Matumizi ya Kiswahili katika nyanja mbalimbali nchini

Muktasari:

Kwa mfano mwaka 1974 Makamu wa Pili wa Rais na Waziri Mkuu wa zamani, Mzee Kawawa aliwahi kutoa waraka uliosisitiza umuhimu wa kutumia Kiswahili katika shughuli zote za Serikali. Shuguli hizi ni kwenye mikutano, mawasiliano kwa simu na barua.

Lugha ya Kiswahili ni lugha ya taifa na lugha rasmi nchini Tanzania. Hii imetokana na maagizo ya viongozi wakuu wa nchi waliokuwa na uzalendo na mapenzi makuu wa nchi yetu kama Mwalimu Julius Nyerere na Rashid Mfaume Kawawa.

Kwa mfano mwaka 1974 Makamu wa Pili wa Rais na Waziri Mkuu wa zamani, Mzee Kawawa aliwahi kutoa waraka uliosisitiza umuhimu wa kutumia Kiswahili katika shughuli zote za Serikali. Shuguli hizi ni kwenye mikutano, mawasiliano kwa simu na barua.

Pia, ni lugha rasmi ya kufundishia katika shule za msingi na vyuo vya mafunzo ya ualimu. Juhudi mbalimbali zimefanywa na taasisi na asasi mbalimbali ili kutekeleza azma hii.

Kwa mfano, Baraza la Kiswahili la Taifa lilianza kusanifu istilahi za taaluma mbalimbali kama Kemia, Fizikia, Biolojia, Jiografia, Historia, Uraia, Saikatria, Uchumi na Biashara, Utawala na Wendeshaji wa Ofisi. Lengo ni kuhakikisha kuwa Kiswahili kinaweza kutumika kama lugha ya kufundishia. Kwa mfano kuandika vitabu vya kiada na ziada kwa Kiswahili kwa shule za msingi na sekondari.

Juhudi za kuandika kamusi zenye misamiati ya Kiswahili/Kiingereza, Kiswahili/Kiswahili na Kiingereza/Kiswahili nazo zimetia fora na kumezaa matunda yanayoonekana. Vilevile, viko vijitabu vya istilahi za Kiswahili kwa taaluma mbalimbali kama siasa, uchumi, biashara, kemia, fizikia, biolojia, utawala, uongozi, tiba kwa mfano ugonjwa wa saikatria.

Baraza la Kiswahili la Taifa limesanifu istilahi hizi kwa kushirikiana na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Wizara ya Elimu na wadau wengine wa Kiswahili.

Kwa hali iliyopo sasa hapa nchini hatuna sababu ya kusema kuwa Kiswahili ni lugha duni kwani ni miongoni mwa lugha zinazokua kwa kasi kubwa katika bara la Afrika.

Hivi sasa Kiswahili kina uwezo mkubwa wa kutumika katika nyanja za elimu, uchumi, biashara, mawasiliano, afya na siasa. Jambo linalotakiwa kufanywa ni kuwepo kwa sera thabiti, sheria na Katiba Mpya inayotamka wazi nafasi ya lugha ya Kiswahili.

Katika sekta ya elimu, tayari sera ipo. Hii ni Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inayotaja wazi nafasi ya Kiswahili katika mfumo mzima wa elimu.

Baada ya sera hii kutolewa, kinachotakiwa kufanyika ni kuandaa mipango thabiti ya utekelezaji ambayo itazingatia mambo yafuatayo:

Kwanza ni upatikanaji wa vitabu. Vitabu vinaweza kupatikana kwa kuwahimiza wataalamu kuandika. Kwa kuwa kuna msamiati na istilahi za kutosha na kwa kuwa Bakita wanaedelea kusanifu istilahi za masomo mbalimbali, pawepo na ushirikiano kati ya Bakita na waandishi wa vitabu na majarida na Taasisi ya Elimu wanaotayarisha miongozo ya mada za kufundishia.

Jambo la msingi ni kuandika vitabu na majarida kwa kufuata mpangilio maalumu wa kuanzia madarasa ya chini na kuelekea juu. Pia, kuanza na masomo ya sanaa na kuendelea na masomo ya sayansi na hisabati. Kwa mfano kuanza masomo ya historia, jiografia, uraia na baadaye hisabati, biolojia, kemia na fizikia.

Mbali na vitabu, eneo jingine muhimu ni kuwa na walimu wa kutosha. Tunao walimu wa kutosha na tutaendelea kuongeza idadi yao kulingana na ongezeko la usajili wa wanafunzi mwaka hadi mwaka.

Walimu waliopo kazini wataelimishwa na kunolewa kwenye semina na warsha kutokana na mada mpya zilizoongezwa kulingana na mabadiliko ya mitalaa. Nao walimu tarajali watasomeshwa kulingana na mitalaa kutoka Taasisi ya Elimu.

Wakaguzi na wakufunzi wa vyuo nao waelimishwe ili waende na wakati. Kutakuwapo na kipindi cha hekaheka za kusoma kwa jamii nzima ya wizara ya elimu kuanzai na walimu walio kazini, wakufunzi, wakaguzi na walimu tarajali.

Njia ya tatu ni kutafsiri vitabu na makala za kitaaluma kama ilivyo katika uandishi wa vitabu. Wafasiri nao wanatakiwa kutumia misamiati na istilahi za masomo mbalimbali.

Ni jambo muhimu kufuata taratibu zote za kutafsiri mara inapoamuliwa aina ya vitabu vya kutafsiriwa. Kwa mfano ni lazima kupata kibali cha mchapishaji ambaye naye atawasiliana na mwandishi wa kitabu.

Wako baadhi ya wachapishaji wanaotaka kujua idadi ya machapisho na pia bei ya kila nakala ya kitabu.

Kwa lugha nyepesi ni kwamba bado kuna fikra potofu kwa viongozi wengi katika Serikali na mashirika ya umma wenye kasumba vichwani mwao kuwa lugha ya Kiswahili hakijafikia hadhi ya kweza kutumika kueleza dhana elimu, sayansi na teknolojia.

Stephen Maina ni mdau wa Kiswahili, anapatikana kwa baruapepe: [email protected] na simu namba 0754861664