MAONI YA MHARIRI: Mbeleko ya bosi wa Fifa iwe maana, manufaa

Rais wa FIFA Gianni Infantino

Muktasari:

Wazo hilo la kuwa na timu 40 kwenye fainali za Kombe la Dunia limekuwa moyoni mwa rais wa shirikisho hilo, Gianni Infantino tangu alipokuwa akiomba ridhaa ya kuongoza shirikisho hilo linalosimamia soka duniani.

Jana, gazeti hili lilikuwa na habari kuwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) linafikiria kuongeza idadi ya timu zinazoshiriki fainali za Kombe la Dunia kutoka 32 za sasa hadi kufikia 40 na kwamba katika ongezeko hilo bara la Afrika litaongezewa nafasi mbili zaidi.

Wazo hilo la kuwa na timu 40 kwenye fainali za Kombe la Dunia limekuwa moyoni mwa rais wa shirikisho hilo, Gianni Infantino tangu alipokuwa akiomba ridhaa ya kuongoza shirikisho hilo linalosimamia soka duniani.

Tunachukua nafasi hii kupokea kwa angalizo wazo hilo la Infantino, kiongozi aliyewezesha Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) wakati ule akiwa mtendaji mkuu wa shirikisho hilo kuwa na timu 24 kwenye fainali za bara hilo mwaka huu, Euro 2016 kule Ufaransa baada ya kuziongeza kutoka 16 zilizokuwa zikishiriki awali.

Tunajua Infantino atapingwa na wenzake Fifa kama ilivyotokea wakati akifikiria kuongeza idadi barani Ulaya, ambako kuanzia fainali za mwaka 2020, watacheza mashindano yao, Euro 2020 kwa mfumo wa ligi na kushirikisha nchi 13 zikiwa wenyeji wa fainali hizo, jambo ambalo linawezekana kuigwa Afrika.

Bosi huyo wa Fifa, pia alizungumzia mfumo wa kufuzu kwa nchi zinazowania nafasi hizo kuwa utabadilika, ingawa hakutaka kuingia kwa kina, amekuwa akipendekeza kwa mfano kutumiwa kanda, zitakazotoa mwakilishi wa kucheza fainali hizo.

Kwa kuangalia kiwango chetu, sisi Tanzania na ukanda mzima wa Cecafa (Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati), ndio bado ni dhaifu ikilinganishwa na Afrika Magharibi, Kaskazini na hata kusini, ambako Afrika Kusini ni imara kisoka.

Tunaamini, viongozi wetu wa masuala ya soka, likiwamo shirikisho la mchezo huo nchini, TFF watazinduliwa na azma hiyo ya bosi wa Fifa kuongeza nafasi mbili, wakitambua kuwa miaka 10 si muda mrefu wa kukaa chini na kusubiri baraka, badala yake watafute nafasi ya timu yetu, Taifa Stars ishiriki mashindano makubwa, yakiwamo Afcon ndani ya miaka michache ijayo kabla ya kufikiria Kombe la Dunia mwaka 2026 kwa sababu ya mbeleko ya bosi wa Fifa.

Tunasema, lazima mawazo yetu yawe kushiriki kwanza Afcon kwa sababu hata kwenye mashindano ya wachezaji wa ligi za ndani, Chan tumekuwa watazamaji tangu tuliposhiriki yale ya uzinduzi, mwaka 2009 kule Ivory Coast, ambako Taifa Stars iligeuzwa kichwa cha mwendawazimu.

Tunawashauri TFF na washirika wake, vyama vya soka vya mikoa, wilaya lazima wapokee mbeleko hii ya bosi wa Fifa kwa jicho la kushiriki mwaka 2026, lakini kama kutakuwa na mipango thabiti na endelevu ya kuhakikisha tunakuwa na timu za vijana za umri mbalimbali, ambazo zitashiriki mashindano ya kimataifa na kupata huko uzoefu.

Tunaamini, mashindano kama ya Airtel Rising Star, pia ya Rollingstone kule Arusha na ligi ya vijana chini ya miaka 20, zamani Uhai Cup, pia mashindano ya shule za msingi, sekondari, kwa maana ya Umitashumta na Umisseta, ambayo mwaka huu yalifutwa na Serikali kwa sababu wanazojua wao, lazima yote yafufuliwe haraka na kutoa jukwaa kwa vijana wetu wengi kuibuliwa vipaj vyao na kucheza wakishindana ili hatimaye tupate wale wanaoweza kuwa wawakilishi wetu wazuri wa Kombe la Dunia miaka 10 ijayo. Tunaweza, endapo tutakuwa tumedhamiria, kujipanga!