Mbinu tano za kushirikiana vizuri na wafanyakazi wenzako

Muktasari:

  • Kukosa amani kazini kunaweza kukuondolea ujasiri na uchangamfu wa kuchangamana na wenzako. Hali hii, kwa kiasi kikubwa, inaweza kupunguza ufanisi wako kazini.

Migogoro na wafanyakazi wenzako inaweza kuwa sababu moja wapo ya kukosa ari ya kazi. Unapokuwa na watu wengi ofisini kwako wasiofurahia kukuona; watu wanaokerwa na kazi nzuri unazozifanya; watu wanaokuonea wivu; watu wanaojenga uadui na wewe, ni rahisi kukosa amani na mazingira ya kazi unayoifanya.

Kukosa amani kazini kunaweza kukuondolea ujasiri na uchangamfu wa kuchangamana na wenzako. Hali hii, kwa kiasi kikubwa, inaweza kupunguza ufanisi wako kazini.

Kama ilivyo mitaani, wapo watu kazini huwezi kuwaridhisha. Unaweza kufanya jitihada za kuwatendea yaliyo mema lakini bado wakakuchukulia kama adui. Lakini, hata hivyo, si mara zote watu hujenga chuki na wewe kwa sababu tu hawakupendi. Wakati mwingine, tabia ulizonazo zinaweza kuchochea hisia za wivu, uadui na hata mashindano yanayoweza kuathiri mahusiano yako na watu.

Katika makala haya, tunajifunza tabia tano zitakazokusaidia kuwa na uhusiano mzuri na wafanyakazi wenzako.

Kubali kuzidiwa

Kupenda kuwazidi wengine ni moja wapo ya misukumo iliyojificha nyuma ya mengi tunayoyafanya. Tunapojiona tuna hadhi ya juu kuliko wengine, hiyo peke yake inatosha kutupa namna fulani ya utoshelevu.

Kazini watu hushindana kimya kimya kwa viwango vya elimu; utendaji wa kazi; tija waliyoiletea taasisi na mambo mengine kama hayo. Unapoingia kwenye mfumo wa kazi, unajikuta bila wewe kujua, ukiwa sehemu ya mfumo huu wa mashindano yasiyo rasmi.

Ukikubali kuingia kwenye mashindano haya, utajitengenezea mazingira ya kupishana na watu bila sababu. Utajikuta ukiongea kama mtu anayejua kila kitu. Utashauri mahali ambapo ushauri wako haujaombwa. Utafanya mambo kwa papara ili tu uonekane unaweza. Hutakuwa tayari kujifunza kwa wengine. Haya yote yatakutengenezea ufa wa kimahusiano kati yako na wenzako na utajiweka kwenye hatari ya migororo isiyo na sababu.

Siri ni kuwafanya watu waone wanakuzidi. Weka mazingira ya kuomba msaada kwa watu wanaokuzidi uzoefu. Fanya hivyo kwa uangalifu bila kuwafanya watu wawe na wasiwasi na uwezo wako. Sambamba na hilo, usiwe mwepesi wa kushauri kama ushauri wako haujahitajika.

Badala yake jenga weledi utakaowafanya watu wakufuate wenyewe kwa ushauri. Ukiweza kufanya hivyo, watu hawatakuwa na sababu ya kukuonea wivu, kushindana na wewe.

Kubali kuwa ngazi

Kila mfanyakazi ana dira inayoongoza shughuli zake kazini. Lakini pia, kila mfanyakazi ana malengo yake binafsi. Jambo la kuzingatia ni kuwa wakati mwingine malengo yetu binafsi yanaweza kuingilia na malengo ya mwingine na kusababisha mitafaruku.

Usifanye kosa kuonyesha wazi wazi kuwa unachoangalia wewe ni malengo uliyonayo binafsi. Watu wakigundua unafikiria maslahi yako mwenyewe, watajitenga na wewe kimya kimya.

