Maumivu ya bao la dakika za majeruhi

Muktasari:

Pia, kilio hutokea timu ikitolewa kwa matuta baada ya kukaza dakika 120 ama 90. Ni kawaida baadhi ya wachezaji kama si wote, waliopoteza mchezo, huangua kilio uwanjani.

Inapopulizwa filimbi ya kumaliza mpira iwe dakika 90+ za majeruhi, hapa ndipo vilio hutawala uwanjani na zaidi ni baada ya timu kufungwa bao dakika ya 90 au dakika za mwisho kufikia 120.

Pia, kilio hutokea timu ikitolewa kwa matuta baada ya kukaza dakika 120 ama 90. Ni kawaida baadhi ya wachezaji kama si wote, waliopoteza mchezo, huangua kilio uwanjani.

Utaona tu mchezaji anashika uso, mwingine anachuchumaa akijiinamia, mwingine atavuta jezi kujifunika sura akilia na wengine kulia waziwazi.

Ni baadhi tu ya wachezaji hubakia na majonzi moyoni na wakati mwingine huwasaidia wenzao na wao wakibakia kububujikwa machozi, yote ni kutokana na kupoteza mchezo dakika za lala salama na zaidi ni kutokana na timu kucheza kwa matarajio chanya na matokeo kuwa hasi.

Mara kadhaa, timu za Tanzania zimekuwa zikishindwa kuhimili dakika sita za majeruhi, dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho au dakika tatu za nyongeza na kufungwa mabao ya kusononesha ambayo ama yanaitupa timu nje ya mashindano au kuharibiwa nafasi ya kusonga mbele ilhali wapinzani hawana cha kupoteza au wanasonga mbele.

Hili ni tatizo kwa wachezaji wa Tanzania iwe kwenye timu ya taifa au klabu. Zifuatazo ni baadhi ya mechi ambazo timu za Tanzania zilishindwa kuhimili dakika za majeruhi na kukubali kuharibiwa siku kwa kufungwa mabao ya kusononesha kiasi cha ama kuitoa timu katika mashindano ama kukwazwa kusonga mbele.

 

Ngorongoro v Somalia, Agosti 19, 2005

Timu ya vijana ya Somalia ya U-20 iliwafunga wenzao wa Tanzania Bara, Ngorongoro Heroes mabao 2-1 mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Amaan.

Ngorongoro Heroes, ilikuwa ya kwanza kufunga kwa mkwaju wa penalti baada ya mabeki wa Somalia kumuangusha Julius Mrope ndani ya eneo la hatari. Amir Maftah alifunga penalti dakika ya 25.

Kipindi cha pili Somalia ilisawazisha dakika ya 63 kupitia kwa Abdirahman Othman kabla ya kufunga la pili dakika za majeruhi kupitia kwa Mohamed Nur. Mechi hiyo iliipoteza Ngorongoro na kushindwa kusonga mbele ya michuano hiyo Afrika Mashariki na Kati kwa vijana.

 

Taifa Stars vs Zambia, Feb 28, 2009

Mwaka 2009, Taifa Stars ilifuzu fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN). Ikipangwa kwenye Kundi A na ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na Senegal, lakini ikawalaza wenyeji Ivory Coast kwa bao 1-0.

Mchezo wa mwisho wa makundi ulikuwa dhidi ya Zambia ambao Stars ilitakiwa kupata ushindi wa aina yoyote ili iweze kuingia nusu fainali.

Licha ya Mrisho Ngassa kufunga dakika ya 88 ya mchezo, Stars iliruhusu bao la kusawazisha la Zambia katika dakika ya 90+4 ambalo lilihitimisha ndoto ya Taifa Stars kucheza hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza.

Taifa Stars ilimaliza ikiwa na pointi nne huku Senegal na Zambia zikifuzu kutokana na pointi zao tano kila moja. .

 

Simba v Wydad Casablanca, Mei 28, 2011

Licha ya kutolewa kwa jumla ya mabao 6-3 na TP Mazembe ya Congo DR, Simba ilibahatika kushinda rufani yao waliyoikata CAF dhidi ya TP Mazembe ambayo ilimtumia Besala Bokungu isivyo halali. Bokungu kwa sasa anakipiga katika klabu hiyo ya Msimbazi.

CAF iliamua Simba icheze na Wydad Casablanca ambayo nayo ilitolewa na Mazembe kwenye raundi ya pili ili kupata timu itakayofuzu hatua ya makundi.

Mechi hiyo ilichezwa uwanja huru wa Petro Sport uliopo Cairo nchini Misri, Simba ilifungwa mabao 3-0.

