Masuala ya kujadili ufufuaji wa viwanda

Muktasari:

  • Faida hizi ni pamoja na ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, mapato ya kikodi na yasiyo ya kikodi, fedha za kigeni, kukuza sekta nyingine zinazofungamana na sekta ya viwanda kwa kuwa soko kwa sekta hizi na kwa kuzipatia malighafi na bidhaa nyingine.

Serikali ya awamu ya tano imejipambanua na mambo kadhaa. Kati ya hayo, katika maendeleo ya uchumi ni kuwa na uchumi wa viwanda. Hili ni jambo zuri kwa sababu ya faida zake katika uchumi wa viwanda.

Faida hizi ni pamoja na ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, mapato ya kikodi na yasiyo ya kikodi, fedha za kigeni, kukuza sekta nyingine zinazofungamana na sekta ya viwanda kwa kuwa soko kwa sekta hizi na kwa kuzipatia malighafi na bidhaa nyingine.

Kati ya mikakati ya kufikia azma ya uchumi wa viwanda ni kuanzisha viwanda vipya na kufufua vilivyokuwapo lakini havifanyi kazi kwa sasa.

Katika muktadha wa kufufua viwanda, kuna masuala kadhaa ya kimjadala. Masuala hayo ni muhimu yakajadiliwa kwa upana ili kuchangia azma hiyo njema ya uchumi wa viwanda. Makala haya yanaonyesha baadhi ya masuala ya msingi ya kimjadala katika juhudi za kufufua viwanda.

Azma ya uchumi wa viwanda

Azma ya uchumi wa viwanda Tanzania imejadiliwa na kuandikwa sehemu nyingi. Kuna aina tatu kubwa za viwanda vinavyofikiriwa na Serikali ya awamu ya tano. Hivi ni viwanda vinavyoweza kuajiri watu wengi, vinavyoweza kuzalisha bidhaa kwa walaji wengi wa nchini na vile vitakavyozalisha ili kuuza nje ya nchi.

Pamoja na mambo mengine, Serikali inalenga kuimarisha viwanda vilivyopo; kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika pato ghafi la Taifa toka asilimia 9.9 ya 2013 hadi asilimia 15 ifikapo 2020. Pia, inalenga asilimia 40 ya ajira nchini itoke katika sekta ya viwanda ifikapo 2020 na inapanga kuishawishi sekta binafsi kuwekeza katika viwanda vidogo vya kati na vikubwa vikiwamo vitakavyotumia malighafi ya ndani kwa wingi.

Serikali pia inalenga kuvikinga viwanda vya ndani dhidi ya ushindani toka nje. Mpango mwingine ni kwa viwanda vya Tanzania kuuza katika masoko ya upendeleo ya Afrika Mashariki, Afrika, Ulaya, Marekani na Asia.

Kufufua viwanda

Kati ya mikakati ya kufikia aina ya uchumi wa viwanda inayofikiriwa na Serikali ni kufufua viwanda. Hii ina maana vipo viwanda vilivyokufa na sasa vinahitaji kufufuliwa. Historia ya uchumi wa viwanda Tanzania itaonyesha msukumo wa kuwa na uchumi wa viwanda ulioanza baada ya uhuru 1961. Imekuwapo mipango mingi ya uchumi iliyolenga pamoja na mambo mengine, kuwa na uchumi wa viwanda. Viwanda vingi vinavyotakiwa kufufuliwa wakati huu ni pamoja na vile vilivyokuwa vikimilikiwa na watu binafsi kabla ya 1967 na kutaifishwa katika Azimio la Arusha la mwaka 1967. Vingine ni vile vilivyoanzishwa na Serikali wakati wa Ujamaa. Viwanda hivi vilibinafsishwa wakati wa mageuzi makubwa katika uchumi wa Tanzania katikati ya miaka ya 1980 hadi 1990.

