Maswali yanayowatesa wanafunzi wa kike

Wanafunzi wa kike kama hawa pichani, wanakabiliwa na vikwazo vingi vya kimaisha, ikiwamo unyanyasaji wa kijinsia. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Swali hilo gumu ni kati ya mengi yanayowatesa wanafunzi wa kike na kuamua kuchukua hatua zinazoweza kuathiri maisha yao kwa kukosa majibu.

“Ikiwa wewe ni mwanafunzi wa kike umepata mimba, halafu ukafukuzwa nyumbani, shuleni na mwanaume aliyekupa mimba hiyo akakukataa; utafanyaje?”

Swali hilo gumu ni kati ya mengi yanayowatesa wanafunzi wa kike na kuamua kuchukua hatua zinazoweza kuathiri maisha yao kwa kukosa majibu.

Shirika la Kimataifa la Equality Now lilikutana na maswali hayo lilipoamua kufanya utafiti wa sauti za wanafunzi wa kike walio na umri wa kati ya miaka 11 hadi 18.

Lengo hasa lilikuwa kujua changamoto wanazokumbana nazo, nje ya zile zinazojulikana na ambazo zimekuwa zikitajwa kama sababu ya kupata mimba katika umri mdogo na hatimaye kuacha masomo yao.

Katika mkutano wa shirika hilo ulioandaliwa kwa kushirikiana na Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenment), wadau wa elimu nchini walichambua maswali 12 yanayowatesa wanafunzi hao ili kuja na suluhisho la kumaliza ukatili wa kijinsia, mimba na ndoa za utotoni.

Wanafunzi wengi wa kike hawajui nani anaweza kuwajibu hasa wanapokumbana na changamoto zinazotishia kuondolewa masomoni.

“Maswali yao hayana majibu, hawajui wafanye nini na wapi wapate majibu hayo. Hii ni sababu nyingine, ya kundi hili muhimu katika maendeleo ya taifa siku zijazo kuangamia,” anasema Mratibu wa sauti za watoto wa kike, wa Equality Now, Florence Machio.

Machio anasema walitaka kujua na kuandaa mkakati wa namna wanavyoweza kuwasaidia wanafunzi hao kutimiza ndoto zao za maisha.

Meneja miradi wa Tenment, Nikodemus Eatlawe anasema maswali mengi kwa wanafunzi hao yanatokana na ukweli kwamba, hawapati elimu ya afya ya uzazi, makuzi, jinsia na kujitegemea.

Wengi wanapokutana na mambo magumu huishia kufanya maamuzi hata yale yanayoweza kusababisha, utu wao ukapotea na mwisho kufukuzwa masomo.

“Maana yake tumewasahau watoto wetu, hatuwapi nafasi ya kuzungumza nao kwa sababu kila mtu katingwa,” anasema na kuongeza;

“Mwanafunzi anapokosa majibu ya maswali yake, anatafuta yake hata yale yanayoweza kumuathiri. Ni hatari.”

Machio anasema sio kwa Tanzania tu, nchi nyingi za Afrika, hazina sera na miongozo inayoweza kuwasaidia wasichana kujitambua.

“Mila na desturi zinawaweka mbali wanafunzi wengi wa kike, kuna maswali mengine tuligundua watoto wamejitwisha kwa muda mrefu na hawajui wafanyaje, ”

Fikiria unakutana na mtoto aliyewahi kubakwa na mtu wake wa karibu! Halafu anauliza afanye nini kwa sababu, alikataaa kusema,” anasema.

Ndoa za utotoni, mimba na mwisho kuacha masomo ni moja kati ya athari za watoto kukosa elimu ya afya ya uzazi na makuzi.

Mwaka jana kulikuwa na mjadala mpana kuhusu watoto wa kike wanaopata mimba shuleni kufukuzwa shule.

Eatlawe anasema japo kuna nia mbadala za kumsaidia mwanafunzi wa kike kuendelea na masomo yao wakati anapopata mimba, nguvu kubwa lazima ielekezwe kuhakikisha anaandaliwa mazingira mazuri ya kusoma.

Maswali magumu

Mratibu wa Tenment, Cathleen Sekwao anasema baadhi ya wanafunzi wametumbukia kwenye kwenye ngono, mimba zisizotarajiwa na hivyo kufukuzwa masomo yao na wengine, hata kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa kutojua.

“Kama mtoto hajui h unadhani ataweza kujinasua kwenye mitego anayowekewa? Lazima tuje na suluhisho,” anasema.

