Mbinu ya kuchagua kazi itakayokupa utoshelevu

Friday September 29 2017

 

By Christian Bwaya, Mwananchi [email protected]

Uamuzi wa kazi gani ufanye ni moja wapo ya mambo ya msingi yanayoathiri maisha ya mtu.

Kazi iwe ya kujiajiri au kuajiriwa ndiyo maisha yako.

Muda unaoutumia ukiwa kazini unaweza kuwa mwingi kuliko unaoutumia ukiwa kwingineko.

Maana yake ni kwamba unapofikiri kazi ipi uifanye kimsingi unafanya uamuzi utakaoathiri mfumo mzima wa maisha yako.

Uamuzi sahihi utakufanya uridhike zaidi na uwe mtu mwenye furaha na matumaini.

Uamuzi mbaya kwa upande mwingine, unaweza kukusababishia kukata tamaa ya maisha.

Ni dhahiri kufanya uamuzi wa kazi ni changamoto kubwa kwa sababu mara nyingi ni rahisi kuongozwa na msukumo wa nje.

Makala haya yanatathmini baadhi ya sababu unazoweza kuzitumia kufanya uamuzi unaohusu kazi.

Uzingatie kile unachokipenda?

Ukimsikiliza kijana anayefikiri afanye nini baada ya masomo yake, mara nyingi sababu anayoitoa ni mapenzi aliyonayo na kitu fulani.

Mfano, kijana anakwambia anataka kuwa mwanasheria, injinia, rubani, daktari kwa sababu hicho ndicho kinachomvutia.

Hata hivyo, changamoto ni kwamba, mambo yanayotuvutia hubadilika kulingana na umri.

Kila hatua ya maisha anayopitia binadamu hutengeneza mahitaji mapya ya kimaisha yanayoweza kubadili mambo yanayomvutia.

Kuna umri kwa mfano, anaweza kujikuta anavutiwa na vitu visivyo halisi.

Mashujaa unaowasikia kwenye vyombo vya habari, masimulizi unayokutana nayo mitaani, yanaweza kukufanya ukatamani kufanya kitu fulani kwa sababu tu umesikia kitu hicho kipo.

Leo unaweza kufikiri unapenda kuwa rubani na kurusha ndege ndiyo yakawa maisha yako.

Hata hivyo, shauku ya kuwa rubani inaweza kuwa imetokana na matamanio ya sifa tu ya kufanya kazi ya kipekee.

Kesho, kadri anavyokutana na uzoefu mpya, mvuto huo wa kurusha ndege unaweza kuhamia kwingine.

Kwa kuwa ni vigumu kujua atapenda nini kesho, kufanya uamuzi wa kazi ipi ufanye kwa kuangalia unapenda nini inaweza kuwa kosa la kiufundi.

Uige wanachofanya wengine?

Kwa namna fulani wapo watu wanaoathiri uamuzi wao. Wazazi, marafiki, watu tunaowaona kwenye vyombo vya habari wana nguvu ya kujenga ushawishi fulani kwenye maisha ya mtu.

Kuna uwezekano mkubwa, mtoto wa mwalimu naye atakuwa mwalimu. Mtoto wa daktari anaweza kuwa daktari kama mtoto wa mwanasiasa naye anaweza kuwa mwanasiasa.

Pia, marafiki ulionao nao wana nafasi kubwa ya kuathiri mitazamo yako.

Unapoona wanafanikiwa kwenye eneo fulani la kimaisha, upo uwezekano na wewe ukatamani kujaribu eneo hilo.

Changamoto ni kwamba, kila mtu ana upekee wake. Si kila kinachofanywa vizuri na wengine na wewe unaweza kukifanya kwa uzuri ule ule.

Uamuzi wako wa kazi ukiathiriwa na yale tunayoyaona kwa watu wengine uwezekano wa kutokufanya vizuri ni mkubwa.

Ukubwa wa mshahara?

Nilipokuwa shuleni niliota kupata kazi itakayonilipa fedha nyingi.

Nilifikiri kazi yenye kipato kikubwa ndiyo mafanikio kwenye kazi.

Ndivyo wanavyofikiri vijana wengi wanaoanza maisha.

Hata hivyo, utoshelevu wa kazi ni zaidi ya kipato. Ingawa ni kweli moja wapo ya sababu kwa nini tunafanya kazi ni kujipatia kipato, ni dhahiri kipato si sababu pekee.

Wapo watu wengi wanaopata kipato kikubwa lakini bado wanalamikia kazi zao.

Wengine wanaacha kazi zenye kipato kikubwa na kwenda kufanya kazi tofauti ikimaanisha kuwa kipato kikubwa si sababu inayotosha kuridhisha nafsi zao.

Unapofanya uamuzi wa kazi ukilenga kuwa tajiri pekee, unaweza kuishia kuwa mtu mwenye huzuni.

Pamoja na uzuri wa kuwa na fedha, bado kuna ukweli kwamba mafanikio yako kazini ni zaidi ya hitaji la kupata fedha.

Kugusa maisha ya watu?

Kulenga kugusa maisha ya watu ni kufanya kazi inayowanufaisha watu wengine.

Kwenda mbele ya mahitaji yako binafsi na kutumia ujuzi na muda wako kuangalia watu wengine wanahitaji nini kutoka kwako.

Changamoto kwa kizazi chetu, mara nyingi tunajiangalia sisi wenyewe na mahitaji yetu.

Tunataka kufanya kazi zitakazotufanya tuwe bora kuliko wengine na hata kuwatumia watu kwa maslahi yetu.

Ingawa ni vigumu kufikiria mahitaji ya wengine kwa asilimia mia, unapojaribu kufanya hivyo kimsingi unajiwekea akiba ya kundi la watu linalokutakia mema.

Ufanye uamuzi gani?

Jambo la kwanza ni kujidadisi. Hapa nina maana ya kujaribu kujichunguza ili kujua kitu gani unakiona kwenye jamii ambacho wewe unaweza kuwa sehemu ya ufumbuzi.

Kwa vyovyote vile, ufumbuzi wa tatizo huhitaji ujuzi.

Ikiwa unataka kuwatetea watu wanaonyang’anywa haki zao kwa mfano, ukiwa na ujuzi wa sheria au uandishi wa habari, itakuwa rahisi kufikia malengo yako.

Changamoto kama nilivyotangulia kusema, kile unachofikiri unaweza kukifanya leo, si lazima ukifanye kesho kwa sababu maisha yanabadilika.

Hata hivyo, tofauti na mtu anayeamua kuwa mwanasheria ili awe tajiri au maarufu, wewe utajifunza sheria ili uweze kutatua tatizo fulani unaloliona kwenye jamii inayokuzunguka.

Kutatua tatizo la mtu mwingine, ni utoshelevu usiobadilika. Katika kila hatua ya maisha yetu, sote tunatamani kuwa watu wenye manufaa kwa wengine.

Haya ndiyo matamanio ya kila mwanadamu anayejitambua.

Haitoshi kuwa na ujuzi fulani. Lazima kuutumia ujuzi huo kutatua matatizo halisi.

Utumie ujuzi huo kufanya kazi itakayopunguza tatizo unalofikiri linaisumbua jamii.

Hii ndiyo siri kubwa ya uamuzi bora wa kazi utakaokupa utoshelevu. Kutatua matatizo halisi yanayowasumbua watu wa jamii yako. Nenda katatue tatizo ambalo pengine limepuuzwa na jamii.

Kadri unavyotatua tatizo hilo, ndivyo thamani yako itakavyoongezeka na ndivyo utakavyoendelea kufurahia kile unachokifanya.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754870815

Advertisement