Hata hivyo, licha ya kujituma kwa dakika 87 za mchezo huo huku matokeo yakisimama 0-0 na kila mmoja akiamini kuwa mchezo utaamriwa kwa mikwaju ya penati, Wydad ilifunga mabao matatu kwenye dakika za 88, 90+4 na 90+6 ambayo yalimaliza ndoto za Simba mapema kuwa mchezo ungeamriwa kwa mikwaju ya penalti kama wangecheza kwa umakini dakika zote.

 

Yanga v Al Ahly, Aprili 20, 2016

Baada ya matokeo ya sare ya 1-1 nyumbani, Yanga ilikwenda Cairo ikihitaji suluhu au ushindi wa aina yoyote ili kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.Katika mchezo huo wa marudiano, licha ya Al Ahly kutangulia kupata bao lililowekwa kimiani na Hossam Ghaly, Yanga ilipigana na kusawazisha dakika ya 67 kupitia kwa Donald Ngoma baada ya kuunganisha kwa kichwa, pande la Juma Abdul, matokeo ambayo yangeifanya mechi hiyo iamriwe kwa mikwaju ya penalti kama mabeki wangekuwa makini dakika zote 120.

Hata hivyo, Yanga ilishindwa kujitetea kwani ilisalia sekunde moja yaani dakika 119 na sekunde 59 baada ya mchezo kwenda dakika 120. Mshambuliaji wa Al Ahly, Abdallah El-Said aliipa timu yake bao la ushindi la kichwa na kuzima ndoto za Yanga kupambana kuingia hatua hiyo ya makundi.

Wadau mbalimbali wa soka wametoa maoni kuhusu mambo yanazosababisha wachezaji kushindwa kujipanga hata kuruhusu mabao kufungwa dakika za lala salama.

 

Serengeti Boys vs Congo, Okt 2, 2016

Wiki tatu zilizopita, timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys iliondolewa kwenye mashindano ya kuwania kufuzu fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika Antananarivo, Madagascar mwakani.

Ikiwa imebakiza hatua moja kabla ya kufuzu fainali hizo, Serengeti Boys ilitakiwa kubaki na matokeo ya 0-0 lakini ilikwaa kisiki mbele ya vijana wa Congo Brazzaville baada ya kutolewa kwa faida ya bao la ugenini la wapinzani wao baada ya matokeo ya jumla kuwa 3-3. Mchezo wa kwanza ulimalizika kwa Serengeti Boys kushinda mabao 3-2 katika mchezo wa kwanza.

Serengeti Boys iliyokuwa ikijiamini sasa imevuka baada ya ushindi wa mabao 3-2 nyumbani kwenye mechi ya kwanza, lakini ilichapwa bao 1-0 ugenini huko Congo.

Ingawa kuondolewa kwa Serengeti Boys kwenye mashindano hayo kumeacha majonzi kwa Watanzania, kinachoumiza zaidi ni kuwa bao lililoivusha Congo lilifungwa dakika ya pili ya muda wa nyongeza kati ya tatu zilizoongezwa baada ya muda wa kawaida kwisha.

Serengeti Boys iliyokuwa inahitaji suluhu tu kwenye mchezo huo isonge mbele, iliweza kumaliza salama kwenye dakika 90 za mchezo huo, lakini ikafia kwenye dakika tatu za nyongeza kwa kufungwa bao hilo.

 

Kauli za wadau

Kiungo wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Ally Yusuf ‘Tigana’ anataja sababu mbili, timu zetu kuruhusu mabao ya ‘usiku’ hasa katika mechi za kimataifa.

“Sababu ya kwanza ni kutojiamini, jambo linalochangia wachezaji wetu kujijengea mawazo kuwa ni lazima timu mwenyeji iibuke na ushindi pale inapocheza nyumbani na kujikuta wanacheza kwa hofu kubwa inayowatoa mchezoni.

Sababu ya pili ni kutokuwa makini na kujiamini kulikopitiliza kwa wachezaji wetu hali inayowapa mwanya wapinzani kujipanga na kupeleka mashambulizi ya mara kwa mara ambayo mwisho wa siku huzaa mabao,” anasema Tigana.

Beki wa zamani wa Yanga, Simba na Taifa Stars, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ anasema anaamini kuwa sababu kubwa ya timu zetu kuruhusu mabao mengi dakika za majeruhi ni wachezaji kutokuwa fiti.

“Wachezaji wetu wana uwezo wa kucheza dakika 45 tu za kwanza na wakijitahidi sana angalau wanakuwa na kasi na nguvu waliyoanza nayo mpaka dakika ya 60. Lazima tuwe wakweli, katika hilo na kuachana na hadithi za kuwa suala hilo linatokana na bahati mbaya.

“Baada ya dakika 45 na hadi dakika ya 60, nusu saa iliyobaki, mara nyingi pumzi na stamina huisha kwa sababu hawakufanya mazoezi magumu. Wachezaji wetu ni wavivu wa mazoe na hawapendi mazoezi magumu yanayotakiwa yafanyike kwa saa tatu.

