Mbinu za kufanikiwa ujasiriamali kujifunza na kusonga mbele

Muktasari:

Hizi ni fursa za kuwekeza na kufanya biashara za aina mbalimbali. Hata hivyo, kuna umuhimu wa kuelewa mambo ya msingi kuhusu fursa kwa wajasiriamali wa aina zote.

Katika siku za hivi karibuni neno fursa limekuwa likitumika sana hasa katika muktadha wa ujasiriamali. Kati ya mambo yanayosisitizwa ni kutafuta, kuona na kuchangamkia fursa za ujasiriamali.

Hizi ni fursa za kuwekeza na kufanya biashara za aina mbalimbali. Hata hivyo, kuna umuhimu wa kuelewa mambo ya msingi kuhusu fursa kwa wajasiriamali wa aina zote.

Yapo mambo muhimu kuhusiana na dhana ya fursa yanafanyiwa uchambuzi kwa mitizamo ya kiuchumi na kibiashara kwa lengo la kuelemisha na kushauri ili kuboresha juhudi za wajasiriamali.

Dhana ya fursa

Dhana ya fursa ni pana. Kimsingi inamaanisha uwezekano wa kutumia mazingira yaliyopo kwa manufaa. Katika ujasiriamali dhana ya fursa inatumika kuzungumzia uwapo wa vitu au hali itakayoweza kuleta manufaa ya uwekezaji na biashara kwa wajasiriamali.

Ni muhimu kuelewa kuwa fursa ni uwezekano wa mjasiriamali kufaidi na siyo faida yenyewe. Ili kuzifaidi fursa zilizopo ni lazima juhudi zifanyike kuzibadili na kuwa katika hali ya kunufaisha.

Ujasiriamali Tanzania

Ni muhimu kwa wasomaji na wadau wa ujasiriamali kuelewa historia ya fursa zilizopo Tanzania leo hii. Hali halisi ya fursa imekuwa ikibadilika kulingana na mifumo ya kiitikadi ya nchi.

Kuna vipindi viwili muhimu sana kuhusu fursa katika historia ya uchumi wa Tanzania. Kipindi cha kwanza ni miaka ya 1967 hadi katikati ya miaka ya ya 1980. Hiki kilikuwa kipindi cha uchumi hodhi kufuatia Azimio la Arusha la mwaka 1967 na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea iliyoambatana nalo.

Njia kuu za uchumi kama viwanda, mashamba makubwa, migodi, benki na taasisi za uzalishaji wa huduma na bidhaa zilikuwa chini ya Serikali. Sekta binafsi haikuwa na nafasi katika uchumi wa nchi kama ilivyo leo. Kwa maana hiyo ujasiriamali haukuwa na nafasi kubwa hivyo fursa zilizokuwapo hazikutumika kijasiriamali

Katikati ya miaka ya 1980 Tanzania ilifanya mageuzi ya namna ya kuendesha uchumi wake. Mabadiliko haya yalitokana na mitizamo na itikadi mpya za kiuchumi duniani.

Pamoja na mambo mengine, taasisi duniani mfano Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) zilishinikiza baadhi ya nchi ambazo hazikuwa nao, kuanzisha uchumi wa soko huria ambao unaendeshwa kwa nguvu za soko.

Katika uchumi huu sekta binafsi inamiliki na kuendesha shughuli kuu za uchumi. Kuanzia katikati ya miaka ya 1980 hadi sasa kumekuwapo na fursa nyingi za uwekezaji na biashara. Hii inaonyesha kuwa fursa zinaendana na mfumo na itikadi ya nchi husika.

Aina za fursa

Fursa zipo za aina mbalimbali kutegemeana na anayeziangalia. Zipo fursa za muda mfupi, wa kati na mrefu. Pia zipo fursa ndogo, za kati na kubwa. Fursa nyingine ni zile za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Ni muhimu kwa wajasiriamali kuona wanajihusisha na fursa gani kati ya hizi. Fursa za muda mrefu lazima zipangiliwe tofauti na za muda mfupi. Hivyohivyo fursa kubwa lazima zitizamwe kwa jicho tofauti na fursa za kati au ndogo.

