Mbegu za mafuta ni fursa ya uchumi wa viwanda

Muktasari:

Hili litawezekana ikiwa wakulima hasa wadogo watajengewa uwezo wa kuzalisha, kusindika na kuuza mafuta yatokayo na mbegu. Hii haimaanishi wakulima wanafanya kazi zote ila washirikiane na wadau wengine kwenye mnyororo wa thamani.

Tanzania ina fursa kubwa kunufaika na biashara ya mafuta ya kula endapo itaamua kuwa na mkakati mahususi wa kutokuuza mbegu za mafuta na badala yake kuziongezea thamani na kupata bidhaa kamili.

Hili litawezekana ikiwa wakulima hasa wadogo watajengewa uwezo wa kuzalisha, kusindika na kuuza mafuta yatokayo na mbegu. Hii haimaanishi wakulima wanafanya kazi zote ila washirikiane na wadau wengine kwenye mnyororo wa thamani.

Jambo muhimu ni kuhamasika kwa wakulima, wadau wengine, kuelewa na kukubali kutekeleza mkakati huo ambao utasimamiwa na kuendeshwa na wakulima wenyewe.

Ili mkakati huu ufanikiwe Serikali inatakiwa ifanye mapinduzi kwenye umiliki wa ardhi ili kila Mtanzania anayehitaji kulima awe na fursa hiyo. Wale wenye ardhi kubwa isiyotumika wanapaswa kuirudisha ili kutoa nafasi kwa wengine kuitumia.

Nia ni kuhakikisha Watanzania wengi wana fursa ya kuongeza kipato kutokana na kilimo ambacho kitachangia kuongezeka mzunguko wa fedha ambao ni muhimu kukua kwa uchumi.

Mkulima mdogo mwenye uwezo wa kuzalisha, kusindika na kuuza mafuta ya mbegu na bidhaa nyinginezo atashiriki kupanga bei badala ya kupangiwa.

Mfano ni msafiri anayetoka Mwanza kwenda Dar es Salaam kwa basi au gari binafsi anaweza kusimama Singida kununua mafuta ya alizeti. Ni wakati ambao atakubaliana bei na muuzaji ambaye ni mkulima ambaye anafahamu gharama za kuzalisha lita tano za mafuta au kiasi kingine chochote na faida atakayopata.

Mkulima atauza kwa faida anayoitaka na makubaliano yatakayofanyika yatakuwa ni kwa ridhaa yake. Atapata anachostahili kutokana na jasho lake. Kwa mfumo huu itakuwa nadra kwa mkulima kupata hasara sokoni endapo atakuwa amewekeza juhudi ya kutosha shambani.

Mfumo wa ongezeko la thamani ambao unaendeshwa na kusimamiwa na mkulima mdogo utamuwezesha mkulima kuajiri wasaidizi wa kulima, kuvuna, kusindika au kusambaza mafuta. Kwa kufanya hivi atakuwa amepunguza uhaba uliopo, umasikini na kukuza uchumi.

Kufanikisha hili, mkulima atahitaji msaada wa wataalamu wa masuala ya biashara watakaomuongoza kusimamia mapato yake na uendelevu wa shughuli zake bila kutetereka. Wanaweza kuwa wafanyabiashara wazoefu wa usambazaji wa bidhaa wanaopatikana kwenye eneo alilopo au washauri na wakufunzi wa ujasiriamali.

Minyororo tuliyoizoea inahamisha umiliki wa zao au bidhaa kila baada ya muuzaji na mnunuzi kulipana. Kwa hiyo kila faida inayopatikana baada ya hapo ni ya mnunuzi na mkulima hana masilahi.

Huwa inatokea mkulima anauza mazao yake yakiwa shambani kutokana na tatizo alilonalo kwa wakati fulani hivyo kuhamisha umiliki wa mazao hayo kwa mnunuzi ambaye huneemeka na faida itakayopatikana licha ya juhudi za mkulima kulitunza shamba hilo.

Tanzania inaweza ikajitegemea kwa kuzalisha mafuta ya kula ya kutosha kutokana na alizeti, mawese au pamba na kutimiza adhima ya kuwa na nchi ya viwanda. Mazao haya yanalimwa sehemu nyingi nchini hivyo kutoa mwanya wa kukuza pato la taifa na ajira hasa vijijini. Kwa kushirikiana na wadau wengine, Serikali inatakiwa kuwasaidia wakulima hawa kutumia rasilimali hizo vizuri ili kukuza pato la familia kutoka maeneo wanayoendeshea shughuli zao bila kuacha athari za kimazingira.

Hili likifanyika kilimo kitastawi, maradhi yatapungua vijijini kutokana na lishe bora itakayochangiwa na kipato cha uhakika huku idadi ya vijana wanaokimbilia mjini ikipungua baada ya uhakika wa ajira vijijini.