Masanja : Nimevuna mpunga ekari 15 Mbarali Estate Mbeya

Masanja Mkandamizaji

Muktasari:

  • Masanja ambaye pia ni mwimbaji wa kwaya ya New Jerusalem alisema: “Mimi ni mchungaji mtarajiwa lakini huduma yangu ya uchungaji nimeanzia kwenye kundi langu hili la Ze Komedy, kupitia hilo nina washirika wangu ambao natamani wawe kama mimi mchungaji wao wafuate nyayo zangu, naomba maombi ya watumishi wengine wamuombee Joti

Mchekeshaji maarufu kupitia kipindi cha Ze Orijino Comedy, Emmanuel Mgaya maarufu kama Masanja Mkandamizaji amesema kuwa vijana wanapaswa kufikiria namna ya kuwekeza mashambani kwenye fursa za kutosha kuliko kuendekeza majivuno yasiyo na msingi.

Akizungumza na Starehe Masanja alisema anafurahi kwani mwaka huu amefanikiwa kuvuna tani kadhaa za zao la mpunga katika shamba lake lililopo Mbarali Estate.

“Nimelimia Mbarali Estate namshkuru Mungu kwa kufanikiwa kuvuna mpunga wangu baada ya kuwekeza shamba lenye ukubwa wa ekari 15, huu ni uwekezaji mzuri unaotoa matunda kwa muda mfupi iwapo utahudumia shamba lako ipasavyo.”

“Vijana wengi wana nguvu na uwezo wa kuingia mashambani ila wanaendekeza ‘usharobaro’ kitu ambacho hakina mavuno kwao,” alisema Masanja aliyetumia mashine ya kisasa katika zoezi hilo.

Masanja ambaye pia ni mwimbaji wa kwaya ya New Jerusalem alisema: “Mimi ni mchungaji mtarajiwa lakini huduma yangu ya uchungaji nimeanzia kwenye kundi langu hili la Ze Komedy, kupitia hilo nina washirika wangu ambao natamani wawe kama mimi mchungaji wao wafuate nyayo zangu, naomba maombi ya watumishi wengine wamuombee Joti,” alisisitiza!

Kwa sasa, Masanja anahudhuria ibada katika kanisa la EAGT, Mito ya Baraka pia amefanikiwa kutoa nyimbo 10 za Injili na tayari album yake ya ‘Hakuna Jipya’ iko mitaani.