Mbinu bora za kuogesha mifugo

Uogeshaji wanyama kwa kutumia njia za kisasa zaidi. Picha na mtandao wa mprnews.org

Mfugaji anapoogesha mifugo yake kama vile mbuzi, kondoo, nguruwe, ng’ombe na wengine husaidia kwa kiasi kikubwa kufanya mazingira yanayowazunguka wanyama hao kuwa rafiki hasa kwa kuwa maficho au mazalia ya bakteria au wadudu yanapofikiwa na dawa huwa salama zaidi.

Kuogesha mifugo kuzuia kupe

Ili kuweza kuzuia kupe kikamilifu na hivyo kutoweza kuwashambulia mifugo na kuwaambukiza magonjwa mbalimbali, ni muhimu kuhakikisha kuwa wakati wa kuogesha, dawa imeenea sehemu zote za mwili wa mnyama na kwamba imeingia hadi kwenye ngozi na kulowanisha ipasavyo badala ya kuishia juu ya manyoya peke yake.

Nini cha kufanya kabla ya kuanza kuogesha? Kabla ya kuanza kuogesha kama ni ng’ombe, hakikisha amefungwa vizuri au awekwe moja kwa moja kwenye kibanio na bomba au pampu litakalotumika kupuliza dawa ifanyiwe majaribio ili kuhakikisha kuwa inafanya kazi vizuri.

Changanya dawa ya kuogesha pamoja na kiasi maalumu cha maji kilichopendekezwa na mtaalamu au mtengenezaji wa dawa husika.

Mwogeshe ng’ombe nje au mbali kidogo na banda mahali ambapo dawa inayotumika haitaweza kuruka na kuingia kwenye malisho au maji ya kunywa.

 Njia za kuondoa kupe mwilini

Zipo njia za zamani na nyingine za kisasa ambazo huweza kutumika kuzuia au kuondoa kupe mwilini mwa mnyama badala ya kuogesha. Iwapo njia hizi zitatumia vizuri na kwa umakini, zinaweza kusaidia kupigana na magonjwa yanayoambukizwa na kupe.

Njia hizo ni mosi  uondoaji wa kupe kutoka mwilini mwa ng’ombe kwa kutumia mkono ambayo hufanywa na baadhi ya wanafamilia za wafugaji katika baadhi ya nchi duniani. Uondoaji wa kupe kwa njia hii ni rahisi na mazingira hayachafuliwi kwa kuwa hakutakuwa na madawa yaliyotumika.

 Hata hivyo njia hii huweza kuleta madhara iwapo haitafanywa kwa umakini na hivyo baadhi ya kupe kusalia mwilini mwa ng’ombe hasa wale wadogo.

Mbili, Kutumia dawa ambazo humwagwa mgongoni mwa mnyama kwa mchirizo kuanzia kichwa hadi kwenye shina la mkia. Licha ya kuzuia kupe, dawa za aina hii hufukuza pia mbung’o, inzi na wadudu wengine wanaoweza kusumbua ng’ombe.

 Dawa za aina hii zinaweza kutumiwa mara moja tu katika kipindi cha majuma mawili tofauti na zile za kuogesha ambazo mfugaji huhitajika kuwanyunyizia ng’ombe mara moja au mbili kwa juma kufuatana na wingi wa kupe katika eneo lake.  Baadhi ya wafugaji pia hutumia dawa za kupaka zilizotengenezwa kwa pareto kama vile py-grease kwa ajili ya kufukuza inzi na vile vile kuzuia au kuua kupe.

  Uzuiaji wa kupe utafanywa zaidi iwapo dawa hizi zitapakwa kwenye sehemu zinazofahamika kushambuliwa zaidi na kupe kama vile eneo la kuzunguka masikio, chini ya shina la mkia na kati ya miguu na kiwiliwili. Tatizo mojawapo la matumizi ya dawa hizi ni kwamba kupe huweza kujishika sehemu ambazo kwa bahati mbaya dawa haikupakwa.

