Matokeo sera ya uchumi wa viwanda ni madogo kuliko ilivyotarajiwa

Muktasari:

  • “Kwa dhamira aliyonayo Rais (John) Magufuli, sasa hivi tulitakiwa tuwe tunazalisha baadhi ya bidhaa badala ya kuendelea kuagiza kutoka nje,” anasema Minja.

Baada ya miaka miwili ya kuinadi sera ya uchumi wa viwanda, aliyekuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Johnson Minja anasema matokeo yanayoonekana ni madogo kuliko ilivyotarajiwa.

“Kwa dhamira aliyonayo Rais (John) Magufuli, sasa hivi tulitakiwa tuwe tunazalisha baadhi ya bidhaa badala ya kuendelea kuagiza kutoka nje,” anasema Minja.

 Minja alisema hayo kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili na kubainisha masikitiko yake kuona bado tunaagiza mafuta ya kula wakati wao wanakuja kununua alzeti kwetu au kuagiza ‘toothpicks’ (vijiti vya meno) ilhali tunauza magogo.

Kwa maoni yake, anasema Rais Magufuli ana nia ya dhati ya kubadili uchumi wa Tanzania lakini kuna changamoto kwa wasaidizi wake ambao anasema bado hawajamuelewa hivyo kutototekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa kufanikisha ndoto hiyo.

Anasema hilo linajidhihirisha kwenye taasisi nyingi zinazoendeleza ukiritimba na kufanya mazingira ya biashara kutokuwa rafiki kama inavyobainishwa na ripoti za kimataifa mfano ile ya Benki ya Dunia; easy of doing business.

“Hali ya biashara kwa ujumla ni mbaya, hakuna mzunguko wa fedha. Tunaona benki zinafungwa na maduka hayauzi,” alisema Minja na kuongeza:

“Sioni msisitizo nilioutarajia kwenye ajenda ya viwanda badala yake imekuwa ni siasa tu hata vyerehani vine eti ni kiwanda licha ya kwamba havina mchango katika kujenga uchumi wa nchi.”

Maboresho

Minja, mshauri wa masuala ya biashara na kodi, anasema  mzunguko wa fedha umekuwa mdogo hivyo kuhitaji mkakati utakaorahisisha ufanyaji biashara.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa JWT ambaye alisaidia kwa kuiasisi jumuiya hiyo anasema ugumu huo wa uchumi upo maeneo mengi duniani na kila taifa linajipanga kulingana na changamoto ilizonazo.

“Watanzania tunapaswa kutumia rasilimali zetu vizuri kukidhi mahitaji yetu na si kuendelea kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi. Serikali iliangalie hilo,” anasema Minja, baba wa watoto wawili.

Anasema anasikitika kuona watu wanaagiza vitu vinavyoweza kutengenezwa nchini kutoka nje ya nchi kwa fedha za kigeni ambazo zingetumika kununua bidhaa ambazo hatuna uwezo wa kuzitengeneza akitoa mfano wa ndege, treni au meli.

“Serikali iangalie nini kinatumika katika kuzalisha vitu vingi zaidi viwandani mfano mitambo na mashine na iweke wepesi wa upatikanaji wake. Ajenda ya viwanda inatakiwa kuchukuliwa kwa msisitizo mkubwa,” anasema.

Kero

Mabadiliko yaliyoanza kutekelezwa Julai mwaka jana baada ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 kuanza kutumika, anasema yameongeza kero kwa wafanyabiashara.

Kwenye mabadiliko hayo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilipewa jukumu la kukusanya kodi ya majengo nchi nzima ambayo awali ilikuwa inakusanywa na halmashauri husika.

Kutokana na hilo, halmashauri zimelazimika kutafuta vyanzo vingine vya mapato ili ziweze kujiendesha. Kwenye ubunifu wa too mpya uliofanywa na halmashauri, Minja anasema umeongeza kero kwa wafanyabiashara.

“Naunga mkono TRA kukusanya kodi ya majengo. Wao wana utaalamu mkubwa kwenye ukusanyaji mapato ila kosa lililopo, fedha hizo hazirudishwi halmashauri hivyo kuzipa changamoto ya kufanikisha mipango ilizojiwekea,” anasema.

Kutokana na ukosefu wa fedha, anasema halmashauri zimeanza kuchukua tozo ya huduma ambayo ni asilimia 0.3 ya mauzo ghafi jambo ambalo ni kinyume na inavyotakiwa kuwa.

Anasema tozo hiyo inakiuka baadhi ya kanuni za kodi zinazotaka iwe rahisi kukusanywa kwani kwani kinyume chake inakuwa haifai na inapaswa kufutwa mara moja.

Kwa utaratibu uliopo, anasema mfanyabiashara wa duka anakuwa amelipia gharama za leseni ambayo hutolewa na halmashauri, mabango na kodi ya pango inayokusanywa na TRA lakini bado anaongezewa mzigo.

“Kanuni zinataka kodi itozwe kwenye faida, baada ya kuondoa gharama zote za uendeshaji lakini tozo hii imeelekezwa kwenye mauzo. Halmashauri hazijali umeuza kwa hasara ama la, zinataka asilimia 0.3 ya kila ulichouza. Hii ni kero na haikubliki,” anasema Minja.

