wa kisiasa Zanzibar ukaibuka baada ya chama kikuu cha upinzani Chama cha Wananchi (CUF) kudai kwamba kilishinda uchaguzi huo, lakini Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ikamtangaza mshindi mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hali ya kisiasa Zanzibar ilianza kuwa ya utatanishi baada ya Uchaguzi Mkuu wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi vya siasa uliofanyika mwaka 1995 miaka michache baada ya mfumo huo kuanza mwaka 1992.

Baada ya uchaguzi huo mpasuko wa kisiasa Zanzibar ukaibuka baada ya chama kikuu cha upinzani Chama cha Wananchi (CUF) kudai kwamba kilishinda uchaguzi huo, lakini Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ikamtangaza mshindi mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hali hiyo ilileta msuguano baina ya vyama hivyo viwili na wafuasi wao wakaanza kubaguana katika huduma mbalimbali za kijamii na hali ya utulivu na amani kutoweka katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Sintofahamu ikazidi kuwa mbaya katika Kisiwa cha Pemba ambako kulikuwa na matukio kadhaa ya hujuma na kuharibu miundombinu na wakati mwingine kutia vinyesi katika visima vya maji ya kunywa na kuchoma shule.

Hata hivyo, vitendo hivyo vilikoma baada ya kugundulika kwamba wanaovifanya siyo wafuasi wa CCM wala CUF, bali ni watu wengine na tukio la kutambua hivyo lilitokea katika Shule ya Shengejuu iliyopo Wilaya ya Wete Kaskazini Pemba.

Pamoja na vitendo hivyo kukoma hali ya kubaguana kati ya wafuasi wa CCM na CUF iliendelea hadi awamu ya Serikali iliyofuata licha ya kuwapo mwafaka ambao ulisimamiwa na Jumuiya ya Madola.

Hali hiyo ya mvutano ilimalizika baada ya Wazanzibari wenyewe kuamua kuufikia mwafaka ambao ulileta hali ya amani na utulivu Zanzibar.

Mwafaka huo ulioafikiwa kati ya CCM na CUF ukiongozwa na aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na kuidhinishwa na wananchi kupitia kura ya maoni mwaka 2009.

Suluhu hiyo ilileta hali ya utulivu na amani katika visiwa vya Zanzibar kiasi kwamba wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 wakati wa kampeni za uchaguzi huo vijana wa CCM na CUF walikuwa wakikutana barabarani wanasimamisha magari yao na kucheza ngoma kwa furaha.

Mwafaka huo uliiwezesha Zanzibar kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyoongozwa na CCM na CUF kwa kipindi cha miaka mitano hali iliyoleta amani na utulivu na Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2005 ukafanyika kwa amani na utulivu wa hali ya juu.

IGP Mangu amshukia Maalim Seif

Akizungumza katika kipindi cha Funguka kinachorushwa na Azam TV hivi karibuni na kuongozwa na mtangazaji Tido Mhando, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu alitamka kwamba vurugu za Zanzibar zimechochewa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif.

Kama madai hayo yangetolewa na mwanasiasa yangechukuliwa kuwa ni madai ya kisiasa na wala asingezua mjadala wowote ule yangeachwa tu yakapita na upepo.

Aliyeyatoa kauli hiyo ana wadhifa mkubwa na ana mamlaka makubwa ya kulinda usalama wa raia na mali zao kwa hiyo kauli yake haiwezi kupita bila kuzua mjadala.

IGP Mangu inasikitisha kwamba ametoa kauli hiyo kama mtu ambaye haelewi lolote lililotokea Zanzibar wala hajui mpasuko wa kisiasa katika visiwa hivyo umesababishwa na jambo gani.

Siyo jambo la siri wala halihitaji mtu kutafuna maneno kwamba kilicholeta mpasuko wa kisiasa Zanzibar ni kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015 na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

Mpasuko huo wa kisiasa Zanzibar uliongezeka baada ya ZEC kuitisha uchaguzi wa marudio wa Zanzibar bila ya kutafuta mwafaka wa vyama vyote vya siasa na kuufanya ususiwe na vyama 10 vikiongozwa na CUF.

Waangalizi wa ndani na wa kimataifa walitamka bayana kwamba Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 ulikuwa huru na haki na ulifanyika kwa njia ya amani.

Kitendo cha Jecha cha kuufuta uchaguzi huo Oktoba 28 mwaka jana siku ambayo alitakiwa kutangaza mshindi wa kiti cha urais wa Zanzibar ndilo jambo ambalo limezua uhasama baina ya wananchi na kuwafanya wabaguane katika huduma za jamii.

Hatua hiyo ya kufutwa Uchaguzi Mkuu ilikifanya CUF kidai kuwa kiliporwa ushindi na kudai kuwa demokrasia ilibakwa jambo ambalo limeudhi wafuasi wake.

Pia, kufanyika kwa uchaguzi wa marudio uliozibadilisha nafasi 27 za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka CUF na madiwani 52 wa chama hicho wakiwamo wote kutoka Pemba kwenda kwa CCM kuliwaudhi zaidi wafuasi wa CUF.

Katika mazingira hayo kwa vile wananchi hao walioudhika hawana uwezo wa kutumia njia za nguvu katika kuonyesha hasira zao wakaamua kuchagua njia hiyo ya kubaguana, lakini haikutokana na ushawishi wa Maalim Seif.

Hata hujuma zinazotokea na kuharibiwa mazao na miti ya biashara zinahitaji uchunguzi wa kina wa hali ya juu kubaini kwamba ni nani walihusika kwani kwa mazingira ya Zanzibar kuna uwezekano mkubwa wanao fanya hivyo siyo wafuasi wa CUF wala CCM.

Suluhu siyo kamata kamata

IGP Mangu alieleza kwamba wataendelea kuwakamata wanaodaiwa kufanya uhalifu katika Zanzibar na baada ya kumhoji Maalim Seif alisema kuwa watampeleka mahakamani kujibu mashtaka ya uchochezi.

Hilo halina shaka kwani kazi ya Polisi ni kukamata na kushitaki, lakini kuhusu mpasuko wa Zanzibar unahitaji uangalizi na utatuzi wa ziada na siyo kukamata na kushitaki na hauwezi kutatuliwa kwa kutumia nguvu za Jeshi la Polisi.

Utulivu na amani utarejea Zanzibar iwapo kutakuwa na maridhiano ya pamoja kati ya vyama vikuu vya CCM na CUF kwa ajili ya kuondoa mpasuko wa kisiasa unaoiathiri Zanzibar.

Kwa hali ilvyo hivi sasa Zanzibar kwa namna yoyote ile mazungumzo baina ya CCM na CUF yanahitajika na itakuwa ni kujidanganya kuwa baada ya uchaguzi wa marudio kila jambo lipo sawa na mambo yatakwenda vizuri.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala la siasa na jamii, anapatikana kwa barua pepe: [email protected]