 Zaidi ya hayo, katika maeneo yenye kupe wengi, inashauriwa kutokutumia dawa za aina hizi pekee kama kinga ya kuzuia kupe.

Kuogesha ng’ombe kwenye majosho ya uma yaliyojengwa mahususi kwa ajili ya uogeshaji huo. Faida ya kutumia majosho haya ni kwamba wafugaji walio wengi wanaweza kuogesha ng’ombe au mifugo yao kila mara bila gharama kubwa ambazo zingehitajika kwa ununuzi wa dawa na bomba au pampu la kuogeshea.

Pia,  majosho ya kuogeshea hayahitaji marekebisho ya mara kwa mara na matumizi yake huokoa dawa nyingi ambayo ingepotea bure kama vile mfugaji angetumia bomba au pampu kuogeshea wanyama nyumbani kwake.

Mashine za kuogeshea (spray race)  pia hutumiwa na baadhi ya wafugaji. Aidha mashine za uma ambazo pia zilikuwa zikitumika kuogesha zimepoteza umaarufu wake kutokana na ukweli kuwa imekuwa vigumu kununua spea na kuzifanyia matengenezo pale zinapoharibika.

 Mbali na hayo, uendeshaji wa mashine hizo ni wa gharama kubwa ukilinganisha na njia nyingine za kuogeshea kama vile majosho. Kukoroga dawa na kutumia brashi kuogeshea. Wapo pia baadhi ya wafugaji ambao wamekuwa wakitumia njia hii kuogesha mifugo yao kutokana na ukosefu wa fedha kwa ajili ya kununua pampu au bomba kwa ajili ya kuogeshea na wakati mwingine kutokuwepo kwa majosho maalumu ya kuogeshea katika maeneo yao.

 Baadhi ya wafugaji pia hukwepa moja kwa moja gharama za uogeshaji na kubaki kujiandaa vyema kwa ajili ya kutibu mifugo yao mara tu wanapoona dalili za maradhi kwa mifugo yao yanayotokana na kuambukizwa na kupe.

 Utaratibu huu si mzuri sana kwani mara nyingine huweza kusababisha kutokea kwa vifo vya wanyama kwa wingi na kwa ghafla kutokana na gharama za madawa na hata malipo kwa wataalamu wa mifugo watakaotumika kutibu mifugo hiyo.

Njia zingine za asili zinazoweza kutumika kuzuia kupe

Moja, tumia unga wa diatomite, ambao ni unga mweupe unaotokana na diatomaceous kudhibiti              kupe. Chembechembe zake kali husambaa katika mwili wote wa mdudu na kunyonya majimaji yote mwilini.

Kukosekana kwa maji mwilini husababisha mdudu kufa. Kutokana na sababu kuwa unga huo husambaa katika mwili wote na kunyonya maji yote, ni vigumu kwa mdudu kujitengenezea kinga kwa wakati huo na ndiyo maana hufa.

Mbili, chukua     gramu 250 za maua yaliyokauka ya pareto, weka kiasi kidogo cha maji kisha tia kwenye kinu na twanga. Baada ya kumaliza, weka maji hadi kufikia lita 10 na chemsha kwa dakika 20. Epua na uiache kwa muda wa saa 12 kisha nyunyizia mifugo yako.

 Tatu unaweza kuchukua gramu 250 za maua ya pareto yaliyokauka, weka maji lita 10 , peleka katika chumba cha giza na uache kwa muda wa saa 12 kisha tayari kwa kutumia kuitibu mifugo yako.

Nne, chukua kilo moja ya majani mabichi ya tumbaku, tumbukiza katika maji lita 10 kisha iache kwa muda wa dakika tatu.
Chukua kitambaa safi na tumia kumpaka ng’ombe. Kwa ng’ombe mmoja, lita 5 zinatosha.