Zamani, anasema tozo hiyo ilikuwa inalipw ana kampuni kubwa zenye shughuli zinazoathiri mazingira ghafla hazijahamishiwa kwa wafanyabiashara wenye maduka.

Licha ya tozo hiyo, Minja anasema watendaji wengi wa Serikali na jamii kwa ujumla bado wana mazoea ya uchumi wa kijamaa ama hawaupendi au hawaukubali uchumi wa soko hivyo kusababisha kero zinazoepukika.

Anatoa mfano: “Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wanapita kwenye maduka kukagua na kutoza faini wafanyabiashara ambao hawajatekeleza masharti ya jeshi hilo. Haya mambo hayakubaliki.”

Anafafanua kuwa ni muhimu kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara kwa Watanzania ili kubadilisha maisha ya wafugaji na wakulima, kwa kuwa hawatokosa soko la mazao yao endapo wafanyabiashara watawekeza kwenye viwanda vya usindikaji.

JWT

Zamani, Minja anasaema kulikuwa na Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK) ambayo ilikuwa inashughulikia kero zao kabla ya kufanya maboresho kadhaa miaka minane iliyopita.

Minja anakumbuka ilivyokuwa. Anasema kuna wakati TRA ilitaka wafanyabiashara wote wa Kariakoo wasajiliwe kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) tofauti na sheria inayotaka wenye mauzo yanayozidi Sh40 milioni kwa mwaka.

Wafanyabiashara hao hawakukubali utaratibu huo uliopendekezwa na TRA hivyo wakalazimika kwend akumuona Waziri Mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda ambaye baada ya kusikiliza hoja zao akasema hilo lilikuwa suala la kitaifa hivyo liwasilishwe kwa sura hiyo.

Ilikuwa mwaka 2010 walipoenda kumuona Pinda na wakaanza mchakato wa kuisajili Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania naye akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa kwanza.

Baada ya kufanya uhamasishaji nchi nzima, anasema jumuiya ilianzishwa mwaka 2012 hivyo kuwasilisha kero au malalamiko ya wafanyabiashara nchi nzima.

“Ilikuwa ni lazima maduka maduka yafungwe kila kulipokuwa na malalamiko ya wafanyabiashara. Nafurahi sasa hivi kuona hakuna maandamano tena. Serikali inakaa meza moja na wafanyabiashara kushughulikia kero zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi,” anasema.

Haikuwa rahisi kufika hapo na Minja anakumbukwa kwa migomo ya wafanyabiashara wenye maduka aliyoiendesha akiwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo enzi za Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

Mara kadhaa alikamatwa, kuwekwa mahabusu na kufunguliwa kesi kutokana na kukithiri kwa migomo ya wafanyabiashara iliyokuwa inafanyika maeneo tofauti nchini.

Migomo hiyo ilishamiri zaidi kati ya mwaka 2014/15 kwa wafanyabiashara kufunga maduka yao wakimtaka Rais Kikwete kuyafanyia kazi malalamiko yao. Miongoni mwa walivyolalamikia ilikuwa bei kubwa ya Mashine za za Risiti za Kielektroniki (EFD).

Wakati huo, ilishuhudiwa, wafanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam na mikoa ya Dodoma, Mbeya, Mara, Mwanza na Tanga wakigoma kufungua maduka yao kushinikiza kusimamishwa kwa matumizi ya mashine hizo.

Anasema umuhimu wa jumuiya hiyo unajidhihirisha kwenye mambo mengi. Kwanza, wamekuwa familia moja baada ya kuwa na chombo cha kuwasemea na kupitia semina mbalimbali zinazoandaliwa nayo, wanafundishwa mambo muhimu hasa kuhusu kodi.

Kutokana na semina ambazo JWT imeziandaa kwa kushirikiana na TRA pamoja na wataalamu wengine wa biashara na kodi, Minja anasema uelewa wa wafanyabiashara umeongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Tumepanua wigo wa walipakodi,” anasema.

JWT na siasa

Kwa miaka minane aliyoiongoza jumuiya, anasema changamoto kubwa ilikuwa kukataa ushawishi wa kisiasa uliokuwa unataka uungaji mkono ama wa chama au mgombea hasa wa Urais.

Ilikuwa changamoto kwa kuwa, anasema, usipokuwa makini ni rahisi kutanguliza masilahi binafsi badala ya hoja za wafanyabiashara waliokuamini kwanza.

“Kipindi cha kampeni nilipokea simu nyingi za kushawishi jumuiya umuunge mtu au chama fulani. Sikufanya hivyo kwa kutambua wapo watu walioniweka nilipokuwa,” anakumbuka.

JWT na TPSF

Wakati wafanyabiashara wakiunganishwa na jumuiya hiyo, bado si sehemu ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF). Ni kama hawaongei lugha moja.

Minja anasema zipo tofauti za asili kati ya vyombo hivyo viwili ingawa ukiwapo ushirikiano miongoni mwao kutaongeza tija kwa makundi yote mawili.

Anabainisha kuwa, JWT inaundwa na wafanyabiashara wadogo ambao ni masikini tofauti na wanachama wa TPSF ambao mitaji na soko lao ni kubwa.

“Kila mmoja ana masilahi yake. Hakuna anayetaka kutumika kwa mwenzake. Lakini TPSF na JWT wakiheshimiana, mchango wao utakuwa mkubwa zaidi nchini ila wanatakiwa kuheshimiana,” anasema Minja.