Mastaa Ivory Coast wapewa Sh13bil kutetea ubingwa

Wachezaji wa Ivory Coast wakishangilia baada ya kutwaa ubingwa wa Afcon mwaka juzi.

Muktasari:

DONDOO: Kocha wa Ivory Coast amesema ameita mchezaji mmoja tu wa ndani, wengine wote ni wanaocheza nje ya nchi hiyo

Wakati kocha mkuu wa Ivory Coast, Michel Dussuyer akiita wachezaji 24 wa kulipwa kutetea ubingwa, Serikali ya nchi hiyo imetenga Sh12.9 bilioni kwa ajili ya timu hiyo.

Waziri wa Michezo wa Ivory Coast, François Albert Amichia alisema kuwa imetenga Dola6mil kwa ajili ya The Elephants kushiriki Fainali za Afcon 2017 nchini Gabon.

Taarifa ya Serikali imesema kuwa fedha zinazotumika kwa ajili ya fainali hizo, ni sawa na kiasi kilichotumika kufikia hatua hiyo.

Fedha hizo zilizotolewa na Serikali, zimesababisha wachezaji wa Ghana kuanza mzozo na wao wakitaka wapewe fedha ‘ndefu’ kama wenzao wa Ivory Coast.

Mabingwa hao watetezi wako Kundi C, wataanza kutetea ubingwa wao dhidi ya Togo Januari 16 kabla ya kuivaa DR Congo na Morocco.

Katika fainali zilizofanyika Equatorial Guinea, Ivory Coast ilitwaa ubingwa kwa kuifunga Ghana penalti 9-8.

Mafanikio

Ivory Coast inawania kutwaa ubingwa mara ya tatu, ilianza kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka 1992 dhidi ya Ghana kwa mikwaju ya penalti mechi iliyopigwa Stade Leopold Senghor mjini Dakar, Senegal kabla ya kurudia tena mwaka 2015 kwa kuilaza Ghana kwa mikwaju ya penalti, mechi iliyochezwa Estadio de Bata kwenye mji wa Bata, Guinea ya Ikweta.

Nyota 24

Dussuyer ameshaita wachezaji 24, akiwamo Serge Aurier wa PSG, na beki wa Manchester United, Eric Bailly na Lamine Kone  wa  Sunderland.

Pia yumo Serey Die wa FC Basel na dogo, Franck Kessie wa Atalanta Bergamo. Straika Wilfried Bony na Salomon Kalou, pia wameitwa.

Timu hiyo itaanza kutetea ubingwa dhidi ya Togo Januari 16 kwenye Uwanja wa Oyem, na baadaye kucheza na DR Congo siku nne baadaye kwenye uwanja huo wa Oyem itacheza na Morocco.

Winga wa Crystal Palace, Wilfried Zaha ameitwa kwenye kikosi cha Ivory Coast ikiwa ni mara ya kwanza, kwani aliwahi kuichezea England, 2012 dhidi ya Sweden na mwaka uliofuata dhidi ya Scotland.

Beki wa Manchester United, Eric Bailly yumo huku Dussuyer, akimwita mkongwe, Salomon Kalou ikiwa ni fainali zake za tano.

Kikosi kinaundwa na:

Makipa: Sylvain Gbohuo (TP Mazembe, DR Congo), Badra Sangare (AS Tanda, Ivory Coast), Mande Sayouba (Stabaek, Norway)

Mabeki: Serge Aurier (PSG, Ufaransa), Mamadou Bagayoko (St Trond VV, Ubelgiji), Eric Bailly (Man United, England), Simon Deli (Slavia Prague, Jamh ya Czech), Ousmane Viera Diarrassouba (Adanaspor, Uturuki), Wilfried Kanon (ADO, Uholanzi), Lamine Kone (Sunderland, England) na Adama Traore wa Basel ya Uswisi.

Viungo: Victorien Angban (Grenada, Hispania), Cheik Doukoure (Metz, Ufaransa), Franck Kessie (Atalanta, Italia), Yao Serge N’guessan (Nancy, Ufaransa), Geoffroy Serey Die (Basel, Uswis), Jean Michael Seri wa Nice ya Ufaransa.

Washambuliaji: Wilfried Bony (Stoke, England), Max Gradel (Bournemouth, England), Salomon Kalou (Hertha Berlin, Ujerumani), Jonathan Kodjia (Aston Villa, England), Nicolas Pepe (Angers, Ufaransa), Giovanni Sio (Rennes, Ufaransa) na Wilfried Zaha Palace ya  England.