Aliyewahi kuwa kocha mkuu wa Toto Africans, Mjerumani Martin Glerics anasema hali hiyo husababishwa na saikolojia ya wachezaji kuanza kujiamini mapema kuwa wameshinda au matokeo yanawabeba wakati mechi haijamalizika.

“Zinapofika dakika za majeruhi, wachezaji hujiaminisha kuwa mechi imeshaisha hivyo wanapoteza ule umakini waliokuwa nao kwa dakika nyingi za mechi sasa wanapokutana na timu pinzani yenye wachezaji wanaotambua wajibu wao uwanjani ni lazima ufungwe. “Ili kumaliza tatizo hilo ni lazima benchi la ufundi liwe na watu ambao watawajenga wachezaji kisaikolojia pale wanapokuwa wanahitaji matokeo ya aina fulani,” anasema Glerics.

Kiungo na nahodha wa Kagera Sugar, George Kavila anasema kinachofanya timu zetu kufungwa lala salama ni ukosefu wa mbinu sahihi za kujilinda kwa wachezaji na benchi la ufundi.

“Wenzetu wanafahamu nini kifanyike na kwa wakati gani na ndiyo maana unaona wanaweza kupata matokeo wanayoyahitaji tofauti na sisi. Dakika za mwisho zinahitaji kuwe na mbinu mbadala za kujilinda na hata kushambulia kwani ndizo zinakuwa na presha kubwa kuliko nyingine.

“Wenzetu muda kama huo, iwapo wanalinda bao, wanatumia ujanja wa kupoteza muda kama vile kipa kujifanya kaumia, kukaa sana na mpira kwa kupiga pasi nyingi zitakazofanya mpinzani ausake mpira na pia hata benchi la ufundi kufanya mabadiliko ya kuchelewesha muda. Hilo kwetu halipo na ndiyo maana hatufanikiwi.”

Kocha wa Serengeti Boys, Bakari Shime ambaye alipatwa na dhahama hiyo, Congo Brazzaville anasema tatizo hilo linaweza kusababishwa na kujiamini, bahati mbaya na wapinzani kubebwa.

“Mchezaji anaweza kuamini mechi imemalizika hivyo anapoteza ule umakini ambao alikuwa nao mwanzoni lakini wakati mwingine ni bahati.

“Kingine ni fitina za timu mwenyeji hasa kwa kubebwa na waamuzi kwa kupewa penalti au kuongezwa dakika nyingi kwa lengo la kuwatafutia bao. Suluhisho kubwa la hili ni kupata matokeo mazuri nyumbani ambayo yatakuwa na faida ugenini.”

Beki wa Taifa Stars na Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyekuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwamo kwenye kikosi cha Stars kilichoruhusu bao la dakika za jioni kwenye mchezo dhidi ya Zambia mwaka 2009 anasema wakati mwingine wanaponzwa na uchovu.

“Huwa inatokea mnachoka sana mwili na kisaikolojia baada ya kucheza kwa dakika nyingi, pia inaweza kuchangiwa na kujisahau tu na kuamini mechi imeisha.

“Kwa asilimia kubwa hilo linachangiwa na timu kutokukaa na kumiliki mpira ndani ya muda huo. Ni vigumu kujilinda pindi mpinzani anapokuwa na mpira,” anasema Cannavaro.

Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, raia wa Uganda anafafanua kuwa tatizo hilo linachangiwa na timu kutowaandaa wachezaji kisaikolojia na kiufundi.

“Mchezaji anatakiwa kufahamu kuwa dakika moja kwenye soka ni muhimu hivyo ni lazima atengenezewe mazingira ya kumfanya aone kuwa ushindi ni pale filimbi ya mwisho inapopulizwa.

“Pia, mchezaji anatakiwa apewe mbinu sahihi za kucheza kulingana na matokeo yanayohitajika kwenye mechi hiyo,” alisema Mayanja.

Kocha wa zamani wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ anasema tatizo hili linatokana na wachezaji wenyewe.

“Wachezaji wa Kitanzania wana kawaida ya kuridhika na kujisahau hasa pale wanapokuwa wanaongoza. Hiyo inafanya wapunguze kasi waliyoanza nayo na kuzipa nguvu timu pinzani,” anasema Julio.

Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, beki wa Simba anasema anaamini tatizo hilo hutokea kwa bahati mbaya na si kwa sababu ambazo wengi wamekuwa wakizitoa.

“ Hakuna mchezaji mwenye lengo la kuruhusu bao dakika za mwisho. Kinachotokea ni hali ya kawaida tu kwenye soka ambayo huwakuta hata wachezaji wa nchi zilizoendelea kisoka,” alisema beki huyo kipenzi wa Simba ambaye kwa nidhamu na soka yake iliifanya klabu imzawadie gari.