Badala ya kuwatumia watu kufikia malengo yako, fikiria namna unavyoweza kuwa ngazi ya wenzako kufikia malengo yao. Chukulia, kwa mfano, umebaini kuna mwenzako anapata shida kuandaa ripoti na wewe ujuzi huo unao. Jitolee kumsaidia afanikiwe. Ujisikie vibaya kuwa atafanikiwa. Kufanikiwa kwake, kutakuwa akiba kwako. Siku nyingine mtu huyo huyo atajisikia kudaiwa fadhila kwa kukusaidia na wewe.

Kubali kuanzia chini

Wafanyakazi wapya huwa na matumaini makubwa. Wengi wetu huwa na ndoto za kulipwa mishahara minono itakayobadilisha maisha yetu ndani ya muda mfupi.

Ukiacha kipato, kuna mambo ya vyeo. Wafanyakazi wapya hufikiri ni rahisi kukwea ngazi na kupewa madaraka makubwa kirahisi. Wasichojua ni kuwa viongozi wanaowaona sasa kazini, wamefanya kazi kwa muda mrefu kufikia hatua ya kuaminiwa.

Fikra kuwa unaweza kuanzia juu zinaweza kukuingiza kwenye matatizo kazini. Kwanza, utakosa uvumilivu wa kufanya kazi chini ya watu wengine kwa kujiona una sifa za kutosha kukupandisha juu kimamlaka. Fikra hizi zinaweza kuzaa misuguano isiyo ya lazima na wenzako kazini.

Unahitaji kuwa mtu wa subira. Jizuie kujipatia sifa za haraka haraka. Ukweli ni kwamba mafanikio yoyote kazini ni matokeo ya jitihada na bidii zinazoweza kuchukua muda kulipa. Kila aliyefanikiwa leo, alianza chini. Ili ufanikiwe unahitaji kuwa na subira.

Linda heshima ya wenzako

Mazingira ya kazi hayakosi watu wanaopenda kueneza maneno ya watu. Utakaa na mtu unayemheshimu wakati wa chai kisha ataanzisha mazungumzo yanayomhusu mtu asiyekuwepo kwenye mazungumzo hayo. Nani anatoka nani. Nani hawezi kazi. Nani ni swahiba wa bosi na mambo kama hayo.

Mazungumzo kama haya yanaitwa majungu. Lengo, mara nyingi, ni kubomoa hadhi za watu wengine. Wakati mwingine mambo haya hulenga kuimarisha makundi ya kimaslahi kazini.

Unahitaji ukomavu kufanya kinyume. Jenga utaratibu wa kulinda heshima ya wenzako hata wanapokuwa hawapo kwenye mazungumzo. Unaposikia habari mbaya za mfanyakazi mwenzako, usiwe mwepesi kushabikia. Habari mbaya zilizobomoa heshima ya mwenzako hazikusaidii kuongeza ufanisi wako.

Badala ya kushabikia mazungumzo yanayomharibia mwenzako asiyekuwepo, tafuta jambo jema na liseme kwa ujasiri. Ukijenga tabia ya kuwatetea wenzako, unajijengea heshima yako. Watu watakuheshimu. Unapokwepa kuwa sehemu ya makundi yanayofuga ‘siasa’ za maslahi kazini, utajenga kuaminika kazini. Mbinu chafu zinaposukwa dhidi yako, utakuwa na watu watakaokuwa tayari kukutetea.

Ruhusu watu wakukosee

Wapo watu ambao kwa vyovyote vile wanaweza kuwa kinyume na wewe. Unaweza kujitahidi kuishi vizuri na watu, kwa kusimamia haki lakini bado wakawepo watu watakaochukulia wema huo kama sababu ya kukosana na wewe.

Hali hii isikuvunje moyo. Jichukulie kama binadamu anayeweza kuchukiwa bila sababu na mtu yeyote. Jichukulie kama mtu anayeweza kufanyiwa visa na watu wenye kutumia mbinu chafu kufikia malengo yao. Ukielewa hivyo, hutapata shida unapogundua kuna watu wanakuzunguka.

Kufanya hivyo, hata hivyo, haimaanishi kukubali kuonewa bila sababu. Hapana. Ni ule ukomavu wa kikazi unaokufanya uwe tayari kufanya kazi na watu wasiokupenda bila kuathiri kazi zako.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. http://bwaya.blogspot.com , 0754 870 815