Wadau hao wa elimu katika utafiti wao walikutana na mtoto wa miaka 11, aliyekuwa akijiuliza namna atakavyoweza kumweleza baba yake kuhusu kuvunja ungo ikiwa mama yake hatakuwepo nyumbani.

“Kwa hiyo mwanafunzi huyu wa miaka 11 anajua kuna kuvunja ungo, lakini anajiuliza anawezaje kumweleza baba yake? Kama angepata nafasi ya kupata elimu ya makuzi, swali hilo lisingekuwa gumu sana kwake.

Anafafanua kuwa wanafunzi wengi wa kike wanapopevuka, hushindwa kusema ukweli na kuwaficha wazazi wao hasa wakiume, wakihofia suala la mila na desturi.

“Huyu mtoto aliuliza kama baba yake ndiye yupo nyumbani wakati anapopevuka, mama yake hayupo, ni sawa kumweleza ukweli? Swali hili linaonekana kumsumbua na huenda lilimkuta. Lakini pengine alikaa kimya alipoona mabadiliko ya mwili wake,” anasema.

Swali jingine linalowatesa wanafunzi wengi wa kike ni sababu zinazowafanya baadhi ya walimu kutaka kufanya nao ngono.

“Mwanafunzi aliyeuliza hili swali inaonekana linamtesa sana kwa sababu aliuliza kwa hisia akisema; ‘Kwa nini sasa walimu hawa wa kiume wanataka ngono na wanafunzi wao’, inasikitisha,” anasema.

Mratibu huyohuyo aliuliza akiamini, mwalimu anapaswa kuwa mlezi mwenye hekima na maadili sasa pale anapoamua kufanya jambo kinyume na maadili yake, linawapa maswali magumu wasichana hawa.

Anasema swali jingine walilokutana nao ni sababu zinazowafanya wanaume kuwabaka watoto wa kike!

Analitaja swali jingine kuwa ni kujua kama msichana aliyekeketwa anaweza kushika ujauzito.

Anasema wanafunzi wengi wa kike wanajiuliza Serikali inaweza kuwasaidia vipi, pale wazazi wao wanapowalazimisha kuacha masomo na kuolewa.

Anasema wapo wasichana wengi wamejikuta wakiozwa kwa kulazimishwa wakati wakiwa masomoni na hawajui hatua wanazoweza kuchukua wakati suala hilo linapotokea.

“Je, mtoto akibakwa inafaa kufukuzwa nyumbani? Hili ni swali jingine linalowatesa,” anasema.

Nini kifanyike?

Wadau wa elimu wanasema mbali na kushughulikia suala la miundombinu shuleni ikiwamo mabweni, uhakika wa vifaa vya kujisitiri wakati wa hedhi, vyoo na maji, lazima suala la jinsia liingizwe kwenye mtalaa wa elimu.

“Watoto wawe huru na wajifunze tangu wadogo kuhusu masuala ya jinsia, hii itawaongezea uelewa,” anasema Nashivai Mollel, ambaye ni ofisa mhamasishaji wa jamii wa asasi ya Femina Hip.

Anasema lazima wazazi na walezi wajenge urafiki na watoto wao, ili wakati wanapokuwa na maswali hayo magumu iwe rahisi kuzungumza nao.

Kauli ya Serikali

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Anna Mhina anasema ni kweli kwamba, wanafunzi wa kike wakiweza kujibiwa maswali yao ya msingi wanaweza kukwepa mitego mingi ambayo mwisho wake huwa ni kuwaangamiza kielimu.

“Serikali inatambua kwamba mtoto wa kike anahitaji elimu ya afya ya uzazi, elimu ya jinsia na uangalizi wa karibu sio tu anapoanza kukua au anapokua, hata wakati akiwa mdogo,” anasema.

Anasema Serikali kwa kutambua changamoto hizo imeshaandaa mpango kazi wa kupinga ukatili dhidi ya watoto.

“Kwa hiyo walimu shuleni, maofisa maendeleo ya jamii wa ngazi zote kuanzia vijiji wana kazi ya kuwasaidia watoto na kuwaelewesha wazazi umuhimu wa kuwa karibu nao,” anasema.

Mhina anasema sio tu jukumu la Serikali isipokuwa wadau wote wanapaswa kushiriki katika kuhakikisha mtoto wa kike anaanza masomo yake na kumaliza salama kama ilivyo kwa mtoto wa kiume.