Masuala ya kimjadala

Yapo masuala kadha wa kadha ya kimjadala katika mkakati wa kufufua viwanda. Ni muhimu kuyajadili masuala haya kwa kina na upana wake ili kusaidia na kuchangia katika mijadala na hatimaye mafanikio ya azma ya kuwa na uchumi wa viwanda. Yafuatayo ni baadhi tu ya masuala ya msingi ya kimjadala katika muktadha wa ufufuaji wa viwanda;

Kwanini vilikufa

Kati ya masuala ya msingi ya kimjadala katika juhudi za kufufua viwanda ni kujua kwanini vilikufa. Kuna sababu nyingi nazo ni pamoja na uongozi na uendeshaji mbaya, ukosefu wa mitaji na utaalamu wa kutosha, ushindani mkubwa, teknolojia iliyopitwa na wakati, ukosefu wa nguvukazi madhubuti, ukosefu wa malighafi, hujuma na kuisha kwa muda wa kuishi wa mitambo. Ili kuwe na mafanikio ya kufufua kiwanda chochote, lazima utafiti wa kina ufanyike kujua ni nini kilisababisha kife na muhimu wa nini kifanyike kukifufua. Utafiti huo unaweza kufanywa kwa ngazi na muktadha mbalimbali. Kwa mfano, wanafunzi wanaofanya utafiti wa kina kwenye ngazi mbalimbali chini ya uangalizi na mwongozo wa walimu wao wanaweza kutoa mchango mkubwa katika hili.

Vinafufuka?

Si kila kilichokufa kinaweza kufufuka. Kabla ya kuingia gharama za kufufua viwanda mfu kama ilivyo kwa biashara nyingine ni lazima kujiuliza kama kiwanda husika kitafufuka.

Lengo halipaswi kufufua tu, bali kufufua na kuhakikisha vinafanya uzalishaji bora na wa kisasa. Katika hili ni muhimu kujua, baadhi ya viwanda mfu ni vya zamani sana. Uchakavu na ‘ufu’ wa kiwanda unaweza kuwa mkubwa kiasi cha juhudi na gharama za kufufua zikawa kubwa kuliko faida kiuchumi.

Hii ni muhimu kuelewa ili kuepuka fikra kuwa kila kilichokufa lazima kifufuliwe. Hata kama kitafufuliwa kwa kiasi kikubwa, lazima kiwe tofauti na kilichokuwapo. Hii ni kwa sababu ya mabadiliko ya haraka kwenye nyanja mbalimbali za uchumi, biashara, teknolojia, mazingira, sera, sheria, mikakati na udhibiti. Hii inaibua suala jingine la kimjadala ambalo ni uanzishaji upya badala ya kufufua.

Fufua au anza upya

Uchambuzi yakinifu unaweza kuonyesha kwa baadhi ya viwanda hasa vile vya zamani sana, ni bora kuanza ujenzi upya badala ya kufufua.

Hii ni katika muktadha wa mabadiliko makubwa ya kiteknolojia pamoja na mambo mengine. Kwa maendeleo ya sasa kiteknolojia kwa mfano, pengine viwanda havitahitaji eneo kubwa kama ilivyokuwa miaka ya sitini, sabini na themanini. Ufanisi wa mitambo iliyofufuliwa unawezakuwa mdogo kuliko mtambo mpya. Katika hali hii italipa zaidi kiuchumi kuanza kiwanda kipya kuliko kufufua cha zamani.

Soko

Masoko ya bidhaa na huduma hubadilika mara kwa mara. Viwanda vilivyoanzishwa miaka ya 1960 hadi 1980 vililenga katika kuzalisha aina fulani ya bidhaa katika mazingira ya wakati ule.

Kwa kiasi kikubwa miaka ya 1960 hadi katikati ya miaka ya 1980 Tanzania ilikuwa na uchumi usiotizama sana nje. Bidhaa za viwandani kutoka nje hazikuwa nyingi kama miaka hii ya 2010. Kabla ya kufufua viwanda vilivyokuwa vikizalisha bidhaa ambazo kwa sasa zinatoka nje kwa wingi ni muhimu kuona kuwa kuna haja ya kuanzisha viwanda vipya vitakavyoshindana na bidhaa za nje kwa mazingira ya sasa ya soko.