Zilipo fursa

Ni muhimu kwa wajasiriamali kutambua fursa zinapatikana wapi. Ni vizuri kuwa na mtizamo mpana katika jambo hili. Kwa Tanzania fursa zipo sehemu nyingi na ni za aina nyingi pia.

Zipo katika maono na matamanio ya nchi. Haya ni pamoja na Dira ya Maendeleo ya 2015; Mipango ya Maendelo kama ule wa 2016 – 2021; katika sera na mikakati, katika mipango na bajeti za kila mwaka.Inaweza pia kuwa kwenye changamoto za ukosefu wa bidhaa au huduma katika matukio mbalimbali kama kampeni za uchaguzi katika misimu ya mvua au kiangazi na sikukuu za kidini na elimu yakiwamo mahafali mbalimbali.

Cha kuzingatia

Kuna mambo kadhaa ya msingi ambayo wajasiriamali wanapaswa kuzingatia katika muktadha wa fursa. Jambo la msingi zaidi siyo uwapo wa fursa tu bali kuzitendea kazi fursa hizo.

Kati ya mambo muhimu katika kuzitendea haki fursa ni kuhakikisha zinatumika ipasavyo. Mjasiriamali hapaswi kupitwa na fursa zilizopo au zitakazojitokeza siku zijazo ila anapaswa kuzitafuta kwa sababu zenyewe haziwezi kumtafuta.

Mjasiriamali anapaswa wakati wote kukaa kimkakati huku akiwa makini na tayari kwa fursa zinazoweza kujitokeza muda wowote. Ni lazima mjasiriamali ajaribu bila woga huku akichukua tahadhari zote muhimu kupunguza uwezekano wa kupata hasara au kuepuka kabisa.

Lazima awe mbunifu na ajitofautishe na wengine katika kuzitafuta na kuzitendea haki fursa. Kunakili mawazo ya biashara na ujasiriamali ya wengine siyo ubunifu na ni jambo linaloweza kuufanya mradi anaotekeleza usiwe endelevu hivyo kuongeza haja ya kuwa wa kipekee kwa ushindani wa hali ya juu.

Mambo mengine ya msingi ya kufanya ni pamoja na kuanza mara moja bila kusubiri kila zinapojitokeza fursa. Hii ni kwa sababu baadhi ya fursa hazikai muda mrefu na hazijirudii. Nafasi za pili ni chache sana na nafasi za tatu hazipo kabisa.

Uthubutu

Ni lazima mjasiriamali awe na uthubutu. Lazima awe tayari kuanguka na kuinuka kila mara itakapotokea hivyo kabla hajatimiza ndoto yake. Katika hili, ni muhimu kufahamu kuwa mjasiriamali lazima ajiinue kutoka kwenye maanguko yake kisha asonge mbele.

Ni muhimu kukumbuka ukubwa wa ujasiriamali haupimwi kuinuka kila unapoanguka ukiwa umejifunza jambo kutoka katika anguko lako na kusonga mbele. Vilevile ukubwa wa mjasiriamali haupimwi kwa kuwaangusha wengine bali kuwainua kila wanapoanguka.

Kubadilika

Mjasiriamali mzuri ni kama nahodha mzuri na makini ambaye hazami na meli yake. Katika ujasiriamali biashara zinaweza kwenda vibaya, kuanguka au kufa kabisa. Mjasiriamali hapaswi kuzama na kufa na biashara yake.

Wazo lake la biashara lazima libadilike kulingana na nyakati na mazingira.

Ni lazima awe tayari kubadilika na kunyumbuka kwa kadiri ya matakwa ya nyakati. Haifai kung’ang’ania wazo la biashara na fursa ambazo zimepitwa na wakati.

Mjasiriamali mzuri anaweza kupata hasara lakini anapaswa kuendelea baada ya kujifunza kutokana na maanguko anayoyapitia na hasara alizozipata. Ni muhimu kutizama na kutafuta kinachowezekana katika kinachooneka kutowezekana.

Mjasiriamali anapaswa kutizama kilichobaki na kuanza nacho badala ya kulalamikia kisichokuwapo au chenye kasoro. Katika ujasiriamali ni lazima kufikiria kwa namna chanya. Yote haya na mengine ya msingi yakizingatiwa wajasiriamali watafanikiwa.