Mastaa wa Man United walivyompa raha Mourinho

Muktasari:

  • Tofauti na michezo mingine ya Ligi Kuu England ambayo Man United ilionyesha udhaifu, juzi wachezaji wa timu hiyo walicheza kwa umakini licha ya kutangulia kufungwa dakika ya 11.

Alexis Sanchez ameongoza nyota wa Manchester United kucheza kwa kiwango bora na kurejesha matumaini kwa mashabiki wa klabu hiyo ya Old Trafford.

Tofauti na michezo mingine ya Ligi Kuu England ambayo Man United ilionyesha udhaifu, juzi wachezaji wa timu hiyo walicheza kwa umakini licha ya kutangulia kufungwa dakika ya 11.

Man United imetinga fainali baada ya kuinyuka Tottenha Hotspurs mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Wembley, London.

Wachezaji wa Man United walicheza kwa kiwango bora mchezo huo na kumpa furaha kocha Jose Mourinho.

Sanchez ambaye amekuwa akipewa lawama na wadau wa soka, alicheza vyema akifunga bao la kwanza kabla ya kiungo Ander Herrara kufunga bao la pili.

Awali, Spurs ilitangulia kufunga kwa bao lililowekwa wavuni na kiungo mshambuliaji Delle Ali aliyemchambua kipa David de Gea.

Mourinho amekiri alikuwa na wakati mgumu ndani ya nyumba vya kuvalia nguo baada ya kutokea mgawanyiko.

Licha ya kuibuka mzozo baina ya Mourinho na Paul Pogba, alimpanga nyota huyo wa Ufaransa katika mchezo huo.

Pogba amekuwa na mzozo wa mara kwa mara na bosi wake baada ya kudaiwa kiwango chake kupanda na kushuka.

Sanchez, mchezaji wa kimataifa wa Chile, hakumuangusha bosi wake, alirejesha makali yake kama zamani na alikuwa nyota wa mchezo.

Ushindi dhidi ya Spurs umewatuliza mashabiki waliokuwa wakimsakama Mourinho kwa madai ya timu yake kucheza chini ya kiwango.

Mourinho amesifu kazi nzuri ya wachezaji na amewashukia waliokuwa wakimponda wakidai Man United haichezi katika kiwango bora.

“Tunapaswa kujiuliza kwanini wamekuwa wakituponda, nadhani tunastahili kupata matokeo ,” alisema Mourinho.

Kocha wa zamani wa Man United Sir Alex Ferguson alikuwa jukwaani kushuhudia kikosi hicho kikipata ushindi mbele ya timu ngumu kutoka White Hart Lane.