NUSU MWAKA: Matukio yaliyobamba katika tasnia ya burudani

Muktasari:

Huu ni mwaka wa mafanikio kwa wasanii hapa nchini baada ya wengi wao kuanzisha lebo za muziki zilizoingia mkataba na wasanii kadhaa.

Imebaki miezi mitano na siku 28 mwaka 2016 umalizike. Katika kipindi cha miezi sita na siku mbili matukio mengi yametokea katika burudani nchini. Wakati unaianza nusu ya pili ya mwaka, jikumbushe matukio makubwa ambayo yaliteka vichwa vya habari nchini kote.

Lebo za wasanii

Huu ni mwaka wa mafanikio kwa wasanii hapa nchini baada ya wengi wao kuanzisha lebo za muziki zilizoingia mkataba na wasanii kadhaa.

Awali wasanii wengi walijikabidhi kwa watu walioitwa ‘mameneja’ lakini mwanzo wa 2016 kumekuwa na mfumo mpya ambao wasanii wameanzisha lebo zao kwamba wasanii sasa watasimamiwa na kampuni.

Kampuni ya Wasafi Classic Baby (WCB) inasimamia wasanii zaidi ya wanne wakiwamo Harmonize, Rich Mavoko, Queen Darling na Raymond.

Poz Kwa Poz (PKP) nayo imeonyesha kwamba ina uwezo wa kufanya kazi na kuingia mkataba wa kumsimamia mwanamuziki chipukizi, Nerdy Music.

Mirabaha

Kupitia kampuni ya Copyrights Management East Africa Limited (CMEA) wasanii walianza kukadiriwa malipo yao kutokana na kazi zao zinavyochezwa katika runinga na redio, lakini mafanikio zaidi kuhusu utaratibu huo wasanii wanasema bado hawajaanza kunufaika. Kikubwa kampuni hii imewasaidia wasanii kujua wimbo gani unapigwa zaidi Afrika Mashariki , hivyo kujua nafasi zao ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Chura wa Snura

Katika mambo ambayo yalitikisa tasnia ya burudani nchini ni video ya mwanadada Snura Mushi ambayo ilitayarishwa nchini na mtayarishaji Pablo.Video hiyo iliyoishi kwa siku zisizozidi tano katika mtandao wa YouTube ilipigwa marufuku na Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Licha ya kuifuta katika mitandao ya kijamii, Snura aliambiwa atengeneze video nyingine ili kufuta maudhui ya video ya awali zoezi ambalo limezimwa kimya kimya.

Wasanii kujitoa kwa jamii

Ni mwaka ulioonyesha mafanikio makubwa zaidi baada ya mastaa kujitoa kwa jamii katika mambo mbalimbali. Wapo wasanii ambao wametumia kumbukumbu zao za kuzaliwa kula chakula na watoto yatima, kutoa vifaa mbalimbali vya msaada mashuleni na kwingineko.

Diamond Platnumz alitoa msaada wa madawati 600 kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda yenye thamani ya Sh48 milioni.

Kili Music Awards

Katika matukio ambayo yamewasononesha wasanii mwaka huu ni ukimya kuhusu uwapo wa tuzo za muziki Kili Music Awards.

Kilimanjaro Music Awards’ni tuzo zilizoanzishwa nchini na kufanyika kwa kipindi cha miaka 22 mfululizo na hivyo kuwajengea wasanii utamaduni wa kuenzi kazi zao.

Uwapo wa tuzo hizo uliwawezesha wasanii kutengeneza kazi zenye ubora, tija na zenye kuleta hamasa, huku wakijitahidi kutengeneza kazi zenye ubora.

Ikilinganishwa na miaka ya nyuma, mwaka jana wasanii walifanya kazi nzuri zaidi huku wakiangalia uwezekano wa wao kushindana zaidi katika tuzo hizo.

Wengi wao walijitahidi kufanya video na watayarishaji wa kimataifa na hata waliofanya ndani kazi zilikuwa zenye viwango.

Alikiba kuingia Sony

Kati ya mambo ambayo yameufanya mwaka 2016 kuwa wenye utofauti ni baadhi ya wasanii kujikuta wakitua katika mikono salama ikiwamo mwanamuziki Ali Kiba kusaini mkataba na kampuni kubwa duniani ya Sony Music.

Kampuni hiyo sasa itasimamia kazi za mwanamuzi huyo ikiwamo kumtafutia shoo na soko la nyimbo zake.

Tandale to The Wolrd Tour

Kila mwaka mwanamuziki Diamond Platnumz anazidi kupanda hatua moja. Nusu ya mwaka huu amefanikiwa kufanya mengi ikiwamo kuongeza idadi ya wasanii katika lebo yake, kushirikiana na wasanii wa kimataifa wakiwamo mapacha kutoka Nigeria, P Square.

Mwaka huu Diamond amefanikiwa kufanya ziara katika bara la Ulaya iliyotambulika kama ‘Tandale to The Wolrd Tour’ iliyomwezesha kufanya shoo nyingi Ulaya kwa kipindi cha mwezi mmoja ziara iliyozidi kutunisha mifuko yake.