Matokeo kidato cha sita na kurudi kwa hadhi ya shule za Serikali

Muktasari:

Katika matokeo hayo, shule za wanafunzi wa vipaji maalumu nne na moja ya kawaida, zilitajwa kuwa katika orodha ya shule bora 10 kitaifa.

Matokeo ya kidato cha sita yaliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) yameonyesha kuzirejesha shule za Serikali kwenye chati ya shule zenye ufaulu mzuri.

Katika matokeo hayo, shule za wanafunzi wa vipaji maalumu nne na moja ya kawaida, zilitajwa kuwa katika orodha ya shule bora 10 kitaifa.

Ni matokeo yaliyoleta ahueni hasa kwa kuwa kwa kipindi cha miaka kadhaa, shule hizo zilishindwa kufua dafu mbele ya shule binafsi.

Shule 10 zilizofanya vizuri ni Kisimiri ya Arusha, Feza Boys ya Dar es Salaam, Alliance Girls ya Mwanza, Feza Girls ya Dar es Salaam na Marian Boys ya Pwani.

Nyingine ambazo ni za Serikali ni Tabora Boys ya Tabora, Kibaha ya Pwani, Mzumbe ya Morogoro, Ilboru ya Arusha na Tandahimba ya Mtwara.

Hata hivyo, kijumla matokeo hayo yameonyesha kuwa ufaulu umeshuka kwa asilimia 0.93 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambao ufaulu ulikuwa asilimia 98.87. Matokeo hayo pia yanaonyesha wanaume wameongoza kwa wingi katika 10 bora.

Ni matokeo yaliyotarajiwa

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi, George Simbachawene anasema matokeo hayo ni matunda ya Serikali kufanya maboresho mbalimbali kwenye sekta ya elimu.

Aidha, anasema hali hiyo imechangiwa na mwamko wa elimu wa wadau mbalimbali waliokuwa wakitoa maoni yao juu ya kuboresha elimu na Serikali ikayafanyia kazi, huku pia akiahidi kuwapo kwa mabadiliko makubwa miaka miwili ijayo.

Wadau wanasemaje?

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (Duce), Dk Luka Mkonongwa anasema kuna sababu mchanganyiko zikiwamo juhudi binafsi za wazazi na wanafunzi.

“Imekuwa ni mshangao kwa sababu kwa muda mrefu shule zile kongwe zilianza kuanguka kwenye ufaulu, lakini sasa tunafurahi zinapanda. Inawezekana ni kutokana na programu mbalimbali zilizoanzishwa na Serikali.

Kwa mfano, hivi karibuni kulikuwa na program ya jinsi ya kufundisha masomo ya sayansi,” anasema Dk Mkonongwa ambaye hata hivyo, anasema shule hizo zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu.

“Shule nyingi za Serikali hazina walimu wa kutosha, kwa hiyo wanafunzi wanatafuta masomo ya ziada. Hizo ni juhudi binafsi za wazazi, lakini shule ndiyo zinapata sifa. Kwa mfano, Shule ya Sekondari ya Tabora haina walimu wa sayansi, hata Mzumbe hakuna walimu wa kutosha.”

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch anasema pamoja na madai ya muda mrefu ya walimu na uchache wa vifaa vya kufundishia, bado wameendelea kufundisha kwa bidii.

“Siku zote walimu wamekuwa wakilalamikia masilahi lakini hawaachi kufundisha, tena wanafundisha kwa bidii, hilo la kwanza.

Halafu hizi shule za Serikali baadhi yake zimejengwa kwa viwango vizuri vya kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri.

“Kwa mfano shule ya sekondari Kismiri, imejengwa na nchi ya Uswisi na imekuwa ikichukua watoto waliofaulu vizuri, hivyo hata kama walimu hawatoshi, bado wanafunzi wanapata moyo wa kujifunza zaidi,” anaeleza.

Anaendelea kutaja mfumo mpya wa utumishi unaoongeza masilahi kwa kuangalia uwajibikaji, akisema umewafanya walimu kuwa na bidii katika ufundishaji kwa mategemeo ya kupewa motisha.

“Walimu wanajipa moyo kwamba ipo siku mwajiri atawakumbuka kutokana na utendaji wao.

Hata sisi chama cha walimu tumekuwa tukiwatia moyo ili waione kazi ya ualimu kuwa ni nzuri.”

Doa la Sekondari ya Azania

Pamoja na shule hizo kongwe kuitoa Serikali kimasomaso, bado kwa upande mwingine imepata pigo la mwaka baada ya shule ya Sekondari ya Azania ya jijini Dar es Salaam kutajwa kuwa miongoni mwa shule 10 zilizofanya vibaya.

Kilichoshangaza wengi ni hadhi ya shule hiyo na hata umaarufu wake kitaaluma tangu ianzishwe mwaka 1934.

Katika matokeo hayo, wahitimu 29 wa shule hiyo walipata daraja sifuri, huku 11 wakipata daraja la kwanza. Waliopata daraja la pili ni wanafunzi 33, la tatu 115, na la nne wanafunzi 36.

Shule nyingine katika orodha hiyo ni Mpendae, Ben Bella, Tumekuja, Jang’ombe, Kiembesamaki, Al Ihsan Girls, Lumumba (zote za Unguja). Pia zimo Green Bird Boys (Kilimanjaro), Tanzania Adventist (Arusha).

Akizungumzia kufeli kwa shule hii na nyinginezo za Serikali, Olouch anasema hali hiyo inatokana na shule hizo kuwa na wanafunzi wengi kuliko uwezo wa kuwahudumia.

“Shule nyingi za mijini zina watoto wengi kuliko uwezo wake. Shule kama Azania, Tambaza, Kibasila zina watoto wengi kuliko uwezo wa walimu na vifaa ndiyo maana hazifanyi vizuri. Lakini shule za bweni zinafanya vizuri kwa sababu kule huwezi kupeleka watoto wengi bila kujali idadi ya vitanda na uwezo wa shule husika,” anasema Oluoch.

Bila shaka ufaulu kwa shule za sekondari za Serikali unapaswa kuangaliwa kwa umakini, usije ukawa ni wa bahati nasibu. Serikali ambaye ndiye mmiliki inapaswa kusikiliza kilio cha muda mrefu cha madai ya walimu na kuwekeza zaidi kwenye miundombinu ya elimu ili kuziinua zaidi shule zake kulinganisha na shule za binafsi.