Matatizo ya mfumo wa chakula wakati wa mfungo

Muktasari:

Wakati Waislamu wote duniani wakiwa kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni sehemu moja wapo ya kutekeleza nguzo tano za dini ya Kiislamu ni vyema kuifahamu afya yako

Kipindi hiki Waislamu wote duniani wako katika Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kama sehemu ya imani yao. Uzoefu na machapisho mbalimbali ya kitaalam yanaonyesha kuwa baadhi ya wanaofunga huweza kupata matatizo mbalimbali ya kiafya hasa ya mfumo wa usagaji chakula.

Kwa kutambua hayo si vibaya kutoa elimu iwapo kutajitokeza matatizo ya kiafya kwa baadhi ya watu wanaotimiza ibada ya funga ambayo ni moja wapo ya maamrisho ya Mungu.

Wapo wanaofunga huku wana matatizo ya kiafya ya mfumo wa usagaji chakula ikiwamo wale wanaopata shambulizi la kuta za tumbo (Gastritis) na vidonda vya tumbo (Peptic ulcers disease).

Vile vile wapo ambao wana vihatarishi vya kupata matatizo haya, ikiwamo wale wenye uambukizi unaosababisha vidonda vya tumbo na wenye kiungulia cha muda mrefu.

Matatizo ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara yanayohusisha mfumo wa usagaji wa chakula ni kiungulia/kuzidi kwa tindikali, tumbo kujaa gesi na vidonda vya tumbo.

Kiungulia au kuzidi kwa tindikali ya tumboni huweza kusababisha shambulizi katika kuta laini za tumbo, hali inayojulikana kitabibu kama Gastritis.

Shambulizi katika kuta za tumbo huweza kusababisha kumomonyoka kwa kuta za tumbo na kutengeneza vidonda vya tumbo. Ingawa baadhi wanaweza kufunga na wasipate madhara yoyote au kusiibuke kwa madhara yoyote ila ni muhimu kuchukua tahadhari angalau kwa kufahamu viashiria na dalili zinazojitokeza mara kwa mara kama ishara ya uwapo wa tatizo la kiafya.

Mtu anayefunga na huku ana historia ya dalili kama kiungulia cha muda mrefu, kucheua na kutapika baada ya kula na historia ya kutumia dawa za kupunguza maumivu kwa muda mrefu bila kufuata ushauri wa daktari, wanapaswa kuwa na tahadhari kwani matatizo hayo yanaweza kuongezeka .

Dalili na viashiria vinavyoweza kujitokeza

Dalili zinazoweza kujitokeza kipindi hiki ni pamoja na kichefuchefu/kutapika, kiungulia, tumbo kuunguruma, kucheuwa mara kwa mara, kuhisi tumbo limejaa, kwikwi, koo kukereketa, kujaaa mate mengi baada ya kucheua, tumbo kuuma na kukosa hamu ya kula.

Pale inapotokea ni vidonda vya tumbo dalili huwa ni mbaya zaidi ikiwamo kupata maumivu makali ya tumbo katika maeneo ya chembe ya moyo, kupata maumivu makali kipindi anapokula au mara tu baada ya kumaliza kula .

Wakati kwa yule aliye na vidonda kwenye sehemu ya kwanza utumbo mdogo hupata maumivu makali anapokuwa na njaa na hupata nafuu pindi anapokula.

Dalili zingine ni pamoja na kutapika damu, kupata choo chenye rangi nyeusi, kukosa hamu ya kula na uzito wa mwili kupungua.

Endapo utapata dalili na viashiria hivi ni vizuri kufika mapema katika huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi, ushauri na matibabu.

Yapi ya kuepuka

Epuka uvutaji wa sigara, wapo baadhi ya wafungaji huwa na tabia ya kuvuta sigara mara tu baada ya kufungua hali hii huchochea kuongezeka kwa tindikali ya tumboni.

Epuka kula vyakula vyenye viungo vingi au pilipili nyingi, epuka au kunywa chai kwa kiasi na vyakula vyenye mafuta mengi.

Tumia maji kwa wingi epuka juisi zenye uchachu mkali, wakati wa kufungua kula mlo mwepesi kwa kiasi kwani unapofungua na kula mlo mkubwa kwa ghafla husababisha uchokozi na tindikali kuzalishwa kwa wingi.

Epuka vinywaji vyenye caffeine kama vile soda na kahawa, endapo utashindwa basi tumia kwa kiasi.

Usitumie dawa yoyote ya maumivu pasipo ushauri wa daktari, kwani dawa kama aspirini zinaweza kusababisha uchokozi wa kuzalishwa tindikali tumboni.

Imani ya Kislaam inaonyesha kuwa mtu mgonjwa halazimishwi kufunga, ni vizuri kama una matatizo ya kiafya kuwa shirikisha viongozi wako wa dini ili wakuelimishe au kukushauri kuhusiana na kufunga.

NINI MAANA YA SAUMU?

Katika Uislamu kufunga (saumu) ni kujizuilia kula, kunywa, kuvuta sigara, kuingiza kitu chochote katika matundu mengine mawili kama vile pua na masikio, kujizuia na kujamiiana, kujitoa manii kwa makusudi au kwa matamanio na kujizuia kujitapisha kwa ajili ya Mungu kwa kipindi cha kati ya alfajiri ya kweli mpaka kuingia magharibi. Hii ndio maana ya nje ya saumu katika Uislamu.

Kufunga katika Uislamu kuna maana ya ndani zaidi, ambayo kama haikufikiwa, kuzuilia kufanya vitendo hivyo vilivyoelezwa hakutakuwa na maana yoyote kwa mfungaji.

Kufunga kwa maana ya ndani ni pamoja kujizuilia kutenda maovu yote yaliyokatazwa na Mungu.

Ili saumu ya mfungaji iwe na maana na yenye kufikia lengo, hana budi kukizuilia (kukifungisha) kila kiungo chake cha mwili - macho, ulimi, masikio, mikono na miguu- pamoja na fikra na hisia zake na matendo aliyokataza Mungu.

Funga ya macho ni kujizuilia na kuangalia aliyoyakataza Mungu, Funga ya ulimi ni kujizuilia na mazungumzo yote aliyoyakataza Mungu kama vile kusengenya, kusema uwongo, kugombana na kadhalika.

Funga ya masikio ni kujizuia kufanya yale yote aliyoyaharamisha Mungu pia funga ya miguu ni kujizuilia na kuendea yale yote aliyoyakataza Mungu.

Na funga ya fikra na hisia ni kujizuia na fikra na dhana mbaya ambazo zinampelekea kuvunja amri na makatazo ya Mungu.

Funga ni ibada maalum iliyo muhimu sana katika kumuandaa mja kuwa mcha Mungu kwa kule kukataa kwake matamanio ya kimwili.

Hivyo Allah kwa ukaribu wake ameahidi malipo makubwa kwa wenye kutekeleza ibada hii ili iwe motisha kwao ya kuwawezesha kutekeleza ibada hii kwa hima kubwa na kwa ukamilifu unaotakikana.